
Swali
hili lipo kwenye mawazo ya wananchi wengi na hata baadhi ya viongozi
wenyewe kwenye Serikali Kuu. Viko viashiria kadhaa ambavyo vinaonyesha
hali ya ‘figisufigisu’ kutokana na matamko ya baadhi ya viongozi wenyewe
wa CCM hasa kutokana na mazoea waliyokuwa nayo ya kiuongozi.
Viongozi
wengi ni walewale kwenye idara zilezile ndani ya chama, tena wameshikwa
na butwaa kutokana na aina ya uongozi wa Rais John Magufuli ambao
unaishushua CCM kwa maovu yote yaliyotendeka nchini.
Yawezekana
baadhi ya wanajamii wakaona kuwa ufisadi unaopelekea majipu kutumbuliwa
ni wa viongozi wa Serikali Kuu, lakini hebu tujiulize Serikali hiyo
iliundwa kutokana na chama kipi? Jibu la moja kwa moja na sahihi ni
Chama cha Mapinduzi (CCM). Butwaa linazingira nafsi za wananchi wengi
wanapofikiria juu ya mwingiliano wa uamuzi kati ya Rais Magufuli na
utashi wa kimazoea wa uongozi wa CCM. Yawezekana pia, wananchi na hata
wafanyabiashara wakasema kasi ya Rais Magufuli kiutendaji huenda
itapungua.
Kukosolewa kwa Rais Magufuli
Wapo
baadhi ya wanajamii, wasomi na viongozi wastaafu ambao kwa namna
tofauti mara kadhaa wakionekana wazi kabisa kuukosoa uongozi wa Rais
Magufuli na hata kutilia shaka ya udhaifu wa utendaji kazi wa viongozi
aliowateua.
Wapo
baadhi yao ambao wanaonekana dhahiri wanatenda kazi kwa woga au shaka
na kutojiamini. Pia, wapo ambao hawana uhakika na kesho yao.
Inadhihirishwa
hata na majipu makubwa ambayo yanatumbuliwa na Rais kwenye wizara zao,
ilhali wao wenyewe wapo au wamekaa kimya. Ni hofu au bado wana mawazo ya
mfumo-sera wa kubebana na kulindana ndani ya CCM?
Zipo
pia fikra za wanajamii na viongozi kuwa labda taarifa zote za uozo
uliotendeka hapa nchini zinalengwa kupelekwa moja kwa moja kwa Rais
Magufuli.
Hili
limezuka kutokana na kutojiamini kwa baadhi ya watendaji wakuu kutokuwa
na ujasiri wa kutoa uamuzi mgumu; ama kuendeleza sera ya CCM ya
kuoneana aibu.
Kutokana
na kasi ya kiutendaji ya Rais Magufuli ni dhahiri kuwa Serikali kuu
imekuwa ni mwiba mkali kwa CCM ambayo ndiyo iliyoiunda Serikali zote
zilizopita, bali Serikali za miongo mitatu iliyopita ndizo zilizotia
fora kwa kuwasononesha wananchi. Serikali ya Rais Jakaya Kikwete ndiyo
inayoongoza kwa kashfa tele ambazo zilifumbiwa macho, sasa zinatumbuliwa
kama majipu.
Chimbuko
jema la kila jambo la kiuongozi ni kuanzia kwenye shina lake na shina
la kila serikali ulimwenguni hutokana na chama cha siasa
kilichochaguliwa na wananchi, kiuongozi Serikali hiyo kama chama
kitakuwa na utendaji makini na adilifu.
Rushwa sugu nchini
Kitendo
hiki kiovu kiitwacho ‘rushwa’ kimeota mizizi katika sekta mbalimbali za
kiofisi, hata kwenye maeneo ya kijamii nchini kote.
Kwenye
kila huduma uitakayo utakuta imezingirwa na viashiria vya kuombwa
rushwa ambayo iko katika majina tofauti. Hivi karibuni Rais Magufuli
alifuatana na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia Rushwa (Takukuru)
kwenye kongamano la makandarasi nchini kwa sababu maalumu.
Hii
ni ishara inayoonyesha ni jinsi gani ambavyo Rais anavyoichukia rushwa
na kuwa na nia thabiti ya kuondosha ama kuipiga vita ya aina yoyote
nchini.
Rais
Magufuli alisema tena kwa msisitizo “makandarasi msichukue rushwa na
mtoe taarifa kwa yeyote anaewaomba rushwa hata kwenye bodi za kutoa
tenda za kazi zenu; ndiyo maana nimemleta mkurugenzi huyu mumpe taarifa
zozote mlizonazo’.
Jambo
hili linalokaziwa na Rais linawapa hofu kubwa watendaji waovu, hata
baadhi ya viongozi waliouzoe mfumo mchafu uliozoeleka wa kufumbia macho
matendo hayo.
Najua
ni kazi ngumu hasa kwa baadhi ya viongozi wetu wengi wa nchi za Afrika
ama za ulimwengu wa tatu. Nyingi zimezama kwenye wimbi la uovu
huo-rushwa na ufisadi wa kila aina na nchi nyingine maovu hayo
yanaongozwa na viongozi waku wenyewe, kujilimbikizia utajiri usiolezeka.
Rais
Magufuli anahitaji kushirikiana na mawaziri wake, watendaji wakuu,
watoa huduma mbalimbali pia, wananchi kuipiga vita tabia hii ovu. Ni
kazi inayohitaji uwajibikaji wa kila mwanajamii kwa nia ya dhati;
vinginevyo itachukua muda mrefu kutoweka ama kupungua ipasavyo.
Rai
yangu, wana siasa ambao wananchi wamewapa kura zao wawe wawakilishi wa
majimbo yao, wajinasue wenyewe kwenye mtego wa tamaa za kifisadi hasa
wanapochangamana na baadhi ya wana siasa wanaowakuta kwenye dimbwi hilo
la aibu ya rushwa.
Wapo
wazoefu ambao katika kila kashfa wanatuhumiwa, na hao wadau wao kwa
majina tofauti kama ‘wawekezaji ama wafanyabiashara’ na hata wana ukoo
wa baadhi ya viongozi ndio waliotufikisha katika ‘uozo’ unaolitesa taifa
letu.
