Monday, December 12, 2016
WIZI wa punda umendelea kushamiri wilayani Simanjiro, huku polisi ikiwashikilia watu watatu baada ya kukutwa na ngozi 20 za wanyama hao.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Francis Massawe, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Bahati Patson (40), ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Kimosa Abdallah (41) na Hamis Salimu (36).
Alisema, watuhumiwa hao waliokamatwa juzi jioni ni wakazi wa Orkesumet na polisi wanaendelea na uchunguzi.
Alisema Bahati anadaiwa kushirikiana na watuhumiwa wengine kununua punda wa wizi.
Alidai kuwa watuhumiwa hao wapo kwenye mtandao wa kununua punda na kuwauza mikoa ya Dodoma na Singida.
Alisema siku ya tukio hilo walipata taarifa ya kuwapo kwa baadhi ya watu waliopo kwenye mtandao wa wizi wa punda, wamekusanya ngozi za punda na wanatarajia kuzisafirisha.
Alisema baadhi ya watuhumiwa walikimbia.
Aliwataka wananchi kulinda punda kwa sababu wanaachwa wakizagaa ovyo mitaani.
