
Kuna kazi zinachukuliwa kuwa ni za wanaume tu hata inapotokea mwanamke anafanya huonekana mtu wa tofauti.
Etheldreder
Trecia Koppa (29), ni moja kati ya mabinti wachache ambao wameonyesha
uthubutu kiasi cha kufikia mafanikio ambayo ni nadra kufikiwa hata na
wanaume, huku akifaulu katika kazi iliyo mbele yake.
Hatua hiyo imemfanya Ethel afanikiwe kupata tuzo yake ya kwanza akiwa kama meneja wa mipango na ujenzi Afrika mwaka 2016.
Katika
mazungumzo yake mapema wiki hii, Koppa ambaye ni Meneja Programu wa
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), anasema tuzo aliyoipata hutolewa kwa
wanawake wote ambao wapo katika sekta ya ujenzi Afrika.
“Lilikuja tangazo, bosi wangu akalituma akitaka nishiriki nikajaza fomu akanisainia. Nakumbuka ilikuwa Februari,” anasema.
Anasema
awali alijua ameikosa nafasi hiyo, lakini baada ya miezi miwili
akapigiwa simu na kupata taarifa za kuteuliwa. “Wakanitumia kila kitu
ili niweze kushiriki katika hafla ya utoaji tuzo, nikashinda,” anasema.
Ethel
anasema ili kupata nafasi hiyo mhusika anatakiwa kuwasilisha wasifu
wake japokuwa pia wanangalia elimu, miradi gani amefanya na mchango wake
katika tasnia.
Akielezea
elimu yake anasema alihitimu Chuo Kikuu cha Ardhi shahada ya kwanza na
kufanya kazi kwa mwaka mmoja katika kampuni ya CQS Services na baadaye
alipata fursa ya kujiendeleza kielimu ambayo alikwenda kusoma shahada ya
Uzamili Chuo Kikuu cha Heriot Watt.
“Nilipohitimu nilipata kazi hapa shirika la nyumba, Machi 2014 kama Meneja Programu Msaidizi.”
Katika
ufanisi wake kuna changamoto nyingi anakutana nazo kama binti: “Fani
hii ni ya wanaume bado wanawake hawana mwamko, ninapambana sana kitu cha
kwanza unatakiwa kujiamini wewe na timu yako, unakuta katika timu nzima
mwanamke uko peke yako na wewe ndiyo Project Manager.”
“Hivyo
unawajibika katika kila kitu, unatakiwa kujiamini ili ukamilishe kazi
na unatakiwa kujijenga kisaikolojia na vyovyote unavyojiwekea ndiyo
matokeo ya baadaye, hiyo ndiyo changamoto kubwa, vingine vyote ni vitu
vidogo vidogo kwa hiyo kila siku ninajifunza na nakutana na vitu vipya
kila siku,” anasema Ethel.
Anasema kitu cha msingi anachokifanya ni kusoma kila siku ili kujua mambo mengi, huku akijitahidi kuwa mwenye uharaka zaidi.
“Najua mimi bado ni mchanga sana katika fani kwa hivyo ninatakiwa kujijenga zaidi ili niweze kufanya kazi yangu vizuri.”
Anasema
bado watu hawaamini mwanamke akipewa nafasi, anasema wengi wanafikiri
kwamba huenda kila nafasi ambayo mwanamke ameifikia basi ni kwa
upendeleo.
“Hata
niliposhinda hii tuzo, hongera hazikuwa nyingi wengi waliuliza kwanini
umeshinda ilikuwaje, kitu cha kwanza watakachokuuliza he umepata hiyo
tuzo nani amekupeleka huko yaani hawaamini kama naweza kusimama
mwenyewe,” anasema Ethel.
Akitoa
wito kwa wanawake, Ethel anasema kitu cha kwanza wanatakiwa kufanya
kazi kwa bidii pia wanatakiwa kujiamini, haiwezekani wapewe nafasi kisha
wakaharibu bali wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo
na hata kuonyesha kwamba wanaweza.
Akielezea
malengo yake anasema anataka kuwa Project Manager ambaye ataweza
kufanya kazi sehemu yoyote duniani, “ninajua nikitimiza miezi tisa
nitaweza kuingia huko ili nipate kibali cha kuweza kufanya kazi popote
ambacho kinapatikana Marekani pekee.”
Hata
hivyo, anasema ili afanikiwe kufika huko anatakiwa kuwa amefanya kazi
miaka mitatu, awe na shahada ya uzamili ambayo tayari anayo lakini pia
kuna mitihani anatakiwa kufanya.
Anasema hili kufikia ndoto za wanawake wengi inapaswa kuwapo idara ambayo itashughulika na masuala ya wanawake pekee.
Akielezea
kilichomvutia kusomea fani ya ujenzi, Ethel anasema alipoingia Chuo
Kikuu cha Ardhi haikuwa mpango wake wa awali kwani alihitaji kusomea
masuala ya madawa.
Anasema
mama yake alimwona akifanya kazi za kukaa ofisini kitendo ambacho
hakupendezewa nacho, alipohitmu kidato cha sita mama yake alimshauri.
“Aliniambia
kuna masomo ya ujenzi najua yatakufaa, nikaingia na kuanza kuangalia
hiki na hiki mtandaoni kabla sijaomba kujiunga, nilipoanza masomo
haikuwa vigumu kwangu,” anasema.
Uhusiano
Kama
ilivyo kwa mabinti wengine, Ethel ana hisia za kimapenzi. Lakini katika
maisha yake anasema hataki kuharakishia mambo. Hasa linapokuja suala la
kuolewa.
“Unahitaji
muda wa kukaa sawa, lazima ujitambue kuanzia muda wa kumaliza chuo,
ujipe muda wa kujijenga, ndoa ni kitu kizuri lakini hakihitaji haraka,”
anasema Ethel.
Anasema tangu amalize chuo miaka takribani mitatu iliyopita amekuwa ni mtu mwenye utofauti sana.
“Kuna
watu wananishangaa, ninaamini kwamba ndoa ni nzuri, lakini kabla
hujaikimbilia inahitaji uwe umekaa na kujitafakari uweze pia
kujitambua,” anasema.
Anasema
msichana kujipa muda wa kujijenga inamsaidia kuwa na msimamo katika
maisha kwani hata atakaposhindwa katika baadhi ya mambo anakuwa na
udhubutu, “nimelelewa na mama yangu pekee, kwa hiyo najua unahitaji kuwa
jasiri yaani mkakamavu na unajijua kwamba kesho likitokea la kutokea na
nikabaki peke yangu unaweza kutengeneza familia nzuri pia inakupa
ulinzi.”
Ethel
anasema tayari yupo katika uhusiano wa kimapenzi, “ninaye lakini huwa
sipendi kuulazimisha uhusiano, kwa kuwa watu wananiambia kwmaba kwa
sababu klwa sasa umefanikiwa kuwa hivi unahitaji kuolewa, lakini kwangu
mimi sivyo si kitu cha kulazimisha, kama ikitokea itatokea kila mmoja
aamue kwa wakati wake.”
