Monday, December 12, 2016
NAIBU WAZIRI WA NCHI OFISI YA MAKAMU WA RAIS MUNGANO NA MAZINGIRA, LUHAGA MPINA.
MSAFARA wa Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mungano na Mazingira, Luhaga Mpina, umenusurika kutozwa ushuru wa maegesho wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na taasisi za Muungano Zanzibar.
“Alikuwa akitaka kulipwa ushuru wa maegesho lakini tayari amefahamishwa alikuwa hafahamu kama msafara wa Naibu Waziri.”alisema Afisa mmoja katika msafara huo.
Naibu Waziri Mpina alifika Idara ya Ardhi Zanzibar, kukagua mradi wa kutegeneza ramani mpya ya Zanzibar, unaofadhiliwa na Benki ya Dunia (WB) kupitia Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (Costech), kunakofanyika kazi ya upigaji wa picha kwa kutumia mashine za dirone, badala ya ndege.
Akiwa katika Kituo cha kulea wajasiliamali, Mpina alisema serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetumia Sh. bilioni 2.7 kufadhili miradi ya maendeleo ikiwamo ujenzi wa maabara ya utafiti wa mazao ya kilimo, mradi wa utafiti wa mbegu bora za muhogo, mpunga na viazi, mradi wa ramani mpya ya Zanzibar na kituo cha kulea wajasiriamali, visiwani humo.
Alisema kituo hicho kina umuhimu mkubwa katika kuongeza ajira kwa vijana kupitia wazalishaji wadogo na kufanikisha mpango wa kuondoa umasikini na kukuza uchumi kwa wananchi wake.
Alisema wakati umefika kwa vyuo vikuu kuwa na vituo kama hivyo vya kuwaendeleza vijana kwa kuwapatia ujuzi na baadae kujiajili kwa kuanzisha kampuni zao visiwani hapo.
“Kituo kama hicho pia kinahitajika kujengwa kisiwani Pemba na vyuo vyetu lazima viwe na vituo kama hivyo kutengeneza vijana wenye matumizi makubwa ya Sayansi na Teknolojia,” alisema.
Alisema gharama zinazotozwa kwa wanafunzi katika kituo hicho ni Sh 50,000 mpaka 100,000, ambazo ni nafuu ikilinganishwa na ujuzi wanaopata wa uzalishaji wa bidhaa kwa kutumia mashine pamoja na mafunzo ya kompyuta.
Kituo hicho kinatoa mafunzo ya uzalishaji wa bidhaa ikiwamo siagi, samri, sabuni za kuogea, juisi, mishumaa, maziwa ya mtindi, chizi pamoja na vyakula vya aina mbali mbali vinavyotokana na mazao ya kilimo.
