Iringa. Waziri wa Nyumba, Ardhi na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi
amesema chanzo cha migogoro inayolikabili Taifa kwa sasa hususan
wakulima na wafugaji, imetokana na kukosekana kwa mipango bora ya
matumizi ya ardhi, huku viongozi wa serikali za vijiji wakibadilisha
matumizi bila kushirikisha wananchi.
Alitoa kauli hiyo wakati akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi hati 810
za kimila za kumiliki ardhi kwa wakazi wa Kijiji cha Kinywang’anga,
Wilaya ya Iringa mkoani hapa.
“Tumejifunza kutokana na uzoefu tuliopata, migogoro mingi ya ardhi
imetokana na baadhi ya viongozi wetu wa serikali za vijiji ambao
wamekuwa wakibadilisha matumizi ya ardhi bila kufuata utaratibu,”
alisema.
Lukuvi alisema Serikali haitasita kuwafuta kazi viongozi wa serikali za
vijiji watakaobainika kujihusisha kubadili mpango wa matumizi bora ya
ardhi za vijiji bila ya kushirikisha wananchi.
Alisema licha ya kuwaondoa kwenye nafasi zao, viongozi hao watakamatwa
na kufikishwa katika vyombo vya sheria kwa tuhuma za matumizi mabaya
ya madaraka.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi Msaidizi wa Shirika la Misaada
la Marekani (USAID), Dan Thompson alisema wanaendesha miradi ya aina
hiyo kwenye vijiji 41 vya mikoa ya Iringa na Mbeya kupitia Mradi wa Feed
the Future.