NAHODHA WA SIMBA, JONAS MKUDE.
Taarifa ya Mkude iliyosambazwa na Ofisa Habari wa klabu hiyo, Hajji Manara, ilisema jana kwamba kuna taarifa ya upotoshwaji inayosambazwa mitandaoni ikisema wachezaji wa timu hiyo wanadai mishahara ya miezi miwili kitu ambacho si cha kweli.
“Taarifa hizi za uzushi zinasema hiyo ndio sababu timu haifanyi vizuri. Napenda kuwataarifu wanachama na mashabiki wetu kuwa, taarifa hizo ni za uongo mkubwa na zenye lengo baya la kutuondoa katika nia yetu ya kuipa ubingwa Simba na tunaamini anayesambaza taarifa hizo anatumika na wapinzani wetu,” alisema Mkude kwenye taarifa hiyo.
Aidha, Mkude alisema haiingii akilini timu inayoongoza ligi na ambayo imefuzu hatua ya 16 bora ya kombe la Shirikisho nchini (FA) itajwe kuwa inafanya vibaya.
Katika hatua nyingine, Kikosi cha Simba kimeingia kambini jana maeneo ya Mbweni nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wa ligi kuu dhidi ya Azam Januari 28, mwaka huu.