Wanawake wanaojitoa mhanga nchini Nigeria wameanza kutumia watoto
kuepuka vizuizi vya ukaguzi, jambo ambalo, serikali nchini humo inasema
linaweza kuwa mwelekeo wa hatari.
Tahadhari hiyo imekuja baada ya wanawake wawili waliokuwa wamebeba
watoto mgongoni kufanya mashambulizi ya kujitoa mhanga katika mji wa
Madagali siku 10 zilizopita.
Januari 13 mwaka huu, wanawake wanne waliokuwa wakijitoa mhanga walifika
kwenye mji wa Maddaggalee katika jimbo la Adamawa, wawili walitambuliwa
na walinzi waliokuwa katika vizuizi na kutakiwa kusimama, baada ya
mbinu zao kugundulika.
Lakini wengine wawili walifanikiwa kupita bila ya kugunduliwa. kubeba
kwao watoto kulifanya wasigunduliwe na kuweza kusababisha maafa
yaliyosababisha vifo vya watu wanne, wao wenyewe kufariki na watoto
wawili pia waliokuwa wamewabeba katika mawili tofauti.
Kundi la Boko Haram linajulikana kwa kuwatumia wanawake, hususan
wasichana katika mabomu ya kujitoa mhanga, Hata hivyo ni mara ya kwanza
katika maasi hayo kutumia watoto wachanga.