Pemba.
Mkuu wa Wilaya ya Wete Rashid Hadid Rashid amefunga maduka matatu ya
rejareja na kusimamisha magari ya abiria kati ya Wete na Mtambwe kwa
madai ya kutoa huduma kwa misingi ya ubaguzi wa kisiasa.
Wafanyabiashara waliofungiwa ni Said Juma Seif, Titi Juma Othman wa Mtambwe na Hamad Haji wa Mchangamdogo.
Alisema wafanyabiashara hao wamelalamikiwa na wafuasi wa CCM, wakiwatuhumu kukataa kuwahudumia kutokana na itikadi zao za vyama.
Rashid alisema baada ya kufanya uchunguzi, walibaini kuwa wafanyabiashara hao wanawabagua wanaCCM.
“Tumelazimika
kuyafungia maduka hayo matatu baada ya Serikali ya Wilaya kujiridhisha
kwamba yanawabagua wanachama wa CCM,” alisema.
Akizungumzia
hatua hiyo, Haji aliitaka Serikali kufanya uchunguzi kwanza kabla ya
kuchukua hatua akisema hahusiki na masuala ya kisiasa. Alisema hizo ni
chokochoko za wabaya wake.
Usafiri wasitishwa
Mkuu
huyo wa wilaya, aliagiza kuzuiwa kwa magari yote ya kubeba abiria
kwenye Barabara ya Wete – Mtambwe kwa madai hayohayo ya kuwabagua
wanaCCM.
Alisema mbali ya hatua hiyo, atawasiliana na wizara husika ili kuchukua hatua kwa wahusika kwa kukiuka leseni.
Hata
hivyo, haikufahamika mara moja kama zuio hilo alilosema ni la muda
usiojulikana litayahusu magari ya Ruti B ambayo leo ndiyo yaliyotarajiwa
kutoa huduma kwani yaliyozuiwa jana kwenda Mtambwe, nyumbani kwa Katibu
Mkuu wa CUF, Maalim Seif ni ya Ruti A.
Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Wilaya ya Wete, Mmanga Juma Ali alisema katika
utekelezaji wa agizo hilo hakutakuwa na huruma: “…Hatutaishia hapo
wanaofanya ubaguzi huo watafikishwa mahakamani.”
Hata
hivyo, baadhi wa wahuduma wa vyombo vya usafiri walisema si wao
wanaowashusha, bali ni wananchi na kwamba dereva na konda hawawezi
kufanya hivyo kwa kuwa lengo lao ni kutafuta faida.
Maalim Seif atema cheche
Wakati
uongozi wa Wete ukichukua hatua hiyo, Maalim Seif ameendelea na ziara
yake visiwani hapa aliwataka Wazanzibari kuonyesha kuwa wanaikataa
Serikali ya Dk Ali Mohamed Shein.
Akizungumza
na watendaji na viongozi wa CUF wa Wilaya ya Micheweni, Kaskazini
Pemba, Maalim Seif aliwataka kutomtegemea yeye pekee kufanya hivyo.
“Tukikazana,
Serikali hii itaondoka, ikiwa mnangoja Maalim Seif au Marekani
kuiondoa, kwa sheria ya kimataifa haitawezekana kwani Marekani haiwezi
kuingilia mambo ya ndani ya Zanzibar,” alisema
Makamu
huyo za zamani wa Rais wa Zanzibar, alijitoa kwenye uchaguzi wa marudio
uliofanyika Machi 20 ambao Dk Shein aliibuka kidedea.
Uchaguzi
huo ulikuwa wa marudio baada ya ule wa Oktoba 25 kufutwa na Mwenyekiti
wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Jecha Salim Jecha siku ambayo alikuwa
atangaze matokeo yote.
Katika
mkutano huo, Maalim Seif alisema Serikali ya CCM imeanza kutikisika
kutokana na vikwazo vinavyoendelea kuwekwa na wahisani pamoja na hatua
ya chama chake CUF kutowatambua viongozi wake pamoja na Serikali. “CCM
wajue wamekalia kuti kavu, siku yoyote wataanguka... tufanye kazi mpaka
haki yetu tuhakikishe imerudi na wenzetu hawana safari ya kudumu,”
alisema.
Aliwataka
wanachama wake kuonyesha kwa vitendo kutoitambua Serikali ikiwamo
kukataa kulipishwa kodi za ovyovyo pamoja na kujitenga na viongozi wa
Serikali katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Mfano
tunaweza kuamua siku fulani kuanzia saa sita, tunasimamisha vyombo
vyote vya usafiri na siku nyingine tunaamua kupiga honi Zanzibar nzima
kuonyesha hatuitaki Serikali ya CCM,” alisema huku akishangiliwa na
umati uliofurika katika ofisi za chama hicho.
CUF yajipanga kwenda ICC
Alisema
kuna mwanasheria mzalendo ambaye ameanza kukusanya vielelezo mbalimbali
kabla ya kufungua kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya ICC dhidi ya
viongozi wenye dhamana ya kusimamia vyombo vya ulinzi na usalama wa
raia.
Alisema
tayari Waziri wa Mambo ya Ndani, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Muungano, wamepewa notisi ya kuarifiwa
kufunguliwa mashtaka ICC kutokana na vitendo vya uvunjwaji wa haki za binadamu uliofanyika Zanzibar.
CCM yamjibu
Akizungumzia
kauli za Maalim Seif, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai
alisema chama chake hakina muda wa kujibizana na CUF baada ya kumalizika
kwa uchaguzi na kwamba watakutana tena majukwaani na chama hicho kwenye
uchaguzi wa 2020.
Baraza la wawakilishi kesho
Wakati hayo yakiendelea Baraza la Wawakilishi linatarajiwa kuanza kesho Chukwani, nje kidogo ya mji wa Unguja.
Macho
na masikio ya wananchi yataelekezwa katika Muswada wa Sheria ya Mafuta
na Gesi ambao unaweza kutegua kitendawili cha rasilimali hiyo kubaki
ndani au nje ya Muungano.
Katibu
mpya wa Baraza hilo, Raya Issa Msellem alisema muswada huo utasomwa kwa
mara ya kwanza na wajumbe watapata nafasi ya kuuchangia.