Mama mzazi wa Hoyce Temu
IMELDA MTEMA, Amani
Dar es Salaam: Familia ya Miss
Tanzania 1999, Hoyce Temu akiwemo mama yake mzazi, dada zake watatu na
mdogo wake, wamenusurika kupoteza maisha baada ya gari walilokuwa
wakisafiria, kupata ajali mbaya kwenye makutano ya Barabara za Ali
Hassan Mwinyi na ile ielekeayo kwenye Ufukwe wa Coco, Amani linakujuza.
Akizungumza kwa masikitiko, Hoyce
alisema ajali hiyo ilitokea mchana wa Jumapili iliyopita wakati
wanafamilia hao wakielekea Ufukwe wa Coco kwa ajili ya kupata chakula
cha mchana ambapo ghafla, gari jingine aina ya Range Rover Vogue,
lililigonga gari walilokuwemo ndugu zake na kuwasababishia madhara
makubwa.
Hoyce aliongeza kuwa alipata taarifa za
kupata ajali ndugu zake hao wakati akiwa Bagamoyo, Pwani kwenye kambi ya
watoto wenye ulemavu wa ngozi.
Mrembo huyo alisema kuwa alipigiwa simu
na dada yake mkubwa aitwaye Edith aliyekuwa kwenye ajali hiyo na
kumtaarifu kwamba wamepata ajali mbaya na hali ya mama yao siyo nzuri,
jambo lililomlazimu kurejea haraka jijini Dar es Salaam hadi Hospitali
ya Taifa Muhimbili walikokuwa wamelazwa.
Kwa mujibu wa mashuhuda, ajali hiyo
ilitokea baada ya kijana mwenye asili ya Kisomali, aliyekuwa akiendesha
Vogue, kuvunja sheria za barabarani kwa kuendesha kwa mwendo kasi na
kusababisha aligonge gari hilo, lililokuwa likiendeshwa na mdogo wa
Hoyce aitwaye Rachel.
Baada ya kufikishwa Muhimbili, majeruhi
wote walipatiwa matibabu ya awali na kulazwa kwenye Wodi ya Kibasila
ambapo wawili waliruhusiwa kutoka na wengine wawili, akiwemo mama yake
mzazi, walibaki hospitali.
“Kwa kweli ilikuwa ni ajali mbaya sana,
namshukuru Mungu kwani ningepoteza familia yangu yote na hapa bado
namuuguza mama yangu na ndugu zangu ingawa wengine wanae-ndelea vizuri,”
alisema Hoyce.
