Dar es Salaam.
Uhaba wa vifaatiba ni changamoto kwa Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya
Fahamu (Moi) kutokana na ongezeko kubwa la majeruhi wa ajali za bodaboda
waliolazwa kwa matibabu, imeelezwa.
Ilielezwa kuwa mtu mmoja aliyevunjika kutokana na ajali hiyo, huhitaji vifaatiba vya watu zaidi ya watano.
Akizungumza
katika mahojiano na gazeti hili jana, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa
Mifupa na Magonjwa ya Ajali wa Moi, Dk Kennedy Nchimbi alisema ongezeko
la majeruhi hao limesababisha uhaba wa vifaatiba katika taasisi hiyo kwa
sasa.
Dk Nchimbi alisema mwaka 2010 majeruhi wa bodaboda kwa upande wa madereva walikuwa 887, abiria 218 na watembea kwa miguu 254.
Alisema
kwa mwaka 2015, idadi ya madereva walioapata ajali za bodaboda
iliongezeka hadi kufikia 1,013, abiria 954, waliogongwa 401 na kufanya
idadi yao kuwa 2,268 kwa kipindi cha mwaka mmoja. “Ieleweke hawa ni wale
ambao hufanyiwa upasuaji wa mifupa hapa Moi, idadi hiyo hatujajumlisha
na wale ambao hupatiwa matibabu ya kawaida ambao hufikishwa katika
kitengo hiki baada ya kupata ajali,” alisema Dk Nchimbi.
Alisema
licha ya ongezeko hilo kutishia usalama wa usafiri wa bodaboda nchini,
kwa sasa kuna changamoto nyingine ya kupata mifupa mbadala hasa ya
nyonga na goti. Alisema mfupa wa nyonga umekuwa na gharama kubwa ambayo
hufikia hadi Sh12 milioni kwa mmoja.
Dk NChimbi alisema pia, kuna upungufu wa mashine za kupumulia majeruhi ambao hali zao ni mbaya baada ya kupata ajali.
Vilevile,
alisema taasisi hiyo ambayo imefanya upasuaji wa mifupa kwa watu 55,341
kwa kipindi cha miaka mitano, imekuwa ikielemewa hasa katika upande wa
chumba cha upasuaji wa dharura.
Majeruhi
wa ajali ya bodaboda, Aisha Milanzi (17) aliyelazwa hospitalini hapo
baada ya kupata ajali usiku wa Mei 22 kwa matibabu ya nyonga na mguu wa
kulia, alisema walikuwa wamepakizwa mshkaki na dereva mwenye miaka 17.