
Dar es Salaam.
Mfanyabiashara maarufu wa Magomeni Makanya amekamatwa akiwa nyumbani
kwake kwa tuhuma za kukutwa na kilo moja ya dawa za kulevya zenye
mchanganyiko wa aina ya heroin na cocaine.
Mfanyabiashara
huyo, Omary Kaunga (49), alikamatwa Mei 17 akidaiwa kufunga dawa hizo
kwenye nailoni, akiwa tayari ameshatengeneza pipi 66 kwa ajili ya
kusafirishwa.
Kamanda
wa Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Mihayo Msikhela
alisema walipewa taarifa na raia mwema kuwa mtuhumiwa huyo huwa anafanya
biashara ya dawa hizo.
Msikhela alisema baada ya kupewa taarifa hizo, Jeshi la Polisi lilipitia Serikali ya Mtaa huo kwenda kumkamata mtuhumiwa huyo.
“Tulifika
nyumbani kwa mtuhumiwa huyo na kufanya upekuzi. Tulibaini dawa hizo za
kulevya kazifunga kwenye nailoni mfano wa pipi ambazo zilikuwa 66 zenye
uzito wa kilo moja,” alisema Msikhela.
Alisema
baada ya kuzikamata, zilipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali na utafiti
wa awali umebaini kuwa ulikuwa mseto kati ya cocaine na heroin.
Msikhela alisema upelelezi umekamilika na wanatarajia kumfikisha mtuhumiwa huyo Mahakama ya Kisutu.
Kamanda
huyo alitoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili
liweze kuwakamata watu wanaojihusisha na biashara ya dawa hizo ambazo
zimepigwa marufuku.
Alisema
Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vya usalama na wadau wa
kudhibiti dawa hizo, wamejipanga ili kupambana na wafanyabiashara wa
dawa hizo.
