
Dodoma.
Wabunge wengi wanajadili hoja nje ya muktadha kwani wengi hawafahamu
sawasawa namna ambavyo dhana ya ugatuzi wa madaraka (DBD) inavyofanya
kazi, Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene amesema.
Simbachawene
amesema hayo leo asubuhi wakati wa kipindi cha maswali na majibu
bungeni baada ya kubaini namna ambavyo wabunge wanavyojichanganya katika
suala hilo.
“Wengi
wanataka Serikali irudi kwenye mfumo wa Serikali Kuu kufanya kila
kitu…hii ina maana wengi hawaelewi maana ya DBD (ugatuzi wa madaraka),”
Simbachawene amesema kuna umuhimu ya wabunge hao kuandaliwa semina juu
ya suala hilo.
Amesema
Taasisi ya Uongozi itashirikishwa katika mafunzo hayo, jambo ambalo
limeungwa mkono na Naibu Spika Tulia Ackson aliyeitaka Serikali
kulitaarifu Bunge mara maandalizi yatakapokamilika.
Alipoulizwa
iwapo mafunzo hayo yataleta tija katika dhana nzima ya ugatuzi wa
madaraka, mtafiti kutoka Twaweza, Richard Lucas amesema mafunzo siyo
tatizo pekee bali Serikali inapaswa kuhakikisha ugatuzi unatendekea
katika Serikali za mitaa.
Akitolea
mfano namna bajeti zinavyotengenezwa kuanzia ngazi ya vijiji na fedha
zinazotengwa kwa ajili ya utekelezaji na uchangishaji wa madawati nchi
nzima, ofisa huyo amesema ni miongoni mwa masuala yanayodhihirisha
Serikali kuhodhi baadhi ya mambo ambayo ni kikwazo kwa utekelezaji wa
DBD.
“Kuna
hili suala la uchagiaji wa madawati nchi nzima, mimi nimetembea katika
shule kadhaa Kilimanjaro, suala hilo siyo tabu kwa shule nyingi, lakini
dhana ya DBD ingekuwa inatekelezwa hakika wengi wa wakazi wa mkoa huo,
kipaumbele kingekuwa siyo madawati, huenda kuna jambo tofauti
wanalohitaji tofauti na madawati,” ameeleza Lucas.
Mtafiti
huyo ameongeza kuwa iwapo wananchi wataibua miradi wanayoihitaji
kupitia dhana nzima ya ugatuzi wa madaraka, ni dhahiri itakuwa endelevu
kuliko ile inayotoka moja kwa moja Serikali Kuu.
