Walitoa wito huo kwa nyakati tofauti wakati wakizungumza na Nipashe mwishoni mwa wiki.
Baadhi ya wanachama hao walidai baadhi ya viongozi wa vyama hivyo wamekuwa wakitumia madaraka yao vibaya na kujinufaisha binafsi huku makundi lengwa yakiendelea kudidimia.
Mmoja wa wanachama hao, Zakayo John, alisema licha ya vyama vingi kuwa na mtaji mdogo, lakini baadhi ya viongozi wamekuwa wakijinufaisha na kuvididimiza.
Alimuomba Rais Magufuli kutumia vyombo vyake kufanya ukaguzi wa kushtukiza ili kubaini ubadhirifu kwa kile alichosema vingi viongozi wake wamekuwa wakitumia fedha kwa matumizi binafsi.
Naye Rashid Mbegu, mwanachama wa Ushirika wa Kuweka na Kukopa wa Kiroka Saccos, alisema awali vyama hivyo vilikuwa msaada mkubwa kwa wakulima kutokana na kukopeshana na kulipa kwa wakati, lakini hivi sasa vimekuwa tofauti kwani havinufaishi tena walengwa.
“Tunaomba uchunguzi wa kina ufanyike kwenye hivi vyama vyetu, maana yake sasa hatunufaiki navyo tena kama ilivyokuwa awali, mikopo tunaipata kwa shida na kusotea, lakini tunaona viongozi wetu wanajinufaisha tu,” alisema Mbegu.
Kwa upande wake, Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Morogoro, Peter Bayo, alisema ni mkutano mkuu wanachama pekee unaoweza kubaini changamoto za ushirika na kuzitolea maamuzi ya namna ya kuzitatua.
Alisema kama kuna wanachama wanalalamikia viongozi wao waitishe mkutano kwa kufuata taratibu zilizopo na kufanya maamuzi ikiwamo kufanyika kwa kaguzi ndani ya chama badala ya kuishia kulalamikia nje ya mkutano mkuu.