Mwanza.
Siku moja baada ya kutokea mapambano ya zaidi ya saa 14 baina ya Jeshi
la Polisi na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi kwenye mapango ya
mlima ya Utemini, wananchi wa eneo hilo wameingiwa na hofu ya usalama
wao baada ya baadhi yao kuona wahalifu wakitoroka wakati wa tukio hilo.
Wananchi hao wana hofu kuwa majambazi waliotoroka wanaweza kurejea na kuwadhuru na tayari baadhi wameanza kuhama makazi yao.
Hofu
ya wananchi hao imekuja baada ya polisi kupambana na watu hao usiku wa
kuamkia juzi, wakitumia silaha kali zilizosababisha kizaazaa kwa wakazi
wa Utemini, kutokana na milio ya risasi na mabomu.
“Tuliwaona
wengine wakitoroka, kwa hiyo inawezekana kabisa wakarudi na kutudhuru
kwa sababu watadhani tumewachongea kwa polisi,” alisema mmoja wa
wananchi hao aliyejitambulisha kwa jina la Yeremia Mungula.
Mwenyekiti
wa Mtaa wa Utemini Ibanda, kata ya Mkolani, Jukael Kiula alisema baadhi
ya wananchi wanaoishi jirani na mapango hayo wameanza kuhama makazi yao
wakihofia kurejea kwa majambazi hao.
“Kwa
mujibu wa maelezo ya baadhi ya majirani, walikuwa wakiwaona watu
wakipanda na kushuka kutoka kwenye milima yenye mapango waliyojificha
watu hao. Lakini hawakuwatilia shaka wakidhani ni watu wanaopasua mawe,
hadi siku polisi walipopambana na majambazi hayo,” alisema Kiula.
Mwenyekiti huyo aliiomba Serikali kuimarisha ulinzi na doria kwenye mtaa huo ili kuwahakikishia usalama wananchi.
“Hata
ikibidi, askari wa Jeshi la Wananchi waweke kambi ya muda kwenye eneo
hilo kudhibiti vitendo vyovyote vya uvamizi,” alisema.
Akizungumza
na wakazi wa Utemini jana, mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Baraka Konisaga
aliwahakikishia kuwa Serikali itaimarisha ulinzi kudhibiti uwezekano wa
wahalifu kuendelea kutumia mapango hayo kujificha.
Konisaga
ambaye alitembelea eneo la tukio jana, aliwaomba wakazi kutoa taarifa
za maficho ya wahalifu pale wanapohisi kuna nyendo zinazotilia shaka.
Kamanda
wa polisi wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema kiama cha wahalifu kimefika
na kwamba tayari vyombo vya dola vimebaini mitandao ya uhalifu na
wahusika na itawasaka usiku na mchana.
“Hatutakuwa
na msalie mtume katika mapambano dhidi ya ujambazi Mwanza. Wote
wanaojihusha na ujambazi watambue kuwa yatawakuta yaliyowakuta wenzao
waliojaribu kupambana na polisi,” alionya Kamanda Msangi.
Mkuu
wa Mkoa, John Mongella alisema mkakati wa kuifanya Mwanzaa iwe salama
umeanza na hakuna mhalifu atakayeingia Mwanza na kutoka salama.