
Dar
es Salaam. Hakuna utafiti unaoonyesha hasa idadi ya wanaume wanaolelewa,
lakini kuna ushahidi wa kimazingira katika jamii ambao unazidi kushika
kasi.
Baadhi
ya vijana wamethibitisha kuwa jambo hilo lipo na kwamba ugumu wa maisha
na uvivu wa kufikiri au kutotaka kufanya kazi, umekuwa chachu ya
kushamiri kwa vitendo hivi.
Baadhi
ya vijana katika kijiwe eneo la Ilala Bungoni waliliambia gazeti hili
kwa sharti la kutotaja majina yao wala kijiwe chao licha ya kuwa
maarufu, kuwa ‘wanajibebisha’ na wakati mwingine wanapashana habari ili
kila mmoja anufaike na mwanamke anayejilengesha.
Mmoja
wa vijana hao aliyekuwa ameshika simu kali mbili na kifuani kwake akiwa
amening’iniza cheni ya dhahabu, alisema hajawahi kufanya kazi ila ana
‘kibosile’ mmoja anamtatulia na kuwezeshwa kuishi vizuri mjini.
“Ninaishi
vizuri, kama unavyoniona sijasoma sana lakini nafahamu jinsi ya kudili
na kina mama wanaopenda vijana watanashati, ”anasema huku akikataa
kutaja jina lake kwa madai ya kujiharibia kwa mademu wa makamu yake.
Dogo Boy (siyo jina lake halisi) mwenye umri wa miaka 29, anasema sababu kubwa ya kufanya hivyo ni ugumu wa maisha.
Anasema
vijana wengi hawana kazi akiwamo yeye huku familia ikimtegemea. “Katika
hali kama hiyo nipate mtu wa kunihudumia na kunipa mikwanja nimkatae
nife? ”anahoji kijana huyu.
Boy
anafafanua kuwa kina mama hao wanatambua thamani ya mtu na hujitoa kwa
moyo kuhakikisha mpenzi wake anamtatulia matatizo ya kifedha madogo
madogo. “Unaona gari hii, alinipa nilipokuwa nasheherekea siku yangu ya
kuzaliwa nilipokuwa natimiza miaka 28, na alinifanyia hiyo sherehe,
tangu nizaliwe wazazi wangu hawajawahi kunifanyia wala kunipa zawadi
hata inayogharimu Sh100,000 kutokana na ugumu wa maisha nimepata wa
kunitoa nikatae? ”anahoji Boy.
Kijana
aliyejitambulisha kwa jina moja Kolumba anasema licha ya kuwa na maisha
magumu, alipata msichana wa mtaani kwao, kabila la kwao pia na ni
mrembo, lakini alichomfanyia hana hamu na hataki tena wasichana.
Anasema
kwa kipato kidogo, aliongeza na fedha yake aliyolipwa kwenye kiwanda
fulani baada ya kuachishwa kazi, akamfungulia biashara ili iwasogeze,
lakini baadae aligundua kuwa binti huyo ana mpenzi mwingine.
“Nilimfuatilia,
siku niliyomfahamu mpenzi wake sikuamini kwa sababu alikuwa ni mtu
mzima kuliko mjomba wake aliyekuwa anaishi nae, ”anasema Kolumba.
Kolumba
anasema kuanzia hapo alichofanya ni kubadili utaratibu wa maisha ,
akipata fedha hununua nguo nzuri, manukato na kutengeneza mwili wake kwa
mazoezi ili awe na mvuto.
,“Huyu
niliye nae sasa ni wa tatu, siku za mwanzo nilikuwa naona ajabu, lakini
nimeshazoea na kuona ni kawaida, napata ninachokitaka mtaji wangu ni
kujiweka freshi tu, ” anasema.
Mpenzi
wa Kolumba ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake anasema ana kila kitu
fedha, watoto, magari, nyumba kadhaa, lakini hapati anachohitaji kutoka
kwa mumewe.
Anasema
ukiondoa ubize wa mumewe unaowafanya wasiwe pamoja muda mwingi, lakini
mumewe haoni umuhimu wa kushiriki nae baada ya kuwa na sista duu.
Anafafanua haiwezekani mwanaume akae na mkewe mwezi na zaidi bila kujuliana hali faragha.
Rajabu Hazron anasema ugumu wa maisha unachangia vijana kupenda ‘kulelewa’.
Anasema
mbali ya ugumu wa maisha, uvivu wa kufikiri na kupenda mafanikio ya
maisha kwa njia ya mkato matokeo yake ndiyo wanaangukia kwa hao wanawake
wenye msongo wa mawazo na wajane. “Hali hii ikiendelea baada ya muda
vijana wengi watakuwa na maradhi, kwa sababu wanachoangalia wao ni fedha
tu, hajali afya zao, wanaendeshwa kila wanachoambiwa kufanya
wanafanya,” anasema Hazron.
Andrew James anasema ugumu wa maisha ni kisingizio ukweli ni kwamba vijana wengi ni wavivu kufikiri.
“Vijana
kama hawa wakikosa wanawake wa kuwalea ndiyo wanajiingiza katika mambo
yasiyofaa kwenye jamii ikiwamo katika uhusiano wa jinsia moja kwa sababu
wana tamaa na wanaona mwili wao ndiyo chanzo cha kuwaingizia kipato,
”anasema James.
Kutotaka
kufanya kazi ni chachu ya kushamiri kwa vitendo hivi nchini, lakini
vina athari kwani vinaweza kuwa chanzo cha kupata Ugonjwa wa Ukimwi,
kufumaniwa na kudhuriwa au kuuawa.
