
Dar es Salaam.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliondoka nchini jana kwenda Lusaka, Zambia
kuhudhuria mkutano wa 51 wa mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika
utakaofanyika kesho.
Waziri Mkuu anahudhuria mkutano huo kwa niaba ya Rais John Magufuli ikiwa ni mara yake ya tatu kumuwakilisha mkuu huyo wa nchi.
Mara
ya kwanza alimuwakilisha nchini Botswana katika mkutano wa Sadc na
mapema mwezi huu alimuwakilisha katika mkutano wa wakuu wa nchi wa
kujadili mapambano dhidi ya rushwa London, Uingereza.
Mkutano
huo wa Zambia ambao utafunguliwa na Rais wa Zambia, Edgar Lungu
utajadili masuala ya nishati na mabadiliko ya tabianchi. Pia, mkutano
huo utahudhuriwa na marais Idriss Deby wa Chad, Paul Kagame wa Rwanda na
Uhuru Kenyatta wa Kenya.
Nigeria
itawakilishwa na Makamu wake wa Rais, Yemi Osinbajo huku Msumbiji
ikiwakilishwa na Waziri Mkuu, Carlos Agostinho do Rosário.
Watu
maarufu waliothibitisha kuhudhuria mkutano huo ni pamoja na Kofi Annan,
Ashish Thakkar, John Kufuor, Mary Robinson, Mo Ibrahim, Nancy Lee,
Ngozi Okonjo-Iweala na Tony Elumelu.
Mkutano
huo utakaofanyika kwenye kituo cha mikutano cha kimataifa cha
Mulungushi utakuwa na washiriki zaidi ya 5,000 kutoka nchi 54 ambao ni
wanachama wa benki hiyo, washiriki kutoka nchi 26 ambazo si za bara la
Afrika, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, wadau wa maendeleo na
wawakilishi wa asasi za kiraia.
Wengine watakaohudhuria ni mawaziri wa fedha, biashara na uchumi na wataalamu kutoka vyuo vikuu.
Waziri Mkuu amefuatana na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji, wachumi kadhaa na wataalamu wa sekta ya fedha.
