Dar es Salaam. Mwanzo wa safari yake ya mwisho ulikuwa kwenye lango la nyumba ya wageni ya Rubafu iliyopo Tabata Relini jijini hapa.
Aliingia
saa 8:00 mchana juzi, lakini juhudi zake za kutoka siku iliyofuatia
kuendelea na shughuli zake ziliishia kwenye lango hilo; alianguka na
kupoteza maisha papo hapo.
Kati
ya saa 8:00 mchana juzi na saa 2:00 asubuhi jana, mtu huyo
aliyejiandikisha kwa jina la Amani Daudi, aliomba maji ya kunywa ya
Sh700 na pombe kali ya kwenye pakiti, maarufu kwa jina la kiroba cha
Sh1,500 na baadaye aliondoka kwa saa tatu kabla ya kurejea akiwa
amelewa.
“Alikuwa
amelewa sana,” alidai mhudumu wa nyumba hiyo ya wageni, Sara Mwakyaba
akizungumzia hali aliyokuwa nayo Daudi wakati aliporejea usiku.
“Ilibidi nimwombe mhudumu mwenzangu aliyekuwa anaingia zamu ya usiku, amsindikize chumbani kwake.
Baadhi ya vyumba vilikuwa wazi kwa hiyo nilihofia angeweza kuingia bila kujua.”
Mhudumu
mwingine aliyemsindikiza chumbani usiku, Tulia Leonard Mwakyaba alisema
jana saa 2:00 asubuhi, Daudi alitoka chumbani kwake ili aondoke, lakini
aliuona mwili wake ukiwa umenyong’onyea.
“Nilimwambia akae nikamtafutie supu au mtori ili anywe kabla ya kuondoka, lakini akasema hana hela,” alisema Leonard.
Wakati wakiongea, kulikuwa na mteja mwingine ambaye ni mzee wa makamo aliyempa Leonard Sh5,000 ili amnunulie supu au mtori.
Leonard
alichukua hela na kutoka nje, kununua supu kwenye mgahawa uliokuwa
karibu na gesti hiyo, lakini wakati anatoka Daudi alianza kumfuata na
ghafla akasikia kishindo.
“Niligeuka
nyuma baada ya kusikia kishindo. Kukimbia namkuta Daudi amelala chali,”
alisema Leonard huku akionyoshea mkono kwenye geti alipomkuta Daudi
ameanguka.
“Nilikimbia kwenda kumwita dada (Mwakyaba),”alisema.
Mwakyaba
ambaye alisema tukio hilo ni mara ya kwanza kutokea Rubafu, alijaribu
kumgusa Daudi kuona kama angeitikia au kujigusa, lakini hakushtuka.
“Alikuwa tayari (amefariki dunia) siku nyingi,” alisema Mwakyaba.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Christopher Fuime alisema chanzo cha kifo chake ni kunywa pombe kupita kiasi.
Fuime alisema marehemu alianguka kutokana na kushindwa kujihimili na akagonga kichwa sehemu ya kisogo akiwa anatoka getini.
Kamanda
huyo alisema mwanaume huyo, ambaye vitambulisho vyake vinaonyesha
anaitwa Steve Weston Mloli (46), alifariki akiwa njiani kwenda
hospitalini na si eneo la tukio.
Mloli, ambaye mwili wake umehifadhiwa Hosptali ya Amana, ni derena na alikuwa mkazi wa Tabata Kimanga.
Hili
ni tukio la pili baada ya hivi karibuni mwanamke kufariki dunia akiwa
gesti kwa madai ya kulishwa sumu na mpenzi wake aliyekuwa ameongozana
naye.