Muleba/Bunda. Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa amewashauri Watanzania wasipingane na misimamo ya Rais John Magufuli mpaka itakapofika mwaka 2020.
Alisema wakati huo utafanyika uchaguzi mkuu na ndio wanaweza kufanya uamuzi.
Akihutubia
viongozi wa chama hicho kutoka majimbo ya Muleba Kusini na Kaskazini
jana, Lowassa ambaye alikuwa mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015
kupitia Chadema alisema wanachama hao waache kubishana naye hadi
watakapokutana katika uchaguzi wa 2020.
Hata
hivyo, Lowassa ambaye pia aliwahi kuwa Waziri Mkuu, hakuitaja misimamo
hiyo ya Rais Magufuli lakini tangu aingie madarakani, kiongozi huyo wa
Awamu ya Tano ya Tanzania, ameweka msimamo mkali katika suala zima la
kubana matumizi ya Serikali, kudhibiti watumishi hewa, safari za ndani
na nje zisizo na tija na rushwa. Mambo hayo yamesifiwa na watu wengi.
Lowassa
aliwaeleza viongozi hao kuwa uchaguzi wa mwaka 2020 unaweza kuwa rahisi
zaidi huku akitaka wapinzani wapingwe kwa hoja na si kukandamizwa.
“Tupingane kwa hoja bila kuumizana na kutakiana mabaya, tuwasaidie wananchi wanaopata matatizo bila kuwapuuza,” alisema Lowassa.
Akizungumzia
sababu ya kutembelea Mkoa wa Kagera, Lowassa alisema ni pamoja na
kuwashukuru wananchi kwa kura walizompigia na kuwapa pole kwa tetemeko
la ardhi lililowakumba Septemba mwaka jana.
Kada
wa zamani wa CCM aliyeongozana na Lowassa, Hamis Mgeja, licha ya
kujivunia kukihama chama hicho alisema kwa jinsi mambo yanavyokwenda,
chama hicho tawala kinajifuta taratibu kwa wananchi.
Baadaye, Lowassa, alishiriki kampeni za kumnadi mgombea udiwani katika Kata ya Kimwani, wilayani Muleba.
Kuhusu uhaba wa chakula
Katika
mkutano huo wa ndani, Lowassa alizungumzia hali ya ukame inayoikabili
nchi na kusema kuna tishio kubwa la uhaba wa chakula hivyo kuitaka
Serikali isipuuze majanga yanayoweza kuwapata wananchi, bali iwasaidie
kwa kauli na vitendo.
“Wananchi wasipuuzwe, kuna tatizo la njaa kwenye baadhi ya maeneo ya nchi, kwa hiyo wananchi wasaidiwe,” alisema Lowassa.
Wakati
Lowassa akisema hayo Muleba, huko Bunda mkoani Mara, Mwenyekiti wa
Chadema, Freeman Mbowe alimtaka Rais Magufuli kuchukua hatua kukabili
hali ya upungufu wa chakula nchini.
Akihutubia
mkutano wa ndani wa viongozi wa chama hicho Jimbo la Bunda Mjini
uliofanyikia katika Hoteli ya Harieth, Mbowe alisema ni ukweli
usiopingika kwamba taifa linakabiliwa na uhaba wa chakula, hivyo ni Rais
Magufuli anapaswa akubaliane nao.
Mbowe
aliyetumia takribani dakika 12 katika hotuba yake, alisema ukali
anaouonyesha Rais kuhusiana na taarifa za uhaba wa chakula nchini unatia
shaka.
“Awasikilize
Watanzania waliomchagua kwani ndiyo waajiri wake. Wanaposema wana njaa
awasikilize na kuwasaidia. Kuna uhaba wa chakula... hili halina ubishi.
Ni wajibu wa Serikali kuchukua hatua za haraka,” alisema Mbowe.
Mbowe
alisema si kweli kwamba kuna uhaba wa chakula kutokana na uvivu wa
wananchi kwani wengi ni wachapakazi isipokuwa wamefikwa na hayo yote
kutokana na mvua kutonyesha kwa wakati.
“Njaa haijaletwa na uvivu wa Watanzania, bali imeletwa na ukame ambao uko nje ya uwezo wao,” alidai Mbowe.
Alizungumzia
pia hatua ya Serikali kubana matumizi akisema imechangia kwa kiasi
kikubwa kuongezeka kwa Deni la Taifa, kampuni nyingi kufungwa, kushuka
kwa mapato ya taifa na uwekezaji pamoja na umaskini miongoni mwa
Watanzania na kumtaka alegeze.
Awali,
Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya na Katibu wa Chadema Mkoa wa Mara,
Chacha Heche kwa pamoja walimwelezea mwenyekiti huyo kuwapo kwa uhaba wa
chakula mkoani humo na kumwomba alisemee.
Bulaya
alisema wakazi wengi wa wilayani Bunda wanakabiliwa na upungufu mkubwa
wa chakula kutokana na ukame sambamba na mazao yao kuharibiwa na wanyama
huku akisema watendaji wa Serikali hawataki kutangaza wakihofia
kuondolewa kwenye nyadhifa zao.
