Mwanza.
Shauri la kupinga amri ya polisi ya kupiga marufuku maandamano na
mikutano ya kisiasa iliyofunguliwa na Chadema katika Mahakama Kuu Kanda
ya Mwanza inaanza kusikilizwa mchana huu baada ya kupangiwa jaji.
Msajili wa wilaya wa mahakama hiyo, Francis Kabwe amesema shauri hilo linasikilizwa na Jaji Mohamed Ngwae.
Katika
madai yake ya msingi, Chadema kupitia kwa Mwenyekiti wa wa chama hicho,
Freeman Mbowe inaiomba mahakama kutangaza kuwa amri ya polisi ni batili
na utekelezaji wake pia ni batili kwa sababu inakiuka katiba na sheria
ya vyama vya siasa inayoruhusu uhuru wa mawazo, kukusanyika, kutoa maoni
na demokrasia.
Chadema
pia inaiomba mahakama kutoa katazo la kimahakama kwa polisi dhidi ya
amri kama hizo na pia iviruhusu vyama vya siasa kuendelea na shughuli za
kisiasa, ikiwamo maandamano na mikutano ya hadhara huku polisi
wakiamriwa kutoa ulinzi kama sheria inavyoelekeza.