Rais wa Shirikisho la Soka nchini TFF, Jamal Malinzi amevitaka vilabu shiriki vya ligi hapa nchini kufuata taratibu na kanuni zinazowaongoza katika kubadilisha muundo wa umiliki wa klabu na viongozi ili kuweza kuepusha migogoro ndani ya vilabu vyao.
Malinzi amesema, vurugu nyingi katika vilabu vya ligi hapa nchini hutokana na watu mbalimbali ndani ya vilabu kuchukua maamuzi bila ya kufuata utaratibu unaotakiwa katika kubadilisha umiliki wa klabu pamoja na uongozi suala linalopelekea hata mgawanyiko wa wanachama ndani ya vilabu vya soka hapa nchini.
Malinzi amesema, zipo kanuni ambazo zinatoa maelekezo kwa vilabu iwapo vinataka kubadili kitu ndani ya Klabu lakini imekuwa kama mazoea kwa baadhi ya vilabu ambavyo wanachama wao huwa na maamuzi ya kufanya jambo wanaloliamua.
Malinzi amesema, vilabu vingi vimekuwa vikiwasimamisha kazi viongozi wao bila kuzingatia kanuni ambapo mwisho wa siku hutokea vurugu kubwa ambazo hufikia hatua hata ya kuigharimu timu.
