Dar es Salaam. Huku mashabiki wa Simba wakiisubiri TP Mazembe kupanga mikakati ya pamoja ya ushangiliaji dhidi ya Yanga wakati wa mechi ya Kombe la Shirikisho (CAF), Juni 28, watani zao wamedhamiria kutumia mbinu za ushangiliaji za Waarabu ili kuipa hamasa timu yao.
Mashabiki wa Yanga wameeleza kuwa mbinu sahihi za ushangiliaji ndizo ‘zitaua’ Mazembe hata ikiungwa mkono na Simba.
Vikundi vya ushangiliaji vya mashabiki wa Yanga leo usiku vitakutana Magomeni jijini Dar es Salaam kuweka mikakati ya kuizima Mazembe kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Viongozi wa vikundi hivyo tayari wamewasilisha mapendekezo kwa viongozi wao, wakitaka watoe taarifa polisi ili wanachama wao waruhusiwe kukaa mahali popote uwanjani kama zinavyofanya klabu za nchi za Kiarabu zinapocheza na wageni.
“Tumeambiwa Mazembe wana bendi inayopigwa uwanja mzima ukarindima, tumejiuliza tuifunike vipi,” alieleza kiongozi mmoja wa mashabiki wa Yanga.
Aliongeza kuwa mbinu yao ni kuhakikisha mashabiki wanajaa uwanja mzima, ikiwezekana hata nyuma ya lango la wapinzani ilimradi waruhusiwe na polisi ili kukaa popote na kutowapa nafasi wapinzani.
“Tayari, tumepeana majukumu na kesho (leo), viongozi wetu watakutana na moja ya ajenda ni namna tutakavyoidhibiti bendi ya ushangiliaji ya Mazembe, tumeanza kwa kuwaomba viongozi wetu wapeleke taarifa polisi ili kusitokee vurugu.
“Turuhusiwe kukaa uwanja mzima, kusiwapo jukwaa la Simba wala Yanga, kwani kwa kufanya hivyo tutawapa mwanya Mazembe kutamba wakati hiyo ni mechi yetu, hivyo mashabiki waruhusiwe kukaa popote, wawe huru kushangilia kama zinavyofanya nchi za Kiarabu.
“Kusiwepo na mvutano kati ya mashabiki na polisi, sisi hatutaki vurugu kwani zitatupoka pointi, kilichopo viongozi wetu watoe taarifa mapema kwa kuwa hii ni mechi ya kimataifa, mashabiki wetu waruhusiwe kukaa jukwaa lolote bila kuzuiwa na polisi,” alisema mmoja wa viongozi wa makundi ya ushabiki Yanga.
Alisisitiza kiongozi huyo kwamba tayari wameanza maandalizi na kwamba mkakati wao ni kuizima bendi ya Mazembe katika mchezo huo.
Wakati Yanga ikijipanga kuidhibiti Mazembe, watani zao, Simba wamesema wanaisubiri timu hiyo ya DR Congo ili kupeana mikakati ya namna ya kuwaunga mkono siku hiyo.
Mashabiki wa Simba wameeleza kwamba, Mazembe ni ndugu zao na wamekuwa wakifanya biashara pamoja kimichezo baada ya kuwauzia mshambuliaji Mbwana Samatta.
“Hatuna sababu ya kuiunga mkono Yanga, wao ndiyo walianza, sasa sisi tunamaliza, wapo mashabiki wao hadi leo wana jezi za Mazembe, tunachosema sasa, sisi tunawasubiri Mazembe waje ili tuone ni namna gani tutawasapoti,” alisema katibu wa kundi la ushangiliaji la Wekundu wa Ubungo Terminal.
Aliongeza kuwa Simba ina faida na Mazembe baada ya kuwauzia Samatta kwa faida ambaye alipouuzwa kwa RC Genk ya Ubelgiji, timu yao ilipata mgawo na kuongeza matumaini kuwa timu anayoichezea sasa ikimuuza, Simba itapata mgawo kupitia TP Mazembe, hivyo lazima kuwaunga mkono.
