Trump kwenye hotuba yake alisema taifa hilo kwa muda mrefu limehangaikia masuala ya mataifa mengine lakini likasahau kustawisha maisha ya watu wake.
Sasa akasema Marekani kwanza, tutafanya yale yanayoihusu nchi yetu, tumezitajirisha sana nchi zingine na sasa ni zamu ya Wamarekani. “Wamarekani mlisahauliwa kwa muda mrefu na sasa ni zamu yenu,”
Je kuingia kwake katika Ikulu ya White House kuna maana gani kwa nchi tofauti za Afrika, tuangalie sehemu fupi ya hotuba yake ambayo kwa tafsiri ya haraka inaonyesha kuwa Waafrika waliozoea misaada wajiandae kufunga mkanda.
“Siku hii ya Januari 20 mtaikumbuka kama siku ambayo mmerejeshewa utawala wa nchi yenu, watu wa nchi hii, wanawake kwa wanaume walisahauliwa kwa muda mrefu lakini nawaahidi muda wenu umefika na hamtasahauliwa tena.
Sherehe hii ya leo inamaana maalum kwetu sote, kwasababu leo hatubadilishi utawala kutoka chama kimoja kwenda chama kingine, bali tunabadilisha utawala kutoka Washington, D.C. na kuurejesha kwenu Wamarekani
Kwa miongo kadhaa tumetajirisha viwanda vya wenzetu kwa gharama ya viwanda vyetu, tumeimarisha majeshi ya wenzetu kwa misaada na vifaa huku tukidhoofisha jeshi letu wenyewe, tumelinda mipaka ya wenzetu na kushindwa kulinda mipaka yetu na kutumia matrilioni ya Dola kuimarisha miundombinu ya nje huku ya kwetu ikizidi kuwa katika hali mbaya
Tumezifanya nchi za wenzetu kuwa tajiri wakati utajiri, uimara wa nchi yetu na kujiamini kwa watu wetu kukipotea mwaka hadi mwaka.
Viwanda vyetu vimefungwa kimoja baada ya kingine, bila kujali mamia ya Wamarekani ambao wamepoteza ajira kutokana na viwanda hivyo kufungwa.
Utajiri wa watu wetu wa maisha ya kati umeporwa na kuwafanya watawanyike dunia nzima kutafuta ahueni ya maisha.
Sasa kila uamuzi utakaotolewa na taifa hili kuhusu kodi, biashara, uhamiaji na masuala ya nchi za nje utafanywa kwa manufaa ya wafanyakazi wa Wamarekani na familia zao kwanza.
Kuanzia siku ya leo na kuendelea, mtazamo mpya utaongoza taifa letu, kuanzia wakati huu na kuendelea kwa kila kitu tutakuwa tukiangalia maslahi ya Marekani kwanza.
Lazima tulinde mipaka yetu dhidi ya uvamizi wa mataifa mengine ambayo matokeo yake ni kudhoofisha viwanda vyetu na kuchukua nafasi za ajira za wamarekani. Tutalinda kila kitu kuhakikisha taifa letu linazidi kustawi na kuwa imara zaidi.
Nitawapigania kwa kila pumzi yangu , na nawaahidi kwamba kamwe sitawaangusha. Marekani itashinda na kuwa na nguvu kama zamani, tutarejesha ajira zetu, tutarejesha mipaka yetu, tutarejesha utajiri wetu na tutarejesha ndoto zetu.
Hotuba ya Trump ni ujumbe tosha kwa waliokuwa wakiitegemea kwani ni dhahiri anakwenda kufyeka misaada yote iliyokuwa ikizinufaisha nchi za Afrika na mabara mengine.
Trump tangu mwanzo alionyesha dhahiri kwamba hana mpango wowote na nchi za Afrika na kwamba kukata kwake misaada kwa
Afrika si jambo la mjadala tena bali litakuwa jambo linalosubiriwa muda tu litimie.
Ni vipi baadhi ya nchi zitaathirika na mtazamo mpya wa Trump kuhusu misaada.
Afrika ya Kusini
Afrika kusini imeweza kujiweka katika hali ya nchi ambayo haihitaji misaada bali mshirika mwenye uwezo na anayejiamini kibiashara .
Lakini mazungumzo magumu na Marekani kuhusu makataba wa fursa ya ukuaji wa kiuchumi wa Afrika (AGOA) mwishoni mwa mwaka jana huenda yalikuwa ukumbusho kwa nchi zinazoendelea kuhusu mahala halisi zilipowekwa kiuchumi na Marekani.
Baaadhi ya wakosoaji wa mapatano ya AGOA wanasema Afrika kusini, kama mataifa mengi ya Afrika, ilikuwa ngao thabiti katika kukubali masharti ambayo hayainufaishi kwa minajili tu ya kupata mshirika thabiti.
Trump ana sifa ya kuwa mfanyabiashara maarufu, na huku haijawa wazi ni sera gani aliyo nayo kwa Afrika kusini, baadhi ya watu nchini humo wana hofu kuwa huenda uhusiano mzuri uliokuwepo baina yao na Marekani ukavunjika.
Wanasema utawala wa mfanyabiashara huyo huenda ukaitaka Afrika Kusini kuonyesha ni kwa nini inafaa kuwa katika kikosi cha Trump.
Nigeria
Tangu kuchaguliwa kwa rais Muhammadu Buhari mwaka jana , Nigeria imeboresha uhusiano na Marekani uliotiwa dosari kubwa na shutuma za ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya Jeshi la Nigeria, hususan katika vita dhidi ya wanamgambo wa Boko Haram.
Jeshi la Nigeria lilipata mafunzo na zana kutoka kwa utawala wa Obama na bila shaka itataka kuendeleza uhusuiano huo ulioboreka. Nigeria pia itataka uhusiano wa kibiashara na taifa lililoimarika zaidi kiuchumi duniani.
Kwa upande mwingine nchi hizi mbili zinaweza kujikuta katika uhasama ikiwa Trump ataamua kuwatambua waasi wanaotaka kujitenga wa Biafra. Pia inasemekana kuna raia wa Nigeria zaidi ya milioni moja wanaoishi nchini Marekani , na baadhi wanahofu kwamba sera za uhamiaji za Trump zinaweza kupelekea maelfu yao kurejeshwa nyumbani.
Uganda
Serikali ya Marekani hutoa msaada wa Dola milioni mia saba ($700m) kwa Uganda kila mwaka. Mingi kati ya misaada hiyo huelekezwa katika mipango ya kuboresha afya, hususan dawa utoaji wa dawa za bure za HIV/Aids kwa wale wanaozihitaji.
Kiasi cha pesa kisichojulikana pia hutolewa kwa ajili ya msaada wa jeshi. Hakuna maelezo yanayotolewa lakini kutokana na kwamba Uganda imeongeza kikosi cha askari wake wa kulinda amani katika mataifa ya kigeni, ikiwemo Somalia na Jamhuri ya Afrika ya Kati, serikali ya Washington imekuwa mfadhili wake mkuu.
Marekani pia imekuwa ikitoa msaada wa mafunzo kwa wanajeshi.
Katika barua ya hivi karibuni kwa Wizara ya Mashauri ya Kigeni, maafisa wa mpito wa Trump walihoji kuhusu shughuli hizi.
Hofu ya Uganda ni kwamba utawala mpya utasitisha ama kupunguza msaada huu .Kwa upande mwingine baadhi ya wapinzani nchini Uganda wamedai kuwa wafadhili wa kimataifa hawakuipatia serikali msaada unaofaa.
Katika sekta ya afya , kupunguzwa kwa msaada kunaweza kuwaacha wengi shakani nchini humo.
Kenya na Somalia
Takriban theluthi moja ya Wakenya 90,000 wanaoishi Marekani ni wahamiaji haramu, kwa mujibu wa kituo cha utafiti cha Pew .
Hii inamaanisha kuwa zaidi ya watu 30,000 wanaweza kurejeshwa nchini Kenya kama Donald Trump atatekeleza ahadi yake aliyoitoa wakati wa kampeni ya kuwarejesha makwao wahamiaji haramu.
Hii itaathiri kwa kiasi kikubwa kipato chao wanachotuma nyumbani kinachokadiriwa kuwa dola milioni sitini ($60m ) kutoka Marekani na Canada mwaka 2015.
Walipokuwa wakitathmini uhusiano baina ya Marekani na Kenya pamoja na Afrika kwa ujumla wasaizidi wa Trump walielezea hofu yao kuhusu hali ya baadaye ya ushirikiano huo.
Walihoji ni kwanini Marekani imekuwa ikipigana na al-Shabab kwa muongo mzima bila kushinda vita hivyo. Na walihoji ikiwa pesa ambazo Washington inatoa kama msaada kwa nchi mbali mbali za Afrika zinatumiwa kwa umakini.
Zimbabwe
Serikali ya Rais Robert Mugabe imesema inatumaini mabadiliko ya hali iliyozoeleka yanaweza kuisasidia kurejesha uhusiano baina yake na Washington. Mugabe na baadhi ya maafisa wake na baadhi ya makampuni yanayomilikiwa na serikali yanakabiliwa na vikwazo vya kusafiri nchini Marekani na kiuchumi tangu wakati wa utawala wa rais George W. Bush' kufuatia madai ya ukiukaji wa haki za binadamu.
Mugabe anaamini vikwazo hivyo vinakiuka sheria ingawa hata hivyo bado Trump hajatoa tamko lolote kuhusu Zimbabwe ama Mugabe na hakuna ishara yoyote kwamba msimamo wake kwa Zimbabwe utatofautiana na ule waliokuwa nao watangulizi wake.
Wakati wa kampeni zake Trump alikuwa akirudia kauli ya kwamba atahakikisha anaweka mazingira magumu kwa waislamu kuingia nchini humo, hali ambayo imewaacha baadhi ya watu njia panda.
Kutekelezwa kwa ahadi hiyo kuna athari mbaya kwa watu wengi duniani kwani kwa watakaokuwa wanataka kuingia nchini humo watafanyiwa vitendo visivyofaa.
Hayo ni pamoja na ukaguzi na uangalizi uliopitiliza wakati wa kuingia kwenye taifa hilo na hali hiyo huenda ikawafanya waislamu wengi kukosa fursa ya kuingia nchini humo.