» » MANJI : Wakati mwengine nalala ofisini kutokana na kazi

ILI UPATE HABARI ZETU KWA URAHISI BOFYA HAPA KUINSTAL APPLICATION YA MZALENDO HURU KWENYE SIMU YAKO


Dar es Salaam. Alipogombea udiwani katika Kata ya Mbagala Kuu jimbo la Mbagala, watu wengi walishindwa kuelewa dhamira yake. Wengi waliamini kuwa ni dhihaka, wengine walienda mbali zaidi na kusema pengine amelewa utajiri wake.

Baada ya kushinda, Yusuf Manji amethibitisha si suala la kusaka tonge lilomsababisha kugombea nafasi hiyo bali dhamira yake ni kuwa daraja kati yao na utawala ili kuwahudumia wananchi.

Dhamira hiyo inaonekana wazi kwa mfanyabishara huyu ambaye kwa sasa ametimiza miaka 41, lakini ameisaidia timu ya Yanga kwa kuifadhili kwa miaka mingi.

Manji ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa timu hiyo anasema kuwa anatumia kiasi cha Sh2.5 bilioni kutoka mfukoni kwake kuipiga tatu bajeti ya klabu hiyo kila mwaka.

MLini alianza kuongoza QGL?
Manji ambaye ni Mwenyekiti wa Kampuni ya Quality Group Limited (QGL) anasema safari yake ya kuongoza kampuni hiyo ilianza rasmi mwaka 1995 akiwa na umri wa miaka 20 baada ya kupokea mikoba kutoka kwa baba yake, Mehbub Manji aliyekuwa akiongoza kampuni ya vifaa vya magari.

Hata hivyo, Manji anasema yeye siyo tajiri na kwamba ni mfanyakazi tu katika kampuni hiyo na baada ya baba yake kufariki alimuachia hisa zote mama yake na yeye kubaki msimamizi anayelipwa mshahara kama wafanyakazi wengine.

Manji anasema kwa miaka 20 amemudu kuanzisha kampuni tanzu 17 ambazo zinajishughulisha na biashara 102 zikiwamo za maendeleo ya makazi, usambazaji wa vyombo vya moto, biashara ya kimataifa, vyakula na huduma za uchukuzi katika nchi 28 duniani.

Kwa mujibu wa mfanyabiashara huyo, usimamizi wa kampuni hizo haukuja kwa bahati mbaya kwake na badala yake ilikuwa ni matokeo ya kujituma kufanya kazi bila kuchoka kwa moyo wake wote.

“Mara kadhaa nimekuwa nikilala ofisini kwa siku tatu mpaka nne kutokana tu na kuwa na kazi nyingi, hili si wengi wanaoweza kuamini, lakini ndio ukweli kuhusu maisha yangu,” anasema.

Ratiba yake kwa siku
Manji anasema kwa kawaida huwa anaamka saa 10:15 usiku kila siku ili kuhakikisha hachelewi kazini kwani anaamini kulala sana ni dalili za uvivu.

“Ninapoamka tu naaza kwa kufanya mazoezi, kisha nasali na kuondoka nyumabani. Saa 12:00 asubuhi huwa nafika ofisini kwangu kwa ajili ya ujenzi wa Taifa,” anafafanua

Ataka kugombea ujumbe wa nyumba 10
Manji anasema baada ya kipindi chake cha udiwani kuisha hana mpango tena wa kugombea nafasi hiyo na badala yake atajikita katika ujumbe wa nyumba 10.

“Sina mpango wa kugombea tena udiwani wala ubunge lengo langu ni kurudi chini zaidi kwa wananchi, niweze kukaa nao nivute sigara nao pamoja tuzungumze masuala yanayotuhusu,” anasema.

Manji anasema endapo watamshawishi kugombea ubunge hatagombea jijini Dar es Salaam na badala yake atachagua jimbo lenye umaskini mkubwa ili aweze kuwasaidia wananchi wake kujikwamua na hali hiyo.

Anaongeza kuwa karibu na watu hasa wale wanaomzunguka, ni miongoni mwa mambo anayoyafurahia zaidi katika maisha yake na kwamba hata awapo kazini hupendelea kukutana na wafanyakazi walio chini yake na hivyo kubadilishana nao mawazo angalau mara moja kwa mwaka.

Manji anasema kutokana na hali hiyo alianzisha siku ya kampuni yake inayoitwa, Siku ya QGL ambapo huwa anapata wasaa wa kukutana na wafanyakazi wote wanaohudumu katika kampuni mbalimbali zilizo chini ya QGL, wanafurahia mafanikio yao kwa pamoja na pia kuangalia ni jinsi gani wanaweza kupiga hatua na kwenda mbele zaidi kama timu pja.

Mapenzi yake kwa timu ya Yanga
Yusuf Manji ni miongoni mwa wadau wakubwa wa timu ya Yanga nchini. Licha ya kutoonekana uwanjani mara kadhaa timu hiyo inapocheza, lakini anasema si mara zote hupenda kuangalia timu hiyo inapocheza.

“Unaweza usiamini mimi siwezi kusikiliza au kuingalia inapocheza iwe uwanjani au katika televisheni kwa kuwa sitaki ugonjwa wa moyo. Lakini ukweli ni kwamba napenda mpira na naipenda zaidi Yanga… Natumia fedha nyingi kwa ajili ya timu hii nje ya ule utaratibu wa kawaida,” anasema.

USULI
Yusuf Manji (41) ni mfanyabiashara nchini na Mwenyekiti wa Quality Group Limited (QGL) ambayo hujishughulisha na biashara 102 katika nchi 28 duniani.

Hata hivyo, atastaafu rasmi nafasi yake kwenye QGL mwezi ujayo.

QGL ni miongoni mwa kampuni kubwa nchini yenye takriban kampuni tanzu 17 katika nchi hizo ambazo hujishughulisha na biashara mbalimbali zikiwamo maendeleo ya makazi, usambazaji wa vyombo vya moto, biashara ya kimataifa, vyakula na huduma za uchukuzi

Manji ameoa na ana watoto wawili.
Anatajwa kuwa ni miongoni mwa matajiri 10 nchini wanaojulikana sana na jamii na kujitokeza mara kwa mara kwenye shughuli za kijamii kama michezo ambapo sasa ni Mwenyekiti wa klabu ya mpira ya Yanga.

Kwa mujibu wa Manji hutumia hadi Sh2.5 bilioni ya fedha zake kuongeza katika bajeti ya klabu hiyo kila mwaka.
ILI UPATE HABARI ZETU KWA URAHISI BOFYA HAPA KUINSTAL APPLICATION YA MZALENDO HURU KWENYE SIMU YAKO

About Mashak

About Mzalendo Huru Staff:

Send us your articles, questions, feedback, suggestions, press releases and all others to Whats app on +255657905751
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post