» » Mjane asimulia mumewe alivyouawa

ILI UPATE HABARI ZETU KWA URAHISI BOFYA HAPA KUINSTAL APPLICATION YA MZALENDO HURU KWENYE SIMU YAKO

Mwanza. Muda wa saa 1:30 usiku, mwanamama Getrude Henrico (36), mkazi wa kijiji cha Bulale wilayani Nyamagana alisikia milio ya bunduki maeneo ya nyumbani kwake wakati akirudia kutoka shambani.

“Milio hiyo ilinichanganya. Nikaanza kutetemeka kwa hofu na nilipojaribu kukimbia kuwahi, miguu ilikuwa mizito,” anaanza kusimulia.

Anasema wakati giza likiingia, akiwa mita 100 hivi kutoka nyumbani kwake, aliwaona vijana wanne ambao hakuweza kuwafahamu waliopakizana kwenye pikipiki mbili wakitoka kwa kasi kichakani.

“Sikuthubutu kupiga kelele kwa sababu sikuunganisha milio hiyo ya bunduki nyumbani kwangu na vijana hao kutoka kwa kasi kichakani,” anasema Getrude katika mazungumzo maalumu na Mwananchi.

Anasema kibaya zaidi watu wengine waliokuwa wanakimbia kusalimisha roho zao walipomwona akiwa wanguwangu kuelekea nyumbani walimzuia asubiri hali itulie.

Ghafla Getrude alipata nguvu za ajabu akajipapatua na kuwatoroka waliokuwa wamemshika. Akatimua mbio hadi nyumbani ili kuwaona watoto wake kwa kuwa alikuwa akijua kuwa mumewe, Alphonce Mussa Nyinzi alikuwa kwenye vikao.

Lahaula! Alipofika nyumbani alikuta hali tofauti; watoto wake walikuwa salama lakini wakilia maana risasi zilizosikika jioni ile zilikatisha uhai wa baba yao mpendwa ambaye ni mumewe mpenzi.

Hivyo ndivyo msiba ulivyomfika mwanamama huyo aliyeachwa na watoto 15, wakiwamo 11 ambao Alphonce alizaa na wanawake wengine.

Katika mazungumzo hayo na mwandishi wa habari hizi nyumbani kwake Bulale, Kata ya Buhongwa wiki iliyopita, Getrude alisema laiti angehusisha haraka milio ya risasi na kitendo cha vijana wale kutokea vichakani, angepiga kelele wakamatwe.

Mwananchi: Je, ulijua aliyekuwa analengwa ni mumeo au ulijua baada ya kufika nyumbani?

Getrude: Sikujua chochote ila nilikuwa na hofu kwa sababu milio ya risasi mbili ilitokea hapa nyumbani, hivyo nilihisi kuna maafa lazima nirudi haraka.

Mwananchi: Je, kuna mtu unamhisi hapa kijijini anahusika na kifo cha mumeo?

Getrude: Kwa kweli hapana. Mume wangu hakuwa na ugomvi na mtu yeyote. Isipokuwa wakati natoka shambani huku nakimbia, niliwaona vijana wanne waliopakizana kwenye pikipiki mbili wakiondoka kwa kasi.

Mwananchi: Ulivyozitazama sura unahisi ni vijana wa hapa kijijini?

Getrude: Hapana. Vijana wale ni wageni.

Mwananchi: Wakiletwa leo unaweza kuwajua?

Getrude: Hapana siwezi kuwajua, sikushika sura zao.

Mwananchi: Kwa nini hukupiga kelele ili wanakijiji wenzako wakusaidie kuwakimbiza na kuwakamata?

Getrude: Mimi sikujua kama vijana wale ndiyo waliotenda uhalifu huu.

Mjane huyo alisema anajua kwamba kuna mtu mmoja ambaye wanagombania shamba kwa miaka 20 sasa na kesi iko mahakamani, lakini hadhani kisa kinaweza kuwa shamba hilo. Pia, alisema hana uhakika kama kifo hicho kinaweza kusababishwa na kazi yake ya uenyekiti.

Alisema hatima yake inategemea kikao cha wanandugu ambao pamoja na mambo mengine watajadili namna ya kuwatunza na kuwasomesha watoto 15, ambao wawili kati yao wapo sekondari.

Mjumbe wa halmashauri ya kijiji cha Bulale, Anthony Dillo aliyekuwa pamoja na Mussa wakirejea nyumbani, alisema aliwaona wauaji. Alisema vijana wawili waliokuwa wamebeba mabegi kama wanafunzi walikuwa wakitembea taratibu wakitokea usawa wa nyumbani kwa mwenyekiti.

Alisema baada ya vijana hao kufika mahali alipokuwa amesimama pamoja na mjumbe mwingine, mwenyekiti na wanandoa wawili, walipita lakini baada ya hatua tatu hivi waligeuka na kurudi na kufyatua risasi mbili zilizomuua mwenyekiti. “Sura za vijana wale, mmmh siyo wa humu walikuwa wageni,” alisema Dillo.

Dillo alisema kuwa baada ya risasi kupigwa kila mmoja alikimbia kujisalimisha na wauaji walitoweka na huenda walipita katikati ya msitu na kurudi walikotokea ambako walipanda pikipiki zilizokuwa zinawasubiri na kutokomea kama alivyoeleza Getrude.

Diwani wa Kata ya Buhongwa, Kabadi Joseph Bernard alisema tukio la mauaji ya mwenyekiti wa Bulale limekwamisha ulinzi shirikishi.

“Umekwama kutokana na hofu. Mioyo imekufa, hivi sasa tunaendelea na vikao ili kurudisha mioyo ya watu washiriki kwenye ulinzi,” alisema Bernard.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Kijiji hicho, Sajenti mstaafu Samadu Kigato, alitoa wito kwa Serikali kuona umuhimu wa kuanzisha kituo kidogo cha polisi katika eneo la Bulale-Rwandima ili iwe rahisi kupambana na wahalifu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi amesema wajibu wao ni kulinda watu na mali. Akizungumzia madai kwamba Mussa alikuwa na ugomvi wa mashamba, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella alisema polisi wanafanyia kazi tuhuma hizo zote.
ILI UPATE HABARI ZETU KWA URAHISI BOFYA HAPA KUINSTAL APPLICATION YA MZALENDO HURU KWENYE SIMU YAKO

About Unknown

About Mzalendo Huru Staff:

Send us your articles, questions, feedback, suggestions, press releases and all others to Whats app on +255657905751
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post