Wiki iliyopita tuliwaletea maswali na
majibu ya Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Dk. Khamisi Kigwangalla ambapo alieleza mengi. Leo anazidi
kufafanua mambo mbalimbali, fuatana nasi:
Hivi sasa kuna shida ya upatikanaji wa
dawa hasa katika zahanati vijijini na mijini, wizara ina mpango gani wa
kuhakikisha dawa zinapatikana?
Jibu: Serikali ina mpango mzuri
kuhakikisha vituo vya afya vijijini na zahanati zinapata dawa, chanzo
cha kupatikana dawa ni wateja wao kuchangia au kwa kuchangia mfuko wa
jamii na halmashauri. Tumekuja na suluhisho la kutaka wananchi waingie
mfuko wa jamii wa afya au bima ya afya.
Tunaboresha huduma hiyo kwani kadi ya
afya itakuwa na uwezo wa kutumika hadi kwenye hospitali ya mkoa.
Tunataka kila mtu achangie huduma hii ili mfuko wa afya ukue na asilimia
67 za fedha ziingie kwenye bajeti ya dawa, hivyo dawa zitakuwepo tu.
Tumegundua dawa hizi, baadhi ya watendaji vijijini wanaiba au kugawana.
Niwaonye, tukiwakamata tutawapeleka mahakamani.
Mpango mpya ni kwamba dawa zote za
serikali zitakuwa na logo ya serikali, rangi maalum na asilimia 5 ya
mapato watapewa Kamati ya Afya ya Kijiji ili kuwapa motisha wa
kuzisimamia.
Kamati itatakiwa kubandika kwenye ubao wa matangazo taarifa ya dawa zilizoingia na zikiisha wabandike tena kwenye ubao huohuo wananchi wajue njinsi dawa zilivyotumika.
Kamati itatakiwa kubandika kwenye ubao wa matangazo taarifa ya dawa zilizoingia na zikiisha wabandike tena kwenye ubao huohuo wananchi wajue njinsi dawa zilivyotumika.
Kuna ishu ya vipodozi feki hasa kwa
wanawake maarufu kwa jina la ‘Mchina’ ambayo inashika kasi mjini na vina
madhara kwenye miili yao, wizara inafanya nini kukomesha uingizaji wa
vipodozi hivyo?
Jibu: Ili kuingiza vipodozi ni lazima
kusajiliwa. Ni kosa kutosajili vipodozi, vinasajiliwa na TFDA (Mamlaka
ya Chakula na Dawa). Kabla ya kusajiliwa lazima vikaguliwe na TBS
(Shirika la Viwango Tanzania), TFDA na Mkemia Mkuu wa Serikali.
Watakaokutwa na vipodozi visivyosajiliwa na kuwa na vibali, watakamatwa
na watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Sasa tugeukie suala la matabibu wa tiba asili, wizara ina utaratibu gani wa matabibu hawa kujitangaza?
JIBU: Upo utaratibu wa kujitangaza.
Awali tulizuia matangazo yao lakini Waziri wa Afya (Ummy Mwalimu) ametoa
miezi mitatu waendelee kutangaza kibinadamu kwa kujua kuwa kuna wengine
wana mikataba katika vyombo vya habari wanavyotangaza.
Kwani baada ya miezi mitatu hawatakuwa wanajitangaza?
JIBU: Hapana. Itatakiwa wafuate
utaratibu. Tabibu ili atangaze dawa zake au biashara yake, atatakiwa
apeleke tangazo lake kwenye Baraza la Tiba Asili ili lihakikiwe kwanza
kabla ya kutangaza. Tumefanya hivyo kuzuia watu wasio na ujuzi kufanya
kazi za kidaktari kwa mfano, kuna wengine walikuwa na tabia za
kuwaingiza vidole watu sehemu nyeti huku wakijua kuwa hawana ujuzi wa
kutambua magonjwa kwa njia hiyo. Kwanza huo ni udhalilishaji.
Kuna utaratibu gani unaotakiwa kufuata ili tabibu wa tiba mbadala dawa yake iweze kusajiliwa na serikali?
JIBU: Ili dawa isajiliwe, utaratibu wa
sasa ni kwamba mpaka ziende maabara, TBS, kwa Mkemia Mkuu wa Serikali na
TFDA kufanyiwa utafiti.
Nini mikakati yako kuhusiana na changamoto mbalimbali jimboni kwako za kuwaletea maendeleo wapiga kura wako?
JIBU: Nina mikakati mingi ya kuwawezesha
kiuchumi wapiga kura wangu. Tunataka kutengeneza vikundi mbalimbali
kama vile vya kuzikana, kukausha mbogamboga, vikundi vya miradi kama
vile vya bodaboda na tunawagawia pikipiki kwa awamu ili wajiajiri,
vikundi vya kukamua alizeti ili wauze mafuta, mradi wa pamba ili wawe na
zao la biashara. Wanawake tunawaangalia zaidi kwa sababu wakiwa na
kipato hawanyanyasiki.
Tunatarajia kujenga shule tano za High
School (kidato cha tano na sita), katika hilo bado shule tatu, mbili
zipo tayari na nitazindua.Tunaboresha kiwango cha elimu, tumepata walimu
wengi na tutawapelekea huduma za intaneti na mitandao ya simu huko
vijijini pamoja na watumishi wa afya ili kuwapa motisha ya kuwahudumia
wapiga kura wangu. Tutajenga kambi kwa ajili ya wanafunzi wanaofanya
mitihani kwa mwaka husika lakini pia tutaboresha vituo vitano vya afya,
kimoja tutahakikisha kinakuwa na chumba cha upasuaji.
Vipi kuhusu changamoto ya barabara, umeme na maji katika jimbo lako?
JIBU: Hizo zipo. Tutaboresha barabara za
vijijini, tutaweka makalavati sehemu korofi. Tutahakikisha vijiji
vinapata umeme wa uhakika. Kuhusu maji tutachimba visima, asilimia 65
tumechimba kwa fedha zangu na wafadhili na halmashauri bado tutawaomba
wafadhili wengine kutusaidia kutanzua tatizo hili.
Asante kwa ushirikiano wako.
SOURCE:GP
