» » Kuvibana vyama vya upinzani kunatia doa demokrasia yetu

ILI UPATE HABARI ZETU KWA URAHISI BOFYA HAPA KUINSTAL APPLICATION YA MZALENDO HURU KWENYE SIMU YAKO


Polisi wakimkamata mfuasi wa Chadema aliyekuwa akishiriki mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya DCT wilayani Kahama, Shinyanga wiki iliyopita. Mkutano ulivunjika baada ya polisi kupiga mabomu. Picha ya Maktaba 



Jeshi la polisi limesambaratisha mkutano wa hadhara wa Chama cha Demaokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kupiga mabomu ya kutoa machozi.
Kitendo hicho kimefanyika hivi karibuni katika mji wa Kahama mkoani Shinyanga ambako wafuasi wa chama hicho wakiongozwa na mwenyekiti wao, Freeman Mbowe walitaka kufanya mkutano wa uzinduzi wa Operesheni ya Okoa Demokrasia.
Chama hicho kilitaka kupaza sauti kupinga hatua wanazodai zinachukuliwa katika kuikandamiza demokrasia nchini na kuwanyima nafasi wapinzani.
Polisi waliingia katika eneo hilo la mkutano na kuanza kupiga watu huku wakifyatua mabomu ya machozi na kuusambaratisha mkutano huo.
Ilidaiwa kuwa baadhi ya watu waliopinga kitendo hicho walirusha mawe kwa polisi, lakini haikuwasaidia kuweza kufanya mkutano huo.
Tukio hili linatokea wakati katika nchi ya jirani ya Kenya kuna maandamano ya wafuasi wa upinzani kila Jumatatu.
Wafuasi hao wa upinzani wa Kenya wanadai Makamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Kenya waondolewe madarakani.
Wafuasi hao kutoka upinzani wanadai kwamba maofisa wa Tume ya Uchaguzi wanakipendelea chama tawala kwa hiyo hawataki wasimamie Uchaguzi Mkuu wa Kenya utakaofanyika mwakani.
Serikali ya Kenya ilijaribu kupiga marufuku maandamano hayo, lakini Mahakama Kuu ya Kenya ilikataa na kuruhusu yaendelee na kuwataka Polisi wachukue jukumu la kulinda amani.
Kimisingi hiyo ndiyo kazi ya polisi ya kulinda amani ili wananchi wapate fursa ya kutoa dukuduku lao kwa kufanya maandamano na mikutano ya hadhara kwa njia ya amani.
Polisi wapiga marufuku
Katika hatua ya kushangaza Jeshi la polisi Tanzania hivi karibuni limepiga marufuku maandamano na mikutano ya hadhara yote ya vyama vya siasa.
Polisi walitangaza hatua hiyo wakidai kwamba kuna viashiria vina vyoonyesha kutatokea uvunjifu wa amani iwapo mikutano ya hadhara itafanyika. Jeshi hilo lilieleza kuwa kuna hali inaonyesha kuwa pande mbili zinazohasimiana zinaweza zikaleta vurugu.
Polisi walieleza kuwa wanazuia mikutano hiyo ya hadhara kwa madai kuwa baadhi ya vyama vya siasa vina nia ya kuwaeleza wananchi wasitii sheria za nchi.
Katika mazingira ya Tanzania hakuonyeshi kwamba kuna dalili yoyote ya kutokea uvunjifu wa amani kwa vile hali ni ya amani na utulivu isipokuwa mauaji ya hapa na pale ambayo hayahusiani na sababu za kisiasa. Ni jukumu la polisi kuhakikisha kuwa ni lazima wimbi hilo la mauaji ya wananchi wasio na hatia, lakini jambo hilo halina uhusiano na mikutano ya vyama vya siasa.
Kazi ya Jeshi la polisi siyo kupiga marufuku kwani maandamano na mikutano ni utashi wa vyama vya siasa na wao haiwahusu, bali jukumu lao ni kulinda amani ili ifanyike bila madhara yoyote.
Ni makosa makubwa kwa polisi kujipa jukumu la wenyewe ndiyo waamuzi wa lini vyama vya siasa vifanye mikutano ya hadhara.
Hawana uhalali wa kupiga marufuku maandamano na mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, bali jukumu lao ni kutoa ulinzi kuhakikisha kwamba linafanyika kwa njia ya amani na utlivu.
Kama polisi inaona kuna watu wana nia ya kuleta vurugu kwenye mkutano wa chama fulani wao jukumu lao ni kuwadhibiti hao waleta vurugu na siyo kupiga marufuku mikutano.
Kupiga marafuku mikutano au na maandamno ya vyama vya siasa ni kuizuia demokrasia kuchukua nafasi yake na ni kinyume cha haki za binaadamu.
Watu wowote wale wakitaka kuandamana au kufanya mkutano wa hadhara hata kama wanataka kubishana kati ya kuku na yai ni nani aliyeanza wana haki ya kufanya hivyo na polisi kazi yao ni kuwalinda tu.
Kazi ya polisi siku zote ni kulinda amani, lakini siyo kutoa ruhusa ya kufanyika maandamano au mikutano ya hadhara.
Ni mtihani wa demokrasia
Uamuzi wa aina hii wa polisi unaleta taharuki katika nchi ambayo haikupaswa kuwapo kwani wananchi wanatakiwa wawe huru kutoa maoni yao almuradi hawavunji Sheria.
Siyo jambo la busara hata kidogo kwa polisi kuchukua hatua za namna hii ambazo zinakwaza demokrasia ambayo kwa Tanzania bado ina safari ndefu.
Hakuna haja ya kuwadhibiti watu wasifanye maandamano na mikutano ya hadhara kwa kisingizio chochote kile kwani kufanya hivyo ni ukiukwaji mkubwa wa demokrasia.
Tanzania itakuwa nchi ya kushangaza kama kila kitu kinapigwa marufuku hata matangazo ya moja kwa moja kwa njia ya Televisheni ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Sasa badala ya kupiga marufuku matangazo hayo ya Bunge sasa marufuku inakwenda katika vyama vya siasa hasa vya upinzani ili visipate nafasi ya kuwasiliana na wanachi.
Mtindo wa polisi kuvunja maandamano kwa nguvu kwa kutumia mabomu ya machozi na silaha nyingine ni wa hatari kwani kuna siku wananchi nao watachoka kufanyiwa vitendo hivyo na watakuja juu.
Itakapofika hatua hiyo hali ya amani na utulivu nchini itatoweka na ghasia kati ya wananchi na vyombo vya dola vitachukua nafasi yake jambo ambalo siyo zuri
ILI UPATE HABARI ZETU KWA URAHISI BOFYA HAPA KUINSTAL APPLICATION YA MZALENDO HURU KWENYE SIMU YAKO

About Mashak

About Mzalendo Huru Staff:

Send us your articles, questions, feedback, suggestions, press releases and all others to Whats app on +255657905751
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post