Moshi.
Mkazi wa Njiapanda ya Himo wilayani hapa, Daniel Mshana (41),
amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na kosa la
kufanya ngono na binti yake wa kumzaa.
Suala
hilo liligunduliwa na walimu katika shule aliyokuwa akisoma mtoto huyo
mwenye umri wa miaka tisa, baada kumuona siyo mchangamfu na ufaulu wake
darasani kuanza kuporomoka.
Kwa
mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani, baada ya mtoto huyo kuonyesha
hali hiyo, mwalimu wa darasa alimhoji na ndipo alipoeleza mkasa mzima
na suala hilo kufikishwa polisi.
Mshtakiwa
alikuwa akiishi nammtoto wake huyo baada ya kutengana na mkewe ambaye
aliondoka na watoto wawili wadogo na kumwacha binti huyo na baba yake.
Hukumu
hiyo ilitolewa Ijumaa iliyopita na Hakimu Mkazi wa Mkoa Kilimanjaro,
Anthony Ngowi aliyesema kitendo alichokifanya mshtakiwa ni kibaya
kisichopaswa kufumbiwa macho na jamii.
Awali,
Wakili wa Serikali Kanda ya Moshi, Ignas Mwinuka alidai mahakamani hapo
kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo kwa tarehe tofauti kati ya Oktoba na
Novemba 23, 2015.
Alidai kosa alilolitenda mzazi huyo ni kinyume cha kifungu cha 158 cha kanuni za adhabu.
Kifungu
hicho kinasema mwanamume yeyote anayefanya mapenzi na mjukuu au mtoto
wake, dada au mama yake anatenda kosa la kufanya mapenzi na maharimu
(incest by male).
Akitoa
hukumu hiyo, Hakimu Ngowi alisema ushahidi wa mashahidi sita akiwamo
mtoto mwenyewe, daktari na walimu umeithibitishia Mahakama kuwa Mshana
alitenda kosa hilo.
Kabla
ya hukumu hiyo, Wakili Mwinuka aliiomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa
vile vitendo vya aina hiyo vinaanza kuongezeka nchini.