
Waziri wa Habari, Nape Nnauye
Mwanza. Mzimu
wa kuzuia shughuli za Bunge kuonyeshwa moja kwa moja na vituo vya
televisheni uliopachikwa jina la ‘Bunge Live’, umeendelea kumwandama
Waziri wa Habari, Nape Nnauye baada ya juzi kupokewa kwa kelele kiasi
cha kushindwa kuhutubia wapenzi wa muziki jijini Mwanza.
Nape
alitangaza uamuzi wa kusitisha kurusha moja kwa moja baadhi ya shughuli
za Bunge, akisema Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) linashindwa
kumudu gharama, lakini wabunge, hasa kutoka vyama vya upinzani wamepinga
hatua hiyo wakisema inawanyima wananchi haki yao ya kikatiba ya kupata
habari kuhusu chombo chao cha kutunga sheria.
Lakini
Serikali imeshikilia msimamo wake, ikitoa sababu tofauti na kwenda
mbali zaidi kuzuia vituo binafsi vya televisheni kurusha matangazo, huku
TBC1 ikirusha kipindi cha maswali na majibu pekee ikielezwa kuwa huo ni
uamuzi uliopitishwa katika Bunge la 10.
Juzi,
Nape aliyekuwa mgeni rasmi katika tamasha la Jembeka Festival
lililofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, alipokewa na kelele za
maneno “Bunge Live” wakati akikaribishwa kuhutubia mamia ya wapenzi wa
burudani waliohudhuria tamasha hilo, ambalo lilijumuisha wasanii nyota
kama Shaffer Chimere Smith a.k.a Ne-Yo kutoka Marekani na Diamond
Platnum.
Baada
ya mkurugenzi wa kampuni ya Jembe ni Jembe, Sebastian Ndege
kumkaribisha waziri huyo kuzungumza na wananchi hao, Nape alisimama
lakini akapokewa kwa kelele.
“Bunge live, Bunge live, Bunge live,” walipiga kelele mashabiki waliohudhuria tamasha hilo.
Kelele
za “Bunge Live” zilisababisha Waziri Nape kushindwa kuhutubia na
kulazimika kuketi chini na Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula
alisimama kujaribu kuokoa jahazi, lakini naye akakumbana na kimbunga cha
sauti za wananchi walioamua kulitaja jina la mbunge wa zamani wa jimbo
hilo, Ezekia Wenje.
“Wenje, Wenje, Wenje,” wananchi hao waliimba kwa sauti wakati Mabula akijaribu kuwatuliza ili Nape ahutubie.
Akizungumzia
tukio hilo, Nape alisema wananchi waliompigia kelele za “Bunge Live”
walisukumwa na masuala ya kisiasa, ndiyo maana aliepuka kuendelea
kuzungumza ili kutochafua hali ya hewa uwanjani.
“Pale
uwanjani tulikwenda kwa ajili ya burudani, sasa baada ya kuona wananchi
wanaanza kuleta masuala ya kisiasa nikaona ni busara kuacha kuhutubia.
kuepusha shari,” alisema Nape.
Pamoja
na Nape, tamasha hilo pia lilihudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Makamu wa Rais (Mazingira na Muungano), January Makamba, Mkuu wa Mkoa wa
Mwanza, John Mongella na Mabula.
Ukiachilia
mbali dosari hizo, tamasha hilo lilikonga nyoyo za wapenzi wa sanaa ya
muziki waliokesha uwanjani hapo hadi saa 11:00 alfajiri wakiburudishwa
na wasanii nguli.
Wasanii wengine waliopata nafasi ya kutumbuiza ni Juma Nature, Ney wa Mitego, Ruby na Fid Q.
Maoni ya wadau
Wadau waliozungumza na Mwananchi wameitaka Serikali kuangalia upya uamuzi wake baada ya tukio hilo la Mwanza.
“Unapotenda
mambo lazima ukumbuke na historia,” alisema mwanasiasa mkongwe nchini,
Njelu Kasaka ambaye alikumbusha kiini cha Serikali kuamua kuonyesha moja
kwa moja shughuli za Bunge wakati wa utawala wa Rais wa Serikali ya
Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.
“Rais
Mkapa alikuwa na sera ya uwazi na ukweli. Kwa kuonyesha Bunge moja kwa
moja ni kuweka uwazi kwa wananchi ili wajue nchi yao inakwendaje.”
Kasaka
aliyewahi kuwa mbunge wa Lupa ambalo sasa lipo mkoa mpya wa Songwe,
alisema kuonyesha Bunge moja kwa moja kunawasaidia wananchi kujua yupi
ni kiongozi bora na yupi hafai.
“Hata
kama nchi nyingine hazionyeshi live, kusitunyime sisi uhuru wa
kuangalia Bunge letu. Kuna mtu amesema eti watu hawafanyi kazi, hiyo
siyo kweli. Hizo TV walizoweka ofisini ni za nini?” alihoji Kasaka.
Mtaalamu
wa masoko wa kampuni ya The Exchange, Lucas Moreto alisema kitendo cha
kukatisha maonyesho ya Bunge ya moja kwa moja kimewanyima wananchi haki
ya kupata habari.
“Ukilitazama
suala hili kwa undani utaona kuwa wananachi wamebaki ndani ya sanduku,
hawaelewi kinachoendelea nje. Nasikia kuna televisheni ya Bunge lakini
bado wananchi hawapati haki ya kuangalia kinachoendelea wakati wote. Ni
kuwanyima tu haki ya kupata habari,” alisema Moreto.
Mhadhiri
wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard Mbunda
alisema hatua hiyo imetia doa Serikali ya Rais John Magufuli.
“Utawala
wa Awamu ya Tano umejipambanua kuwa na malengo ya kupigania haki za
wanyonge. Hata wanapotumbua majipu husema ni kwa ajili ya mamilioni
wanaoteseka kwa kukosa huduma vijijni,” alisema na kuongeza:
“Sasa
malengo hayo inabidi yajidhihirishe kila kona, ikiwamo kisiasa. Kuona
Bunge live inachukuliwa kama nafasi ya wanyonge kutathmini utendaji wa
wawakilishi wao. Hivyo basi, hatua hii ya kufuta Bunge live haitapokewa
vizuri na inatia doa nia nzuri ya Serikali ya awamu hii.”
