Dar
es Salaam. Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amemtaka
Rais John Magufuli kukabiliana na vikundi vya mafisadi vinavyoiba
mabilioni ya fedha za umma kupitia mikataba mibovu waliyoingia badala ya
kuishia kutumbua majipu.
Zitto
alitolea mfano wa kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow kuwa bado kuna
kampuni inayolipwa Sh8 bilioni kila mwezi kwa ajili ya mitambo yake ya
umeme. Pia, alisema kashfa ya hati fungani imeongeza deni la Taifa kwa
Sh1.2 trilioni.
“Bado
huo mtambo upo chini ya matapeli na kila mwezi Serikali inawalipa Sh8
bilioni wazalishe au wasizalishe umeme. Hivi ndivyo vikundi masilahi
katika sekta ya nishati. Bila kuvibomoa, Rais ataonekana anachagua watu
katika vita hii,” alisema Zitto.
Alisema:
“Ni kweli kuna watu tayari wamefikishwa mahakamani kwa rushwa ya Dola 6
milioni za Marekani zinazohusu hati fungani. Serikali imewafikisha
mahakamani madalali wa rushwa lakini waliotoa rushwa hiyo hawapo
mahakamani. Waliopokea rushwa ambao ni maofisa wa Wizara ya Fedha
hawajashtakiwa.”
Zitto
ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini, alisema vita ya ufisadi siyo ya
kutumbua majipu tu, bali kujenga mfumo madhubuti wa kuzuia mianya ya
rushwa.
Alisema Rais Magufuli anapaswa kuwaongoza Watanzania katika vita ya kukataa mikopo kama hiyo ambayo inawasababishia umaskini.
Aungana na hoja za upinzani
Zitto
alisema chama chake kinaungana na vyama vingine vya upinzani kwa hoja
walizozitoa baada ya kutoka bungeni za kutokuonyeshwa moja kwa moja kwa
matangazo ya televisheni kutoka bungeni, matumizi ya Serikali nje ya
mpango wa bajeti na Serikali kutokuwa na mwongozo kwa mawaziri wake.
Akizungumzia
kusitishwa kwa urushaji wa matangazo ya Bunge, Zitto alisema hatua hiyo
inatakiwa kupigwa vita kwa sababu inajenga udikteta katika nchi na
kuwanyima wananchi haki ya kupata habari za Bunge. “Ina maana TV
zinapaswa kumuonyesha mtu mmoja tu akihutubia bungeni ambaye ni Rais
tu... hapana hii siyo sawa,” alisema Zitto na kuongeza:
Akizungumzia
suala la bajeti, Zitto alisema hakuna sheria yoyote inayompa mamlaka
Rais kuhamisha fedha kwenda kufanya shughuli nyingine. Lakini alisema
tangu Rais Magufuli achaguliwe, amekuwa akihamisha fedha wakati Bunge
lilishapitisha bajeti.
“Rais
Magufuli kwani amekuwa waziri wa fedha, waziri wa ujenzi na Rais kwa
wakati mmoja? Tunamtaka asiingilie majukumu ya mihimili mingine,
wananchi tumnyooshee kidole na kumwambia afuate utaratibu,” alisema
Zitto.
Mbunge
huyo pekee wa chama hicho, alisema tangu walipoapishwa, mawaziri
hawajapewa mwongozo wa kazi na kutoa wito kwa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali kutoa miongozo kwa mawaziri.
“Mpaka
sasa nchi haina mawaziri kwa sababu hawajapewa miongozo. Kwa hiyo,
Baraza la Mawaziri lina mawaziri wawili tu ambao ni Rais na makamu
wake,” alisema Zitto na kulitaka Bunge kutengeneza mfumo wa kuisukuma
Serikali kutekeleza mambo muhimu kwa Taifa.
Kuhusu
hali ya uchumi, Zitto alisema bajeti ya mwaka huu imeongezeka mpaka
kufikia Sh29 trilioni lakini ana wasiwasi itakwama kwa sababu theluthi
moja ya mapato ya ndani yanatoka bandarini ambako ripoti zinaonyesha
kuwa yamepungua.
Alisema
Serikali imepanga kukopa Sh7 trilioni kwa ajili ya utekelezaji wa
bajeti na kwamba hatua hiyo inazidi kuongeza deni la Taifa ambalo
limelalamikiwa pia na Mkaguzi na Mdhibiti wa Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG) katika ripoti yake.
