WAZAZI na walezi wanaosomesha watoto wao katika Chuo cha Biblia Majahida kinachomilikiwa na Kanisa la Africa Inland (AICT) mkoani Simiyu, wameushangaa uongozi wa kanisa hilo kuendesha chuo hicho kwa miaka 50 bila usajili wa serikali.
Hali hiyo imefanya wahitimu wa mafunzo katika chuo hicho, kushindwa kupokewa na kuendelea na masomo ya vyuo vingine.
Wakizungumza katika sherehe ya Jubilee ya miaka 50 ya chuo hicho juzi wazazi hao walishangazwa na taarifa iliyotolewa na mkuu wa chuo hicho, Zakayo Bugota, kuwa chuo kilianzishwa mwaka 1966 na kimeshindwa kupata usajili kutokana na viongozi wa madhehebu hayo kutothamini elimu ya wanafunzi na kusababisha wakimaliza kushindwa kuendelea vyuo vingine.
“Tumekuwa tukipiga kelele kwa viongozi wetu kuhusu kusajili bila mafanikio viongozi wengi wamepita wa kanisa hili na vyuo vyote vinavyomilikiwa na Kanisa la AICT nchini havijasajiliwa kama wanavyofanya madhehebu mengine lakini sisi kama chuo tumeanza mchakato wa kukisajili,” alisema.
Baadhi ya wazazi hao Cosmas Alukito na Mikoloji Kisesa, walisema chuo hicho kinachotoa elimu ngazi ya stashahada kimekuwa kikilalamikiwa na wanafunzi waliopo katika chuo hicho kwani wamekuwa wakisoma huku wakiambiwa na walimu wao ni bora wakatafute chuo kingine ambacho kimesajiliwa na serikali kuliko kukaa hapo na kupoteza muda.
Mmoja wa walimu wa chuo hicho, Bela Kalumbete alisema mpaka sasa hakuna mikakati ya kusajili inayofanywa na uongozi wa kanisa hilo licha ya wanafunzi kulalamika.
Kalumbete alisema mpaka sasa wanafunzi waliopo katika chuo hicho ni 70, idadi inayosuasua kutokana na kukosa usajili kwani wanafunzi wengi hufika kutaka kusoma na wakielezwa hakijasaliwa wanaondoka na kutafuta vyuo vingine.
