Beki mpya wa Yanga , Andrew Vincent ‘Dante’.
Omary Mdose na Said AllyYANGA imempa beki wao mpya waliomsajili hivi karibuni, Andrew Vincent ‘Dante’ kitita cha Sh milioni 30 ikiwa ni ada yake ya uhamisho kutoka Mtibwa Sugar kwenda Yanga.
Dante alimaliza mchakato wake wa kujiunga na Yanga, juzi Jumatatu jioni baada ya kumaliza mkataba wake ndani ya Mtibwa, mwishoni mwa msimu uliomalizika hivi karibuni.
Akizungumza na Championi Jumatano, Dante alisema, mchakato wake wa kujiunga na Yanga ulifanyika haraka huku yeye akiwa hafahamu chochote kutokana na kuwa kwenye kambi ya timu ya taifa, lakini mara tu alipomaliza majukumu hayo, akaambiwa na wakala wake kwamba anatakiwa kwenda kusaini Yanga.
“Ni kweli hata mimi nilikuwa sijui kama nitaenda Yanga kwani wakati nipo kambini na timu ya taifa, nilipanga baada ya hapo niende Mtibwa kuzungumza nao juu ya mustakabali wangu.
“Lakini nashangaa baada ya kumaliza majukumu ya timu ya taifa, wakala wangu akanitaka twende kumalizana na Yanga, nikakubali, ikawa hivyo kama ilivyokuwa. Wamenipa mkataba wa miaka miwili pamoja na shilingi milioni 30 za usajili wangu, lakini masuala ya mshahara si vyema kuyaweka hadharani kwa sasa.
“Bado sijaungana na timu yangu hiyo mpya, lakini natarajia siku za hivi karibuni nitaungana nao, wameniahidi kunipatia sehemu ya kuishi, kabla ya kufanya hivyo nitaangalia kwanza wapi patakuwa ni rahisi ili isiwe tabu kwenda mazoezini.
“Lakini ningependa kuendelea kuishi ninapoishi kwa sasa huku Mbagala kwani nimepazoea sana na najua nikihama huku nitaenda kupata vishawishi ambavyo vitaua kiwango changu,” alisema Dante.
Yanga tayari imeshafanya usajili wa wachezaji wanne ambao ni Hassan Kessy aliyetokea Simba ambaye usajili wake umegharimu Sh milioni 40, Juma Mahadhi (Coastal Union, Sh mil 30), Beno Kakolanya (Prisons, Sh mil 35) na Dante (Sh mil 30), jumla Yanga imetumia Sh milioni 135 kwa wachezaji hao wanne.