
Dodoma. Siku
moja baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga
kutimuliwa nafasi hiyo kwa ulevi, wabunge na wasomi wameendelea kumbana
zaidi wakisema hatua hiyo ya Rais imechelewa.
Wapinzani
wamekuwa wakimtaka Rais amuondoe kwenye nafasi hiyo kutokana na
kuhusishwa na Kampuni ya Infosys ambayo ilitoa ushauri kwa Kampuni ya
Lugumi Enterprises iliyopewa zabuni ya kufunga vifaa vya kuchukua alama
za vidole (AFIS) katika vituo vya polisi.
Wakati
wasomi wakisema hayo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema uamuzi huo
ulikuwa sahihi na swali ambalo Kitwanga hakulijibu vizuri kutokana na
hali ya ulevi, litapaswa kujibiwa upya baada ya wabunge kuomba mwongozo
wa swali hilo.
Majaliwa alisema Rais ametengua uteuzi wa Kitwanga kuanzia juzi baada ya kuonekana amelewa wakati wa kazi.
“Na hili lilibainika pale alipokuwa akijibu maswali ya wizara yake...,” alisema Majaliwa.
Alisema uamuzi wa Rais Magufuli umefuata kanuni za utumishi wa umma ambazo zinakataza mtumishi kulewa akiwa kazini.
Ingawa
Majaliwa hakutaja kanuni hiyo, Kifungu cha 34 cha Sheria ya Utumishi wa
Umma ya Mwaka 2002 pamoja na Kanuni ya 65 (1) ya Kanuni za Utumishi wa
Umma za Mwaka 2003, kinasema, “Watumishi wa Umma wanapaswa kuepuka tabia
ambayo inavunja heshima ya utumishi wao kwa umma hata wanapokuwa nje ya
mahali pa kazi.
Tabia
inayoweza kuvunja heshima hiyo inatajwa kuwa ni pamoja na matumizi ya
dawa za kulevya, ulevi, kukopa kwa kiwango ambacho hawawezi kurejesha na
mwenendo mbaya na kujihusisha na vitendo vyovyote viovu mbele ya jamii.
Bunge kuchukua hatua?
Katibu
wa Bunge, Dk Thomas Kashillilah alipoulizwa adhabu ambazo mbunge
anaweza kupata iwapo ataingia bungeni akiwa amelewa, alisema wanaoweza
kujibu hilo ni Waziri Mkuu ambaye ni kiongozi wa shughuli za Serikali
bungeni na Mnadhimu wa Serikali Bungeni, Jenister Mhagama.
Hata
hivyo, Mhagama ambaye ni Waziri Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,
Uratibu na Bunge, alisema hawezi kueleza hatua zinazopaswa kuchukuliwa
kwa kuwa tayari Rais ameshachukua uamuzi wa kutengua uteuzi huo.
“Ila Bunge lina taratibu na kanuni zake, nadhani Spika au katibu wa Bunge watakueleza vizuri,” alisema Mhagama.
Spika Job Ndugai hakupatikana kwenye simu, huku Naibu Spika simu yake iliita bila kupokewa.
Hata
hivyo, Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alisema: “Kanuni
hazijaweka utaratibu wa mbunge anayeingia bungeni amelewa ila kuhusu
suala la Kitwanga ni la nidhamu ya utumishi wa umma, labda kama atafanya
jambo ambalo siyo la kawaida.”
Wabunge ‘wampa za uso’
Wabunge
wa CCM na upinzani nao walitoa maoni kuhusu hatua hiyo wakisema ilikuwa
haki kwa waziri kuachishwa kazi kwani alikuwa ametia aibu Serikali huku
wakimpongeza Rais Magufuli kuwa yuko makini. Mbunge wa Kaliua (CUF),
Magdalena Sakaya alisema alichokifanya Magufuli ni kizuri na kwa sababu
waziri huyo alishindwa kujiwajibisha mwenyewe.
Sakaya
ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), alisema kitendo cha Dk
Magufuli kumtimua mtu wake wa karibu, ni ishara tosha kuwa amedhamiria
kuwasaidia wanyonge na kuwatahadharisha mawaziri wengine kuwa makini na
kazi zao.
“Huyu
waziri angeweza kujiwajibisha mwenyewe kutokana na makandokando yake,
lakini akachelewa na sasa amekutana na mkono wa Rais kwa kuwa hataki
uchafu, ni kweli jana (juzi) Kitwanga alikuwa amelewa wala siyo utani,”
alisema Sakaya.
Mbunge
wa Sumve, Richard Ndasa (CCM), alimpongeza Rais Magufuli kwa kuona
jambo hilo akisema, haiwezekani kufanya kazi na watovu wa nidhamu hasa
katika masuala ya ulevi.
Ndasa
alisema kulewa ni sehemu ya utovu wa nidhamu lakini inakuwa shida zaidi
pale viongozi wenye dhamana wanapolewa tena nyakati za kazi kwani
inakuwa ni mfano mbaya, hivyo waziri huyo amevuna alichopanda.
Ali
Saleh (Malindi – CUF) alisema Kitwanga alichelewa kuondolewa katika
nafasi yake kwani alikuwa ni miongoni mwa majipu. Alisema waziri huyo
alipaswa kuchunguzwa na Ikulu mapema baada ya kuanza kwa kelele za
wapinzani, lakini watu wengi walishindwa kumpa Rais habari za ukweli
kuhusu waziri wake. Alisema kutumbuliwa kwa Kitwanga kusitafsiriwe kwa
mambo ya ulevi pekee, maana wakuu wa mikoa na wilaya wataanza kufanya
hivyo kwa uonevu kwa watu ambao watakuwa wamewanyima hata pombe
vilabuni.
Joel
Mwaka (Chilonwa – CCM) alimpongeza Rais Magufuli kuwa ni mtu
anayeyaishi yale anayoahidi na hivyo kuwapa nafasi kubwa Watanzania na
hasa wa chini huku akitahadharisha viongozi kuacha kuwadharau watu wa
hali ya chini.
Suzan
Kiwanga (Mlimba – Chadema) aliyezusha sakata hilo, aliwalaumu wasaidizi
wa Kitwanga pamoja na dereva wake kwamba walishindwa kumshauri asiingie
bungeni.
“Hakuwa
katika hali ya kawaida, alilewa sana jamani hadi akashindwa kujibu
swali, ningeshauri Rais aangalie sana kwa mawaziri wake kwani wengi
wanaonekana kulewa hata madaraka na kujibu maswali kwa nyodo,” alisema
Kiwanga.
Mitandaoni
Jana
kutwa nzima, mitandao ya kijamii ilitawaliwa na taarifa za kutimuliwa
kwa Kitwanga ikiambatana na video yake wakati akijibu swali bungeni
katika hali ya ulevi.
Vilevile,
ilisambaa video ya Rais Magufuli wakati wa kampeni akimnadi mbunge huyo
Misungwi mkoani Mwanza, huku akieleza bayana kuwa ni rafiki yake wa
karibu ambaye walisoma wote chuo kikuu.
Pia,
kulikuwa na video nyingine iliyosambaa ikimuonyesha Kitwanga akifurahi
pamoja na Dk Magufuli huku akimpigapiga mabegani walipokuwa wakijadili
kuhusu joto linalohitajika kuyeyusha madini ambako baada ya maelezo
marefu, Kitwanga anasikika akimwambia Magufuli, “chukua fomu basi.” Naye
akajibu “fomu ya nini (vicheko), hebu nieleze... mimi watu watalimia
meno.”
Siri ya Kitwanga
Mmoja
wa wabunge wa karibu na Kitwanga kutoka Kanda ya Ziwa ambaye hakupenda
kutaja jina lake, alitoa sababu za kiongozi huyo kulewa akisema,
inatokana na mawazo mengi aliyonayo ya kufiwa na kijana wake wa kiume.
Mbunge
huyo alisema Kitwanga alikuwa na mtoto mmoja wa kiume ambaye
alimtegemea lakini tangu alipofariki hayuko kwenye hali nzuri na ndiyo
maana amekuwa akinywa pombe kupita kiasi.
Wasomi wamwandama
Kama
ilivyokuwa kwa wabunge wasomi na wachambuzi wa siasa wamesema Kitwanga
alitakiwa kuondolewa madarakani mapema, kutokana na kuhusishwa na kashfa
ya Lugumi.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema ni aibu
kwa waziri aliyetakiwa kuwa mfano wa kuigwa kwa jamii, kuingia bungeni
akiwa amelewa. Alisema licha ya tuhuma za ulevi, aliandamwa na kashfa
nyingine ikiwamo ya Lugumi jambo ambalo lilimuondolewa uaminifu kwenye
jamii na alistahili kuondoka madarakani.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI), Jimson Sanga alisema kwa kuwa waziri
alikuwa na kashfa nyingi, isingekuwa rahisi kwa Rais Magufuli kuendelea
kumuacha kwa sababu tayari alikosa sifa za uongozi.
“Kosa
la ulevi ambalo lingeweza kupelekwa kwenye kamati ya nidhamu ya Bunge
ndilo ambalo limemuondoa, maana yake isingekuwa rahisi kwa Rais
kumuondoa kwa kashfa ya Lugumi ambayo, bado ni kizungumkuti,” alisema.
Mhadhiri
mwingine wa UDSM, Profesa Kitila Mkumbo alisema kiuhalisia, Kitwanga
hakuwa na sifa za kuwa waziri kwenye wizara nyeti, kutokana na sifa yake
ya ulevi.
“Ukiniuliza
kama Kitwanga alikuwa na sifa za kushikilia wadhifa huo, nitakukatalia
kwa sababu hata kwenye kampeni zake kuna wakati alienda akiwa amelewa,
hivyo hakustahili kupewa wizara hiyo nyeti,” alisema.
Mchambuzi
wa siasa mkazi wa Iringa, Dk Frank John alisema ni wakati wa viongozi
waliopo madarakani kuheshimu nafasi zao kwa kufanya kazi kwa weledi na
uadilifu.
Mbunge
wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema alisema: “Eti wanadai
ametumbuliwa sababu ya ulevi, hebu jiulize Waziri wa Mambo ya Ndani ana
wasaidizi, ana mlinzi ana katibu ana dereva, huyu mtu aliyelewa kiasi
hicho katibu alishindwa kumwambia maana kazi yao ni kumsaidia waziri
asifanye mambo ya aibu. Sasa utawala uliofitinika hauwezi kusimama kamwe
kuongoza taifa,” alisema Lema.
Waziri
wa Zamani wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha alimpa pole Kitwaga
akisema, hata yeye alikuwa anakunywa ndovu akiwa waziri lakini hakuwahi
kutimuliwa.
“Namuonea
huruma Kitwanga kwa sababu alikuwa haijui CCM, kama ni pombe mbona hata
mimi nilikuwa nakunywa ndovu, nakijua chama hicho nilianzia chipukizi,
hata umoja wa vijana, lakini niliamua kutoka,” alisema Masha.
Imeandikwa na Habel Chidawali, Fidelis Butahe, Tumaini Msowoya na Beatrice Moses.
