Dar
es Salaam. Kamanda wa Kanda Maalumu ya Kipolisi ya Dar es Salaam,
Kamishna Simon Sirro amesema kitendo cha askari kunyang’anywa silaha na
majambazi ni aibu na fedheha kwao na Jeshi la Polisi, akisema madhara
yake yanaweza kuwa makubwa kwa jamii.
Kamanda
Siro pia amesema tukio la uvamizi wa kituo cha polisi cha Stakishari
jijini Dar es Salaam na silaha kuporwa lilikuwa fedheha kwa Jeshi la
Polisi, lakini akabainisha kuwa halikuwa na viashiria vya ugaidi bali
ujambazi.
Kamanda
Siro, ambaye wakati wa tukio hilo alikuwa Msaidizi wa Kamishna wa
Polisi wa Kanda ya Dar es Salaam, amesema hayo katika mahojiano maalumu
na Mwananchi yaliyofanyika wiki iliyopita.
Kauli
ya Kamanda Siro imekuja wakati nchi ikiwa kwenye mapambano makali na
watu wanaodhaniwa kuwa majambazi ambao wana silaha kali, kiasi cha
kustahimili kupambana na polisi kwa zaidi ya saa kumi.
Akijibu
swali kuhusu matukio ya askari kunyang’anywa silaha yaliyotokea kwa
wingi mwaka jana, Kamanda Siro alisema ‘‘Yalikuwa aibu kwa askari na
Jeshi la Polisi kwa ujumla. Ni aibu kubwa,” alisema Kamanda Siro.
“Fikiria wewe ni kiongozi, unapata habari kwamba askari amenyang’anywa silaha, itakuwaje. Ni aibu kubwa kwa Jeshi la Polisi.
“Na
kuna athari mbili za kunyang’anywa silaha. Kwanza silaha hiyo inaweza
kutumika katika matukio ya uhalifu, lakini pili hujui itatumikaje.
Inaweza kutumika kwenye vikundi hatari. Silaha za Jeshi la Polisi ni
zile ambazo haziuzwi madukani.”
Alipoulizwa
alijisikiaje wakati watu wasiofahamika walipovamia kituo cha Stakishari
kilichopo Ukonga wilayani Ilala Julai 13 mwaka jana, Kamanda Siro
alisema ilikuwa fedheha kwa Jeshi la Polisi.
“Unapokuwa
kiongozi halafu silaha ikichukuliwa, huwa ni tatizo kwetu na lazima
itakupa shida,” alisema mkuu huyo wa zamani wa operesheni za Jeshi la
Polisi.
“Ila namshukuru Mungu hatujapata changamoto kubwa.”
Alisema
wakati huo alikuwa msaidizi wa Kamanda wa Polisi wa Kanda ya Dar es
Salaam, Suleiman Kova na wakati wa tukio alikuwa likizo.
“Lakini niliitwa kazini kutokana na tukio hilo. Lakini tulibaini baadaye kuwa ulikuwa ni ujambazi.”
Tukio la Stakishari lilikuwa miongoni mwa matukio kadhaa ya uvamizi wa vituo vya polisi mwaka jana.
Kabla
ya uvamizi wa Stakishari, majambazi walivamia na kukiteka kituo cha
polisi cha Ikwiriri kilichopo tarafa ya Ikwiriri, wilayani Rufiji,
mkoani Pwani na kuwaua askari wawili, kupora silaha saba na kisha
kulipua bomu. Pia walivamia kituo kidogo cha polisi cha Mngeta mkoani
Morogoro na kupora bunduki aina ya SMG na magazini moja yenye risasi 30.
Pia,
majambazi walivamia kituo kidogo cha Mkamba mkoani Pwani na kusababisha
kifo cha askari mmoja na mgambo. Pia, walipora silaha tatu aina ya shot
gun tatu, SMG mbili na magazini 30 kila moja ambazo zilikuwa kwenye
ghala la muda zikisubiri kupelekwa kwenye kituo kikubwa kwenye ghala kuu
la silaha.
Pia,
majambazi walivamia kituo kikuu cha polisi cha wilayani Bukombe mkoani
Geita mwaka juzi ambako askari wawili waliuawa na kujeruhi wengine
watatu.
Akizungumzia
hali ya kazi tangu ateuliwe kuongoza Kanda ya Dar es Salaam, Siro
alisema Jeshi la Polisi imepambana na watu takribani 100 waliokuwa
wakilitikisa jiji kwa uhalifu na ujambazi na kufanikiwa kuwadhibiti.
Amesema
kuwadhibiti watu hao hakuna maana kuwa polisi imemaliza kabisa matukio
hayo, bali inaendelea kupambana kuhakikisha Jiji linakuwa katika hali ya
usalama wakati wote, huku akieleza mambo saba yaliyofanyika kufanikisha
mkakati wake huo.
Sirro
alisema watu hao 100 walikuwa wakipora raia waliokuwa wanatoka benki,
kuvamia nyumba za watu na kupora na kujihusisha na biashara ya dawa za
kulevya.
Sirro,
ambaye aliteuliwa na Rais John Magufuli Februari 15 kuchukua nafasi ya
Kova aliyestaafu, alisema: “Tangu nimekaa hapa tumepambana na watu wengi
sana, ni watu zaidi ya 100 na hata bunduki tulizokamata ni nyingi.
“Wapo
wanaotangulia mbele ya haki na hao ni wengi maana walipambana na
polisi. Huwa nawauliza askari mtu mwenye bunduki unamkamataje? Stahiki
yake tunajua sisi tulioajiriwa kwa kazi hii.”
Kamanda huyo anayezungumza kwa kujiamini, amewahi kuwa Kamanda wa Polisi katika mikoa ya Tanga, Mwanza na Shinyanga.
Kamishna
Sirro alisema bunduki zilizokuwa zikitumiwa na baadhi ya majambazi hao
ni za kivita kama SMG, ambazo alisema zinapokamatwa wahusika hufikishwa
mahakamani na mahakama hutoa amri silaha hizo kurejeshwa serikalini au
kuteketezwa kama zitakuwa zimeharibika.
