Katika hali isiyokuwa ya kawaida mtoto mchanga anayekadiriwa kuzaliwa akiwa na miezi mitano hadi sita amekutwa amekufa na kutupwa na mtu asiyejulikana katika mtaa wa Fumilwa ”B’’ Manispaa ya Morogoro ambapo serikali imeombwa kutoa adhabu kali kwa wale wote wanaobainika kuhusika na vitendo vya kutoa mimba na kuwatupa watoto wachanga.
Wakizungumza na ITV baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo wamesikitishwa na vitendo ambavyo vinafanywa na baadhi ya wanawake na kuiomba serikali kuweka sheria kali ambazo zitasaidia kukomesha vitendo hivyo vinavyozidi kushamiri kila kona ya nchi.
Mwenyekiti wa mtaa wa Fumilwa ’B’ kata ya mji mpya Manispaa ya Morogoro Said Ally amesema jitihada zinafanyika ili kubaini aliyefanya kitendo hicho kwa kufanya oparesheni huku akiwataka wananchi kutoa ushirikiano.
