Tuesday, December 13, 2016
KOCHA MCAMEROON, JOSEPH MARIUS OMOG.
WAKATI Yanga juzi ikiangukia pua dhidi ya JKU kwa kukubali kipigo cha mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Uhuru, Simba jana imeangukia kidevu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam baada ya kuchapwa mabao 2-1 na Mtibwa Sugar ya Morogoro katika mchezo wa kirafiki.
Mtibwa Sugar ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya kwanza tu ya mchezo huo, mfungaji akiwa Stahmili Mbonde aliyefumua shuti kali lililompita kipa mpya kutoka Ghana, Agyei baada ya kufanikiwa kuwapiga chenga mabeki wa Simba.
Simba ilicharuka na kupeleka mashambulizi mengi langoni mwa Mtibwa Sugar kutaka kusawazisha, hata hivyo safu ya ulinzi ya Wakata Miwa wa Manungu iliyokuwa ikiongozwa na Salim Mbonde ilisimama imara kuzuia hatari zote.
Mtibwa Sugar ikafanikiwa kupata bao la pili dakika ya 34 mfungaji akiwa Jaffari Salum aliyewapiga chenga mabeki wa Simba baada ya kupokea pasi nzuri ya Ally Shomary na kumchambua Agyei tena.
Dakika mbili baadae Simba wakapata bao, dakika ya 36 lililofungwa na kiungo wa zamani wa Mtibwa, Mohamed ‘Mo’ Ibrahim kwa shuti la kushitukiza lililompita kwa urahisi, kipa Said Mohammed aliyekuwa amezubaa.
Kipindi cha pili, Simba iliongeza kasi ya mashambulizi langoni mwa Mtibwa, lakini bado wapinzani wao hao waliendelea kuwa makini katika kujilinda na hadi mwisho matokeo yalibaki kuwa 2-1.
