» » Malecela: Rais Magufuli asilinganishwe na Sokoine

ILI UPATE HABARI ZETU KWA URAHISI BOFYA HAPA KUINSTAL APPLICATION YA MZALENDO HURU KWENYE SIMU YAKO


Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela akisisitiza jambo alipokuwa akifanya mahojiano maalumu na gazeti hili nyumbani kwake mjini Dodoma hivi karibuni. Picha ya Maktaba 

Waziri Mkuu na Makamu wa kwanza wa Rais mstaafu Dk John Malecela, bado anayoimani kuwa Tanzania iko katika hali nzuri na anawaomba Watanzania waache tabia ya kujilinganisha na mataifa mengine.

Akizunguma na gazeti hili katika mahojiano maalumu nyumbani kwake eneo la Kilimani, makamu mwenyekiti huyo mstaafu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) anasema safari ya kimaendeleo kwa Tanzania iko katika nafasi nzuri.

Mzee Malecela anasema kuwa suala la kimaendeleo linamchakato mrefu na safari yake huwa ndefu, hivyo anataka Watanzania waamini kuwa wako katika nafasi nzuri, ingawa anakili kuwa hawajafika wanakokwenda.

Mwanasiasa huyo anasema kuwa hali ilivyo kwa sasa ni wazi kuwa mambo matatu aliyoyasema Mwalimu Julius Nyerere ya ujinga, maradhi na umaskini yamepungua kwa kiasi kikubwa tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Kwa mujibu wa Mzee Malecela, mambo hayo yanapungua kutokana na Taifa kuwa katika umoja, amani, utulivu na maendeleo ambayo ndiyo nguzo za nchi yoyote inayotaka kusonga mbele kimaendeleo.

“Kwenye maendeleo hatuwezi kusema hapa inatosha, inabidi kuongeza juhudi za kusonga mbele zaidi ikiwa ni pamoja na kushikamana na kuendelea na amani na utulivu wetu uliodumu kwa muda mrefu,” anasema.

Ameomba Watanzania kuacha kujilinganisha na mataifa ya Korea na Malaysia ambako anasema nchi za Magharibi zilipeleka misaada mingi zamani lengo likiwa ni kupinga soko la China ambao walianza kujitanua zaidi na hivyo wakafanya mataifa hayo kuwa na maendeleo ya haraka tofauti na Tanzania.

Elimu

Akizungumzia suala la elimu, anasema bado kuna changamoto kwa vijana wa Kitanzania na kuwa inahitajika msukumo wa haraka kwa baadhi ya makabila kusaidiwa ili vijana wao waweze kusoma kikamilifu.

Anaitaka Serikali kuendelea kuandikisha watoto wa kuanza shule ya msingi hata kama hakuna madawati wala vyumba vya madarasa, lakini wanaweza kukaa chini ya miti na elimu ikaendelea kutolewa.

Kiongozi huyo anawapinga wanaobeza mpango wa Serikali kwa kila hatua na anasema elimu inayotolewa hapa ni nzuri na kupitia mpango uliopo kwani wapo waliosoma kupitia njia hii wamefikia hatua ya kuwa maprofesa. Amesema kauli za kuwa elimu ya Tanzania inakwenda chini siyo nzuri kwani tukisema hivyo ni lazima kufanya tathimini Taifa lilitoka wapi, lipo wapi na linakwenda wapi, hivyo akasema ni vyema kuitia moyo Serikali kwa hatua iliyopigwa.

Umeme

Kwenye suala la umeme anakosoa kuwa mipango ya Kitaifa haikuwekwa vizuri tangu mwanzo kwa kuishi kwa kutegemea umeme wa maji ambao umekuwa na shida wakati wote. Anakumbuka wakati nchi ikipata uhuru idadi ya Watanzania ilikuwa ni ndogo ndiyo ambayo ilitosheleza mahitaji ya umeme kwa wakati huo, lakini kadri siku zilivyozidi kwenda ndipo matatizo ya kukatika kwa umeme yakaanza kuonekana.

“Tangu mwanzo tulijisahau utafikiri tulikuwa na mawasiliano na Mungu, hili siyo jambo jema hata kidogo inabidi kujipanga vizuri katika suala hili na kujenga miundombinu mizuri ikiwemo kutafuta vyanzo vingine vya umeme sio kuangalia maji pekee,” anasema.

Serikali kuhamia Dodoma

Malecela anaitaka Serikali kuamua kwa dhati kuwa sasa ni wakati mwafaka wa kuhamishia shughuli zote mkoani Dodoma kwa madai kuwa mkoa huo kwa sasa unaweza kuipokea Serikali tofauti na ilivyokuwa kipindi cha nyuma.

Anasema mji umejengeka na miundombinu yake ikiwamo suala la maji ambalo lilikuwa ni shida kwa kipindi cha nyuma ambacho anasema wakazi wa mji huo walikuwa ni chini ya 35,000 na walitegemea maji yaliyopelekwa kwa treni, lakini sasa kuna wakazi zaidi ya milioni moja na wote wanapata majisafi na salama.

Amzungumzia JPM

Kwa maoni yake kile kinachofanywa na Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, John Magufuli ni kizuri ikiwamo kazi ya kufikiria habari za maendeleo na uwajibishaji wa wazembe ndani ya Serikali. Hata hivyo, anapinga suala la kumfananisha Dk Magufuli na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Sokoine akisema kila mtu anasimama pekee yake na haiwezekani kumlinganisha mtu na mtu mwingine. Kwenye mchakato wa kugombea nafasi ya Urais hajutii kutoshwa kwani anasema demokrasia ndiyo iliyotumika zaidi na hana mashaka na hilo ndani ya CCM.

Maisha yake kwa sasa

Malecela anaishi kwa kutegemea kilimo na mifugo na hasa kilimo cha mtama, uwele na zabibu katika mashamba yake yaliyopo wilaya za Chamwino na Kongwa.

Analima mtama kwa wingi ambalo ni zao linalokubaliana na hali ya hewa ya Mkoa wa Dodoma na amekuwa akivuna zaidi kuliko wakulima wengine ambao wanalima mahindi katika mashamba makubwa.

Kwa mujibu wa maelezo yake, anatumia muda mwingi kwa ajili ya kuwaelimisha na kuwahimiza wakulima wenzake kutumia mashamba yake kama mashamba darasa ili watu waachane na kilimo cha mahindi badala yake walime mtama ambao unavunwa kwa wingi kwenye ardhi ya Dodoma.

Anasema mazao ya biashara anayolima ni alizeti na zabibu ambayo yote hulima kwa kufuata ushauri wa kitaalamu na ndiyo maana anavuna kwa wingi katika eneo dogo.

Ushauri kwa Serikali ni kuingalia Dodoma kwa jicho la huruma ili wafikie katika mipango ya kuwa na kilimo cha umwagiliaji kuliko kutegemea Mvua kwani mkoa umekuwa ukipata mvua chache tena kwa baadhi ya maeneo jambo linalofanya njaa iote mizizi mkoani hapa.
ILI UPATE HABARI ZETU KWA URAHISI BOFYA HAPA KUINSTAL APPLICATION YA MZALENDO HURU KWENYE SIMU YAKO

About Mashak

About Mzalendo Huru Staff:

Send us your articles, questions, feedback, suggestions, press releases and all others to Whats app on +255657905751
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post