Mtuhumiwa Happiness Joel
JOSEPH NGILISHO, Amani
ARUSHA: AMENASWA! Msako
uliofanywa na wananchi wa Kitongoji cha Namayana, Kata ya Kiranyi
wilayani Arumeru mkoani hapa, kufuatia tukio la mwanamke kudaiwa kutupa
vichanga mapacha, umefanikiwa kumnasa mtuhumiwa Happiness Joel (29),
tembea na Amani.
Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Elias
Naigisa akizungumza na gazeti hili mwanzoni mwa wiki hii, alisema June
7, mwaka huu alipata taarifa ya kutupwa kwa vichanga viwili katika
chemba ya choo kinachomilikiwa na mkazi wa kitongoji hicho, Elibariki
Loti.
“Polisi walifika na kuchukua miili ya
vichanga hao na kwenda kuihifadhi katika chumba cha maiti katika
Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru kusubiri uchunguzi,” alisema mwenyekiti
huyo.
Aliendelea kuweka wazi kuwa June 8,
mwezi huu, yaani siku moja baada ya tukio hilo, wananchi walifanikiwa
kumbaini mtuhumiwa huyo ambaye pia alikuwa na mtoto wa miaka 2 mgongoni
na baada ya kuhojiwa, alikiri kuhusika na tukio hilo.
Alisema mtuhumiwa huyo alieleza kwamba
ni kweli alikuwa na ujauzito na aliamua kutupa vichanga hivyo baada ya
kujifungua kwa kile alichodai ni bahati mbaya.
Hata hivyo, taarifa nyingine zinadai
kuwa mama huyo aliwatupa watoto hao kutokana na aibu baada ya kuwa
tayari ana mtoto mdogo mgongoni ambaye bado anamnyonyesha.
Kwa upande wa mwanaume aliyempa ujauzito
huo aliyetambulika kwa jina moja la Godlucky, alikiri kumpa ujauzito
mwanamke huyo na kusema kuwa amesikitishwa na tukio hilo.
