Nimemsikia kiongozi mmoja wa juu wa timu hiyo ya Mwanza akisema kuwa timu yake itaanza maandalizi ya msimu ujao mapema zaidi tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita. Hapohapo akasema, “Wachezaji wote tuliokuwa nao msimu uliopita wamemaliza mikataba.”
Kwa maana hiyo sasa Toto haina mchezaji hata mmoja, duh! Yaani labda tutolee mfano Sunderland ya England leo hii wachezaji wake wote wasiwe na mikataba, Haiwezekani ila kwa Toto Africans imewezekana.
Kiukweli, kama inafikia hatua ya wachezaji zaidi ya 25 kwa wakati mmoja wanamaliza mikataba yao ina maanisha kuwapo kwa udhaifu mkubwa sana katika utawala. Toto ni timu ya kwanza ambayo baada ya kumalizika kwa msimu imebaki bila mchezaji hata mmoja! Tena ni klabu ya ligi kuu Tanzania Bara (VPL.)
Sikatai wachezaji kumaliza mikataba yao, lakini inakuwaje kwa wakati mmoja wachezaji wote wawe huru?
Nadhani uongozi uliopita wa klabu hiyo ulikuwa ukifanya mambo yake na ‘kuyaweka katika urahisi,’ ndiyo maana ukiachana na misukosuko yote, kama hali ngumu ya kiuchumi iliyopelekea ukosefu wa mahitaji muhimu ya wachezaji kama, chakula, malazi, usafiri, ucheleweshwaji wa pesa za usajili, posho na mishahara, vifaa vya kufundishia kwa wakufunzi watatu Wajerumani ambao walikuja kuisaidia kiufundi timu hiyo kwa msaada si malipo.
Ukata si ‘lalamiko la leo tu’ katika timu hiyo, ni tatizo ambalo upande wangu nimekuwa nikilisikia tangu ningali kijana mdogo, lakini sikuwahi kusikia timu hiyo ikiishi bila kuwa na mchezaji hata mmoja baada ya kumalizika kwa msimu.
Wanakosa mapato, kwa maana kuna wachezaji bora katika timu hiyo ambao chini ya dau la milioni nane hadi kumi Toto isingekubali kuwaachia kama wangekuwa na mikataba. Bahati nzuri kwao ni kwamba timu yao ilikuwa na vijana zaidi ambao waliwapata kama wachezaji huru wakati wa usajili wa katikati ya mwaka uliopita.
Wangepata si chini ya milioni kumi kama dau la kumuachia kijana Waziri Junior ambaye ni kati ya chipukizi walioingia VPL na kuleta tofauti. Si kwa kuwa alifunga magoli matatu kwa mpigo ‘hat-trick’ katika uwanja wa ugenini dhidi ya MajiMaji FC au kwa goli lake maridadi sana la mkwaju wa mbali dhidi ya Simba katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, si hivyo, Junior ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa ndani ya uwanja.
Nahodha wao, Hassan Khatib, Salum Chuku, Edward Christopher, Miraj Athuman, Abdallah Seseme ni baadhi tu ya vijana ambao timu za ‘nafuu kuliko Toto’ zingewahitaji hata kama wangekuwa na mikataba. Kwa kuwauza wangeingiza pesa katika akaunti yao na kuitumia kwa mambo mengine muhimu, ikiwemo kusaka vipya lakini sasa watalazimika kuingia gharama mara mbili kama wanahitaji nyota wao wa msimu uliopita wabaki katika timu.
Kumsainisha mchezaji kijana kwa mwaka au pengine miaka miwili ni makosa ambayo yamekuwa yakitendeka hadi katika klabu kubwa. Nafikiri mkataba wa miaka mitatu kwa mchezaji kijana unapaswa kuwa ndiyo wa muda mfupi zaidi.
Mwaka wa kwanza utakuwa ni wakujifunza na kupata uzoefu, mwaka wa pili ni kumjenga kijana kiushindani na mwaka wa mwisho katika mkataba wa miaka mitatu ni mchezaji kuthibitisha usahihi wa kuwapo kwake katika timu,anapaswa kucheza kwa ukomavu na kuonyesha uwezo ndani ya uwanja.
Wakati msimu ukiendelea klabu, mfano, Toto Afrika ilipaswa kuwasainisha mikataba mipya wachezaji wao kama Junior, Seseme, Chuku, Khatib, Christopher na wale wengine waliokuwa katika mwelekeo sahihi, kimpira na kibiashara kwa maana vijana ambao ‘wanaweza kuuzika’ na klabu ikapa faida kipesa. Kosa si kosa, bali kurudia kosa ndiyo kosa.
Toto wanapaswa kuingia mikataba mirefu isiyowaumiza wachezaji vijana wala klabu.
Kwa ukaribu zaidi, tafadhali unaweza ku-LIKE PAGE yangu BSports. Utapata Updates za michuano mbalimbali.
