
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni akijibu swali bungeni, mjini Dodoma jana. Picha na Anthony Siame
Dodoma.
Kitendo cha Charles Kitwanga, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani,
kujibu swali akiwa amelewa kimesababisha jibu lake kuwa batili na jana,
Serikali ilitoa upya bungeni majibu kutokana na maagizo ya Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa.
Kitwanga,
ambaye anatuhumiwa kuhusika kwenye sakata la utekelezaji mbovu wa
mkataba wa ufungaji mashine za kielektroniki za kuchukulia alama za
vidole kwenye vituo vya polisi, alivuliwa uwaziri Ijumaa iliyopita baada
ya kutinga bungeni akiwa amelewa na kujibu maswali kwa namna ambayo
ilielezewa na muulizaji kuwa “ya pozi”.
Akijibu
swali hilo, Kitwanga alijikita kusoma karatasi aliyokuwa nayo,
akisitasita na kuweka vituo sehemu kadhaa huku akinyanyua kichwa kwa
nadra.
“Mheshimiwa
mwenyekiti, kama yalivyowahi kujibiwa maswali kadhaa ndani ya Bunge
lako tukufu kuhusu askari kuboreshewa makazi, Serikali inafahamu kuwa
lipo tatizo la baadhi ya askari wa Jeshi la Magereza na polisi kuishi
katika nyumba chakavu zisizokuwa na hadhi (anazungumza huku
akitabasamu). Namuona rafiki yangu hapa anashusha kichwa, ananyanyua,”
alisema.
“Mheshimiwa
mwenyekiti, katika kukabiliana na tatizo hilo, Serikali imeendelea na
mpango wake wa kuzifanyia ukarabati mkubwa baadhi ya nyumba na kwenye
baadhi ya Magereza na kujenga nyumba na vilevile kuendelea kuona
mahitaji ya nyumba na hivi sasa ni nyumba 14,500 wakati zilizopo ni
nyumba 4,221, hivyo kuwepo upungufu wa nyumba 10,279 ambao unalazimisha
baadhi ya askari kuishi nje ya kambi za magereza.
“Hata hivyo, kasi ya utekelezaji umekuwa ni mdogo kutokana na ufinyu wa bajeti.”
Alipoulizwa
kuwa Serikali itaendelea kujenga nyumba hadi lini wakati sasa ni miaka
54 ya uhuru, Kitwanga alianza kujibu kwa kuuliza swali: “Mheshimiwa
mwenyekiti, huyu ni rafiki yangu. Ananiuliza wapewe miaka mingapi? Na
yeye ana miaka mingapi?”
Jana,
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Yusufu Masauni alijibu swali hilo
namba 211 la Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Devota Minja ambalo
lilikuwa na tofauti kubwa kulinganisha na lililotolewa na Kitwanga
Ijumaa asubuhi.
Kati
swali hilo ambalo awali lilikuwa namba 205, Minja alitaka kujua
Serikali ina mpango gani wa kuboresha makazi ya polisi na magereza
wanaoishi katika nyumba chakavu zisizokuwa na hadhi ikilinganishwa na
kazi zao kwa jamii.
Kama
ilivyokuwa wiki iliyopita wakati swali hilo lilipoulizwa na kwa niaba
yake na Mbunge wa Mlimba (Chadema), Suzan Kiwanga, jana liliulizwa na
Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini.
Tofauti
kati ya majibu ya Kitwanga na Masauni ilijitokeza katika takwimu ya
nyumba za Magereza, lakini kwa upande wa nyumba za polisi majibu
yalikuwa sawa, isipokuwa tu naibu waziri alitoa takwimu za kila mkoa
tofauti na mwenzake.
Masauni
alisema Jeshi la Magereza limesaini mkataba na kampuni ya Poly
Technologies ya China kujenga nyumba 9,500 kwenye vituo vyote vya
magereza nchini.
Alisema
Makao Makuu ya Magereza zitajengwa nyumba 472, Arusha (377), Dodoma
(356) Dar es Salaam (952), Kagera (364), Kigoma (272), Kilimanjaro (390)
na Lindi watajenga nyumba 233.
Mikoa
mingine ni Manyara (206), Mara (378), Mbeya (622), Iringa (336),
Morogoro (669), Mtwara (215), Mwanza (398), Pwani (384), Rukwa (358),
Ruvuma (320), Shinyanga (337), Singida (299), Tabora (408), Tanga (382),
KMKGM Dar (219), Chuo cha Ukonga (115), Chuo cha Kiwira (183), Chuo cha
Ruanda (62), Chuo cha KPF (27) Bohari Kuu (82) na Bwawani nyumba 84.
Kwa
upande wa Jeshi la Polisi majibu yalikuwa ni yale yaliyotolewa na
Kitwanga kuwa Serikali inakusudia kujenga nyumba 4,136 katika mikoa 17
ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Alisema
Serikali itaendelea kutatua changamoto za uhaba wa nyumba kwa kutumia
njia mbalimbali, ikiwamo mikopo nafuu na yenye riba nafuu na miradi
shirikishi kwa kutumia fedha za bajeti ya Serikali.
