
Dar es Salaam. Wakati
Serikali ikiendelea kupambana na jipu la sukari kutoka nje, uchunguzi
mpya wa Mwananchi umebaini kuwapo wafanyabiashara wanaoingiza mchele
usio na ubora kwa magendo kutoka nje na kisha kuuchanganya na ule
unaozalishwa nchini ili kuwa na thamani.
Uchunguzi
huo uliofanywa kwa mwaka sasa, umebaini kuwa mchele huo ukiwamo
unaopaswa kupita kwenda nje, huuzwa katika masoko ya ndani baada ya
kuchanganywa na unaozalishwa nchini.
Mchezo huu wa baadhi ya wafanyabiashara kutafuta faida chekwa kwa njia chafu, huathiri soko la mchele unaozalishwa nchini.
Waziri
wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amekiri kwamba kuna
bidhaa zisizolipiwa kodi katika bandari bubu za mwambao wa Pwani.
“Ni
kweli suala hilo tunalijua ndiyo maana sasa tunapambana na magendo hayo
kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi. Tunawaomba wananchi watoe
taarifa wanapoona uhalifu huo, ili tuudhibiti,” alisema Waziri Mwijage.
Kamishna
wa Kodi za Ndani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuf Salum
alisema mamlaka hiyo imejizatiti kupambana na biashara za magendo kwenye
bandari bubu.
“Unajua
tumedhibiti sana ukwepaji kodi katika bandari rasmi, ndiyo maana
wafanyabiashara wengi wanakimbilia kwenye bandari bubu. Hivi karibuni
Mamlaka imechukua hatua kali kwa kuwakamata baadhi ya wafanyabiashara
wanaotumia bandari hizo kukwepa kodi,” alisema Salum.
Hata
hivyo, msemaji wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Richard Kasuga
alisema biashara ya mchele ni huria kama zilivyo nyingine. “Hatujazuia
mtu kuingiza mchele au bidhaa yoyote ya chakula nchini. Kitu cha msingi
wanatakiwa kulipa asilimia 75 ya kodi.
“Mtu
yeyote anaruhusiwa kuingiza mchele kwa kuwa ni biashara huria, kwa hiyo
kama mtu anaona inampa faida hakatazwi. Ni kama biashara za maji,
juisi, magari na nyinginezo,” alisema Kasuga.
“Si
jukumu la Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kutoa vibali vya
biashara ya chakula, labda kama kuna baa la njaa. Kwa sasa chakula kipo
cha kutosha hakuna haja ya kutoa vibali.”
Ofisa
Biashara wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Christopher Nassari alisema
jukumu la wizara hiyo ni kutoa leseni za wafanyabiashara bila kujali
wanaagiza vyakula aina gani.
Meneja
uboreshaji na uhakikisho katika Kitengo cha Forodha TRA, James Mbunda
alisema kuna wafanyabiashara walioruhusiwa kuingiza mchele na hulipa
kodi. Katika kipindi cha mwaka 2013/ 2014 Tanzania iliingiza tani
22,231.8 na mwaka 2014/2015 mchele ulioingizwa ulifikia tani 32,661.2
wote kwa jumla uliingiza ushuru wa Sh29 bilioni.
Pia,
Tanzania ilisafirisha mchele wa tani 68,962.595 mwaka 2013/2014 na tani
24,600.330 mwaka 2014/2015 wote ukiwa na ushuru wa Sh58 bilioni.
“Mchele unaoingizwa kwa lengo la kusafirishwa nje ya nchi tunaufuatilia
kwa njia ya ‘cargo tracking system’ kuhakikisha unafikishwa
unakokwenda,” alisema Mbunda.
Ofisa
Uhusiano wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Gaudencia
Simwanza alisema ofisi yake haijawahi kusikia kitu kama hicho, hivyo
apewe muda wa kufuatilia.
Umoja wa forodha
Ili
kutekeleza Itifaki ya Umoja wa Forodha ya Afrika Mashariki, nchi
wanachama ziliondoa ushuru wa forodha kwa bidhaa zote zinazokidhi vigezo
vya uasili na kupewa cheti cha uasili. Bidhaa hizo, ukiwamo mchele,
hazitozwi ushuru wa forodha zinapouzwa ndani ya Jumuiya tangu Januari
2010.
Hata hivyo, Rwanda na Uganda zimerejesha ushuru huo ambao ni asilimia 75 kwa mchele kutoka Tanzania kwa kukosa imani nao.
Meneja
Mipango wa Baraza la Nafaka Rwanda, Ikunda Terry alisema Juni mwaka
jana kwamba hatua hiyo inalenga kuwabana wafanyabiashara wa mchele wa
Tanzania ikithibitika kwamba wamechanganya na ule usio na viwango kutoka
Asia.
Kauli ya wakulima
Mkulima
wa mpunga wa Mbarali – Mbeya, Loveness Stephano alisema japo mchele wa
nje haujaingia kwenye masoko ya mkoa huo, lakini unawaathithiri wengi
wanaosafirisha zao hilo nje ya mkoa.
“Huku
Mbarali mchele kutoka nje ya nchi haufiki, lakini wakulima wetu na
wafanyabiashara wanaoupeleka Dar es Salaam ndiyo wanaokumbana na hali
hiyo.
Mwenzake,
Daina Mwaisabila anaongeza kuwa wameathiriwa na mchele unaotoka nje ya
nchi hasa katika masoko ya Dar es Salaam wanakouzia mchele wao.
“Mchele
wetu una kiwango cha juu cha ubora ndiyo maana tunauza bei ya juu. Bei
zetu zinaanzia Sh1,500 hadi 1,650 kwa kilo. Zamani tulitegemea Soko la
Tandale, lakini kwa sasa kuna vituo vingi, unaweza kuuza kuanzia
Chalinze, Mlandizi, Kibaha, Kimara, Mwananyamala, Tandika, Mbagala na
hata Kigamboni. Lakini kwa kweli mchele wa Pakistan na Thailand
unatuathiri kwa kiasi kikubwa,” alisema.
