
Dar es Salaam.
Mwenge wa Uhuru ulioingia jijini jana ukitokea Mkoa wa Mjini Magharibi,
Zanzibar unatarajiwa kuzindua miradi 22 ya maendeleo yenye thamani ya
Sh19.9 bilioni.
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ndiye aliyeupokea Mwenge na baadaye kuanza mbio zake katika Wilaya ya Kinondoni.
Mwenge
huo ulipokewa katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere na kamati ya
ulinzi na usalama ya mkoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi, mameya pamoja
na viongozi wengine wa Serikali na vyama.
Mwenge
huo ulikabidhiwa kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Theresia
Mmbando kutoka kwa Katibu Tawala wa Mjini Magharibi, Juma Ally na
baadaye Mmbando alimkabidhi Makonda.
Baada
ya kukabidhiwa, Makonda alisema utatumika kikamilifu kuhimiza kaulimbiu
ulizobeba na kuzindua miradi ya maendeleo katika mkoa wake baada ya
hapo akamkabidhi mwenge huo Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi kwa
ajili ya kuanza rasmi mbio hizo Dar es salaam.
“Kuna
miradi 22 itapitiwa na Mwenge; mingine imekamilika, mingine haijakamika
ambapo sita itazinduliwa, mitatu itatembelewa, tisa itawekewa jiwe la
msingi na minne itafunguliwa. Yote ikiwa na thamani ya Sh19.9 bilioni”,
alisema Makonda.
Katika
Wilaya ya Kinondoni, Mwenge utatumika kuzindua miradi saba ya maendeleo
yenye thamani ya Sh3.2 bilioni ambayo ni Soko la Mburahati, ujenzi wa
barabara ya Arsenal Magoti, ujenzi wa wodi ya wajawazito, ujenzi wa
Mabweni Mbopo, ujenzi wa kalavati Mabwepande, ujenzi wa Kituo cha Kilimo
Malolo na ujenzi wa kisima cha maji Makongo.
Kiongozi
wa mbio za Mwenge, George Mbijima aliwataka wananchi kuzingatia ujumbe
unaobebwa na Mwenge kwani huangazia masuala muhimu yanayoligusa Taifa
kwa wakati huo.
“Mbio
za Mwenge mwaka huu zimebeba kaulimbiu isemayo: Vijana ni nguvu kazi ya
Taifa washirikishwe na wawezeshwe pamoja na ujumbe wa kudumu kuhimiza
mapambano dhidi ya Ukimwi, dawa za kulevya, rushwa na malaria,” alisema
Mbijima.
Leo Mwenge utafanya ziara zake Wilaya ya Ilala na kesho utakuwa Temeke kabla ya keshokutwa kuendelea na ziara yake mkoani Pwani.
