
Dar
es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetangaza
kuanza ziara nchi nzima ya kuwaelimisha wananchi juu ya ubakwaji wa
demokrasia wanakodai kufanywa na Serikali.
Pia,
katika ziara hiyo, viongozi wa chama hicho watazungumzia utumbuaji
majipu wanaodai kuwa haufuati maadili ya kazi pamoja na kutoonyeshwa kwa
matangazo ya moja kwa moja ya televisheni ya vikao vya Bunge
vinavyoendelea Dodoma.
Mratibu
wa ziara hiyo, Singo Benson alisema ziara itaanza Juni 7 katika Wilaya
ya Kahama mkoani Shinyanga na kuendelea mikoa mingine.
“Wananchi
wananyimwa haki ya msingi ya kutoona matangazo ya Bunge moja kwa moja
na hakuna sababu ya msingi iliyotolewa, hivyo lazima tuwaelimishe na
tutetee haki ya wananchi,” alisema Benson.
Aliongeza
kuwa katika utumbuaji majipu unaofanyika, umekuwa kwa asilimia kubwa
ukilenga majipu madogo (viongozi wa chini) na kuacha viongozi wakubwa
mafisadi bila kuchukuliwa hatua yoyote.
Benson
alitoa mfano wa ubakwaji wa demokrasia akisema ni kitendo cha Serikali
kuingilia mihimili mingine, Bunge na Mahakama, ambapo kwa Bunge Serikali
inadaiwa kuingilia uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Hesabu za Serikali (PAC) ambaye anatakiwa kutoka kambi ya upinzani.
Alisema
ziara hiyo itamjumuisha Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na
Katibu Mkuu wake, Dk Vincent Mashinji, itakuwa na awamu nne huku wabunge
wote na wajumbe wakuu wa chama watashiriki, akiwamo aliyekuwa mgombea
urais 2015, Edward Lowassa.
