
Taifa linapita katika wimbi zito la mauaji ya kikatili ikiwamo watu kuvamiwa na kuchinjwa kama kuku.
Matukio
haya mapya ya watu kuvamiwa na kuchinjwa yameshuhudiwa hadi ndani ya
nyumba za ibada kama ilivyotokea jijini Mwanza baada ya watu waliofunika
nyuso zao kuvamia Msikiti wa Rahman, eneo la Mkolani na kuua watu
watatu akiwamo Imam wa msikiti huo, Fereuz Ismail.
Katika
Kijiji cha Sima, Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, watu wasiojulikana
walivamia familia ya Zakaria Mbata na kuwaua kwa kuwakata mapanga watu
saba.
Miongoni
mwa waliouawa ni pamoja na mama wa familia hiyo, Eugenia Phillipo,
watoto wake watatu na wageni watatu wa familia hiyo. Wiki iliyopita mume
na mke wakachinjwa na watu wasiojulikana waliovamia nyumbani kwao huko
wilaya ya Butiama mkoani Mara.
Vumbi
likiwa halijatulia, watu wasiojulikana wanaoaminika kujificha katika
mapango ya Amboni mkoani Tanga wakavamia Kitongoji cha Kibatini mkoani
humo na kuwaua kwa kuwachinja watu wanane kabla ya kupora vyakula
dukani.
Mauaji ya aina hii ni mapya katika historia ya Taifa letu linalosifika duniani kuwa la amani na utulivu.
Zamani
mauaji ya kukata watu kwa mapanga yalisikika mikoa ya Kanda ya Ziwa
hasa Mwanza, Shinyanga, Geita na Simiyu yakihusishwa na imani za
kishirikina.
Katika
mauaji hayo ya kishirikina walengwa zaidi walikuwa ni vikongwe, hasa
wanawake ambao ama walidaiwa kuhusika na vifo vya wana familia.
Suala
la urithi na mgawanyo wa mali pamoja na migogoro ya mashamba au mipaka
ya ardhi ilidaiwa kuwa miongoni mwa sababu za mauaji hayo.
Hata hivyo, aina mpya ya mauaji ya kukata mapanga na kuchinja yana sura tofauti.
Wauaji wanaua hadi watoto wanaokutwa kwenye eneo la tukio kama tulivyoshuhudia kule Sengerema.
Ingawa
wahalifu wana mbinu na mikakati kadhaa ya kukwepa mikono ya dola wakati
wa kutekeleza uhalifu wao. Nimeanza kutilia shaka uwezo wa
kiintelijensia wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama.
Simaanishi
kuwa vyombo vyetu havifanyi kazi. La hasha! Vinafanya kazi sana kwa
sababu vimefanikiwa kudhibiti au kukabili matukio kadhaa ya uhalifu
nchini.
Hata
hivyo, nadhani uwezo wa kukusanya taarifa za kiintelijensia za vyombo
vyetu na kuzifanyia kazi umepungua katika siku za hivi karibuni.
Yawezekana
watendaji wa vyombo hivi hawatumii ipasavyo fursa za kupata taarifa za
kiintelijensia na hivyo kuwapa mwanya wahalifu kupanga na kutekeleza
uhalifu wao bila kubainika au uwezo wao katika mikakati ya kukabiliana
nao umegota.
Tatizo
lingine ninaloliona ndani ya vyombo vyetu ni kupuuza kwa makusudi au
kwa bahati mbaya baadhi ya taarifa za kiintelijensia zinazofikishwa kwao
na raia wema.
Baada
ya mauaji ya Tanga, kuna taarifa kuwa vyombo vya dola viko imara na
vinatenda kazi kwa haraka vinapopata taarifa zinazohusiana na masuala au
matukio ya kisiasa.
Pia,
yapo madai kuwa baadhi ya watendaji wa vyombo vya dola ama wanashiriki
au wana uhusiano na makundi ya kihallifu. Watendaji hao wasio waaminifu
wanadaiwa kuvujisha taarifa za kiintelijensia kwa wahalifu na hivyo
kuwawezesha kukwepa mikono ya dola.
Kama
Taifa, hatuwezi kuendelea kuvumilia hali hii ambayo siyo tu inaangamiza
maisha ya wapendwa wetu, pia inachafua sura na sifa ya nchi yetu mbele
ya dunia.
Ulianza
ukataji viungo na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi kwa imani za
kishirikina ambao vumbi lake limeanza kutulia. Pamoja na mbinu zingine
za kimafunzo, nadhani muda umefika turejee kwenye mfumo wa zamani wa
enzi ya Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya Mwalimu Julius Nyerere ya
taarifa za kiintelijensia kukusanywa kuanzia ngazi ya nyumba 10.
Mabalozi
wa nyumba 10 warejeshewe nguvu za kisheria za kufuatilia, kubaini na
kuorodhesha wageni na watu wote wanaoiongia na kuishi ndani ya maeneo
yao kiutawala.
Hii
itasaidia kubaini wageni wote na mienendo yao tofauti na sasa watu
wanaweza kuishi mtaa mmoja kwa mwaka mzima bila kuonana wala kufahamiana
nani ni nani na anafanya shughuli gani. Wapo watakaopinga wazo hili kwa
madai kuwa siyo rahisi watu wote mtaani kujulikana shughuli zao. Lakini
napenda kuhoji iliwezekanaje wakati ule, isiwezekane leo?
Ni
suala la uamuzi na kuweka misingi ya sheria kufanikisha hili kwa faida
na masilahi ya jamii yetu. Tuache siasa na mawazo ya kushindwa kabla ya
kujaribu inapofika masuala ya msingi ikiwamo usalama wa raia na mali
zake.
Kama
kweli viongozi wetu wasema kwa dhati kuwa wanamuenzi Mwalimu Nyerere,
basi waanze na hili la ulinzi na usalama kwa kurejesha mfumo imara na wa
kisheria wa ulinzi na usalama kuanzia ngazi ya mabalozi wa nyumba 10
uliofanya Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa yenye uwezo mkubwa
kiintelijensia enzi hizo.
Vita
dhidi ya uhalifu haviwezi kupiganwa na vyombo vya dola pekee
vikafanikiwa. Umma lazima ushiriki kikamilifu kwa kutoa taarifa za
kiintelijensia zitakazosaidia kunasa wahalifu na hiyo sharti ianzie
ngazi ya chini kabisa ya nyumba 10.
