
Profesa Muhongo
SERIKALI ya Japan imetoa Sh bilioni 170 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu na kuweka vifaa vya huduma bora katika Kituo cha afya Murangi katika Jimbo la Musoma vijijini.
Fedha hizo zilitolewa jana na Balozi wa Japan nchini, Masaharu Yoshida ambaye alisema lengo ni kuiwezesha hospitali hiyo kutoa huduma stahiki kwa kila mwananchi.
Alisema fedha hizo zitatumika kuboresha miundombinu, kujenga nyumba za wauguzi, choo cha wagonjwa, shimo la kutupia kondo la nyuma na kurekebisha tanuru la kuchomea takataka za hospitali ikiwa lengo ni kuweka mazingira safi na salama kwenye kituo hicho.
Yoshida alisema suala la afya ni jambo la msingi kwa maisha ya binadamu.
Alisema msaada huo unatokana na ombi la Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo ambaye pia ni Waziri wa Nishati na Madini.
Yoshida alisema ikiwa kituo hicho kitafanyiwa marekebisho kitasaidia kuondoa usumbufu kwa wananchi waliokuwa wakisafiri umbali mrefu kutafuta huduma huku wauguzi wakiishi mbali na sehemu yanakofanyia kazi.
“Ninafuraha kubwa na ni heshima kwangu kusaini mkataba wa mradi huu mpya kupitia mfuko wa mpango wa miradi midogo kwa ajili ya usalama wa binadamu, hivyo basi tunatoa Sh bilioni 170 kwa ajili ya uboreshaji na ununuzi wa vifaa tiba.
“Tumepata taarifa wananchi wengi wanahudumiwa kwenye kituo hiki na wengine wanatoka mbali zaidi, naamini baada ya mradi huu kukamilika hudumu muhimu zitapatikana hapa na zitakuwa zinawasaidia wananchi wengi,” alisema Yoshida.
Alisema Japan itaendelea kutoa michango yake katika kusaidia kituo hicho cha afya kusaidia upatikanaji wa huduma mbambali.
Naye Profesa Muhongo alisema mradi huo utachukua mwaka mmoja kukamilika na kuwataka wananchi kuendelea kuwa na imani naye ikiwa ni pamoja na kushirikiana ili aweze kutimiza ahadi zake.
Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Anarose Nyamubi ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dk.Charles Mlingwa, alisema uboreshwaji wa kituo hicho utakuwa ni suluhisho katika kuboresha afya ya wananchi.
Alisema viongozi wengine wanapaswa kuiga mfano wa Profesa Muhongo kwa kufanya juhudi za kukutana na wadau mbalimbali katika kutaka kuwasaidia wananchi wanao waongoza.
