Kijana Noel Lazaro akiugulia.
DAR ES SALAAM: Kijana mmoja
mwenyeji wa Kijiji cha Mangamba mkoani Mtwara, Noel Lazaro (26)
amelalamika kuwa anateseka kwa maumivu na huenda akapoteza maisha akiwa
katika Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam kwa kukosa
shilingi 200,000 zinazotakiwa ili kuondoa vyuma mgongoni mwake.
Akizungumza na gazeti hili hospitalini
hapo, Lazaro alisema awali alipata ajali ya Bajaj huko kwao na kupelekwa
katika Hospitali ya Ligula, ambao walimpa rufaa ya kupelekwa Muhimbili
alikofanyiwa upasuaji wa mgongo na kuwekewa vyuma.
“Nilikuwa siwezi kukaa wala kufanya
chochote, kutokana na uduni wa hali yangu, baada ya kufanyiwa upasuaji
nilirudi nyumbani Mangamba, Mtwara lakini sikuweza kuja Muhimbili kila
mara kwa sababu sikuwa na fedha za nauli,” alisema kwa masikitiko kijana
huyo.
“Yaani nilikuwa kwenye wakati mgumu,
maumivu makali sana na hata haja kubwa ikitoka hadi sasa huwa sijielewi
hadi ninapojiona nimechafuka, sikuweza kuwa nakuja kliniki kila mara
kutokana na umaskini,” alisema huku akidondosha machozi.
Kijana alisema alimpata mfadhili,
alijitolea na kumpa msaada hivyo akaweza kurejea Muhimbili kwa ajili ya
kufanyiwa upasuaji wa kuondoa vyuma, lakini kwa bahati mbaya alipofika
alitakiwa kutoa shilingi 200,000 ili aweze kufanyiwa upasuaji huo.
“Nimeshamaliza mwezi mzima hapa
Muhimbili sijafanyiwa upasuaji kwa sababu fedha hizo zakulipia gharama
sina, niko hapa nateseka, nina vidonda mgongoni mpaka hivi sasa
havijapona na hapa sina ndugu, naishi kwa tabu na maumivu makali,”
alisema Lazaro.
Ndugu msomaji, ikiwa umeguswa na tatizo
la kijana huyo unaweza kuwaliana naye kwa simu namba 0676 299025 ili
uweze kumsaidia aweze kutibiwa.
source:GP
