
Dar es Salaam.
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inapenda kukanusha taarifa
zinazosambazwa kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii kuwa imetangaza
sifa na vigezo vitakavyotumika katika uchambuzi wa maombi ya mikopo ya
elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2016/2017.
Bodi
hiyo inapinga taarifa zinazosambazwa ambazo pamoja na mambo mengine,
zinaeleza kuwa sifa zitakazotumika kuwa ni ufaulu wa waombaji katika
mitihani yao ya elimu ya sekondari na diploma na kuwa maelezo rasmi
yanapatikana katika tovuti ya Bodi ya Mikopo na Tume ya Vyuo Vikuu
(TCU).
Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Jerry Sabi amesema taarifa hizo sio za
kweli na kuwaomba wadau wote wawe na subira wakati Bodi inakamilisha
taratibu za uombaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2016/2017.
Amesema
baada ya kukamilika kwa taratibu, mwongozo wa utoaji mikopo utatolewa
rasmi na kutangazwa kwa umma kupitia njia mbalimbali vikiwemo vyombo vya
habari na tovuti ya Bodi ya Mikopo (www.heslb.go.tz).
