Dar
es Salaam. Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika, Kamanda wa
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro amesema kuna vikundi
vinavyowapeleka watoto porini na kuwapa mafunzo ya kigaidi.
Alisema
jeshi hilo liliwahi kumkamata mtoto wa miaka tisa, katika pori lililopo
wilayani Mkuranga, Pwani, aliyepewa mafunzo ya kigaidi na
kuwastaajabisha kwa kuwa na uwezo wa kuichambua silaha ya kivita.
Sirro
aliyazungumza hayo jana wakati wa ibada ya shukrani iliyofanyika katika
Kanisa la Katoliki Parokia ya Makabe Bikira Maria, katika kuadhimisha
Siku ya Mtoto wa Afrika.
Aliwataka
viongozi wa Serikali za mitaa kutoa ushirikiano, pindi wanaposikia
mzazi amemuachisha mtoto shule na kumpeleka porini kwa ajili ya mafunzo
ya kigaidi.
“Haya
mambo yanafanyika kwenye mitaa yetu, lakini kinachojitokeza kiongozi wa
Serikali ya mtaa anaposikia kuna mtoto wa fulani amejiunga kwenye
vikundi viovu, hawatoi ushirikiano kwa Jeshi la Polisi,” alisema.
Akiwa
katika maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na Kituo cha watoto wanaoishi
mazingira magumu cha Child in the Sun, Sirro alisema kuna kikundi
kimeibuka ambacho kinawachukua watoto wa shule na kuwapeleka porini, kwa
ajili ya mafunzo hayo ambayo alisema hayajengi nchi bali yanabomoa.
Padri
wa Parokia hiyo, John Maendeleo aliishauri jamii kuwajengea mazingira
mazuri watoto wao ili waweze kuepukana na vitendo vya kihalifu.
Padri
Maendeleo aliwataka wazazi wawajibike kwa watoto wao ili wasiingie
kwenye dhambi ya uvivu, kwa kumuweka mbele Mungu kwani watakuwa kwenye
maadili mema.
Wakati
huo huo, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imesema kutofanyiwa
marekebisho kwa sheria ya ndoa ya mwaka 1971, inayoruhusu mtoto wa kike
kuolewa akiwa na umri wa miaka 15, bado ni tatizo nchini.
Mkurugenzi
wa Haki za Binadamu, Francis Nzuki alisema kutoondolewa kwa kipengele
hicho ni changamoto, ingawa tatizo hilo linatatuliwa kwa mtoto kupelekwa
shule. “Sheria ya elimu inatatua changamoto hiyo ya kisheria, kwa
yeyote atakayekatisha masomo ya mtoto kwa namna yoyote kuchukuliwa hatua
za kisheria,” alisema.
Alisema
adhabu ya miaka 30 kwa atakayekatisha masomo au kifungo cha maisha,
imesaidia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa changamoto za ukandamizwaji wa
haki za mtoto ikiwa ni pamoja na kukosa nafasi ya kupata elimu.
Alisema kuongezeka kwa vitendo vya kikatili katika jamii kunasababishwa na kukosekana kwa elimu na umaskini katika jamii.
Mratibu
wa Shirika lisilo la kiserikali la World Vision, John Massenza alisema
kumekuwa na vitendo vya ubakaji na ulawiti wa watoto huku jamii ikiwa
kimya.
Alisema
Shirika la World Vision limekuwa mstari wa mbele kupigania haki za
watoto, lakini wamekuwa wakipata vikwazo kutoka kwenye jamii kufichua
maovu yanayotokea, hivyo kuihimiza kutoa taarifa kwa vyombo
vinavyohusika.
Imeandikwa na Pamela Chilongola, Colnely Joseph na Filbert Rweyemamu.
