
Thursday, December 15, 2016
Mwenyekiti wa CCM na Rais John Magufuli akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) juzi Ikulu jijini Dar es Salaam. Picha na Ikulu
Kanali huyo, Ngemela Eslom Lubinga, ni mmoja kati ya wana-CCM walioteuliwa kuingia sekretarieti ya CCM kujaza nafasi zilizokuwa wazi baada ya waliokuwa wakizishikilia kupewa majukumu mengine. Nafasi yake ilikuwa inashikiliwa na Dk Asha-Rose Migiro aliyeteuliwa kuwa balozi nchini Uingereza.
Wengine walioteuliwa ni Rodrick Mpogolo, ambaye anakuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara kushika nafasi ya Rajabu Luhwavi aliyeteuliwa kuwa balozi, na Humphrey Polepole (Katibu wa Halmashauri Kuu-Itikadi na Uenezi) kujaza nafasi na Nape Nnauye ambaye amekuwa Waziri wa Habari.
Kabla ya uteuzi huo, Polepole alikuwa mkuu wa wilaya mpya ya Ubungo.
Uteuzi wa Kanali Lubinga ndio ambao umeibua mjadala, hasa kwenye mitandao ya kijamii, wengi wakiuliza alijiunga lini na CCM hadi kufikia hatua ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo nyeti ya utendaji wakati amekuwa jeshini hadi mapema mwezi huu.
“Mimi nimestaafu tangu tarehe 2, Desemba, sijui nimeongea lini, lakini ndiyo nimestaafu na hapa niko Mkoa wa Kagera nimekuja kusalimia,” alisema Kanali Lubinga alipozungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana.
Kanali Lubinga alisema amekuwa mwanachama wa CCM tangu mwaka 1979 na hata mfumo wa vyama vingi uliporejeshwa mwaka 1992, kadi za maofisa wa jeshi hazikutupwa bali zilihifadhiwa kwenye mafaili yao.
“Sisi wanajeshi zamani tuliruhusiwa kuwa wanachama wa CCM. Baada ya mfumo wa vyama vingi kuingia, kadi zetu hazikutupwa bali ziliwekwa kwenye mafaili. Wanajeshi wote waliokuwa wana-CCM kadi zetu ziliwekwa kwenye mafaili yetu, hazikutupwa,” alisema.
“Mimi ni mwanachama tangu mwaka 1979, nimeendelea kutoka pale nilipoishia. Mtu anapostaafu anaweza kujiunga na chama chochote. ”
Kuhusu nafasi ya ukuu wa wilaya aliyowahi kuishika kabla ya kurudishwa jeshini, Kanali Lubinga alisema: “Yale ni mamlaka ya Serikali kama vile makatibu wakuu wa wizara, siyo siasa.”
Vifungu vya Katiba
Lakini ibara ya 147 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inakataza watumishi wa majeshi ya ulinzi na usalama kujihusisha na siasa.
“Itakuwa ni marufuku kwa mwanajeshi yeyote kujiunga na chama chochote cha siasa, isipokuwa tu atakuwa na haki ya kupiga kura iliyotajwa katika ibara ya 5 ya Katiba hii,” inasema ibara ya 147 (3) ya Katiba.
Ibara ndogo ya nne inamuelezea mwanajeshi kuwa ni “askari aliyeajiriwa kwa masharti ya muda au ya kudumu katika Jeshi la Ulinzi, Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza au Jeshi la Kujenga Taifa”.
Waraka wa Utumishi wa Umma wa mwaka 2015, pia umekataza watumishi wa umma, wakiwemo waajiriwa hao wa vyombo hivyo vya dola kuwa wanachama wa vyama vya siasa, ila wanaruhusiwa tu kupiga kura.
Waraka huo namba moja wa mwaka 2015 ulitolewa kuweka mwongozo kwa watumishi wote wa umma ambao wangependa kugombea nyadhifa za kisiasa katika ngazi mbalimbali, lakini unataja “askari wote walio kazini wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Polisi, Magereza, Uhamiaji na Zimamoto; majaji na mahakimu katika ngazi zote” hawaruhusiwi kugombea.
Tangu aapishwe Novemba 5 mwaka jana, Rais John Magufuli amekuwa akiteua wanajeshi kushika nafasi katika ngazi kama za ukuu wa mikoa, ukatibu wa wizara, uenyekiti wa bodi, ukuu wa wilaya na ukatibu tawala wa mikoa na wilaya, na wakati fulani aliwahi kueleza kuwa anafanya hivyo ili kuingiza nidhamu ya jeshi.
Suala la Lubinga si geni. Katika uchaguzi wa mwaka 2010, mkuu wa zamani wa majeshi, Jenerali Robert Mboma baada ya kustaafu aliingia kwenye kinyang’anyiro cha ubunge akaenguliwa ndani ya CCM.
Pia kamanda wa zamani wa polisi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alfred Tibaigana alijitosa kwenye kinyang’anyiro cha ubunge wa Muleba Kusini mwaka 2010 baada ya kustaafu kazi hiyo mwaka 2008
Mwaka jana, aliyekuwa Jaji Mkuu, Augustino Ramadhan aliingia kwenye mbio za urais ndani ya CCM ikiwa ni muda mfupi baada ya kustaafu, jambo lililoibua mjadala uliozimika baada ya kuenguliwa.
Mwaka jana pia, Dk Ackson Tulia aliingia kwenye mchakato wa uspika wa Bunge kwa tiketi ya CCM, kabla ya kujitoa na baadaye kupitishwa kuwania nafasi ya Naibu Spika, ambako alikutana na maswali kuhusu uanachama wake, lakini Spika Job Ndugai akayazima.
Maoni ya wadau
Uteuzi huo umekosolewa na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu aliyesema umekiuka Katiba.
“Huyu Kanali Lubinga alijiunga na CCM lini ili awe na sifa ya kuteuliwa leo kuwa katibu wa mambo ya nje? Ameingia CCM lini? Katiba imesema ni marufuku kwa mwanajeshi kujiunga na chama cha siasa,” alisema Lissu jana.
“Yeye amestaafu lini? Hata kama alikuwa mwanachama tangu miaka ya 1970, Katiba imesema ni marufuku. Iwe ni mwanachama mfu, au aliye kwenye coma (aliyepoteza fahamu) au vyovyote. Katiba inasema ni marufuku,” alisema Lissu.
Hoja kama hiyo ilisemwa na mhadhiri wa Sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Onesmo Kyauke.
“Japo sheria inaruhusu mwanajeshi aliyestaafu kujiunga na chama cha siasa, bado kuna haja ya kuyatenga majeshi na vyama vya siasa ili kutoathiri utendaji,” alisema Dk Kyauke.
“Kama amestaafu kisheria haina tatizo, lakini inabidi sheria zetu zirekebishwe ziwe kama za Marekani ambazo wanajeshi wanatakiwa wakae miaka mitatu wanapostaafu kabla ya kujiunga na siasa. Kwa sababu anaweza kufanya upendeleo kwa chama tawala ili akistaafu ateuliwe,” alisema.
“Si majeshi tu, hata majaji hawatakiwi kuwa karibu na vyama vya siasa hata wakistaafu, kwa sababu wanaweza kufanya upendeleo ili wakistaafu tu wateuliwe kwenye nyadhifa za vyama hivyo.”
Hata hivyo, akizungumza kwa njia ya simu na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani (DW Kiswahili), mwandishi wa habari mkongwe Jenerali Ulimwengu alisema si jambo geni kwa maofisa wa JWTZ kupewa vyeo CCM.
“Kwanini? Kwa sababu ni kanali? Wamekuwepo makanali na maofisa wengine wa majeshi ndani ya CCM. Katibu Mkuu Kinana (Abdulrahman) ni Kanali, kwa hiyo hakuna jambo jipya lililofanyika katika hili?”
Mabadiliko ndani ya CCM
Kwa upande mwingine, akizungumzia mabadiliko yaliyofanywa na Halmashauri Kuu ya CCM hivi karibuni, Ulimwengu alisema ni mwendelezo wa mkakati wa Rais John Magufuli kubana matumizi.
“Ni kupunguza matumizi yasiyokuwa na muhimu yasiyokuwa na maana na kuondoa nafasi za uongozi ambazo hazikuwa na sababu yoyote lakini zinachukua fedha nyingi na kuondoa watu ambao wapowapo tu, lakini hawajulikani wanafanya nini,” alisema.
Aliongeza kuwa mabadiliko hayo yataendelea kwa ajili ya chaguzi zijazo kwa kuwa Rais Magufuli alisema kuna wasaliti ndani ya chama.
“Rais mwenyewe alipochaguliwa mwaka jana, alikuwa akisema amebaini ndani ya CCM wapo wasaliti wanaounga mkono wagombea wa vyama vingine na ndipo alipozungumzia habari ya kutumbua majipu. Nadhani katika hilo atakuwa ameona watu waliokuwa kwenye makundi ndiyo walikuwa wakikiumuiza chama,” alisema Ulimwengu.
Lakini Dk Kyauke anayachukuliwa mabadiliko hayo kuwa na athari.
“Japo kupunguza wajumbe wa Halmashauri Kuu hadi 150 ni kubana matumizi na hivyo kuwa kuwa rahisi kuwa-manage (kuongoza), (kufanya hivyo) ni kupunguza nguvu ya uamuzi,” alisema Dk Kyauke.
“Unakumbuka ule uongozi wa (mwenyekiti wa zamani wa wa Chama cha Mpira wa Miguu, Muhidin) Ndolanga? Ilikuwa vigumu kuuondoa madarakani kwa sababu wajumbe walikuwa wachache na hivyo ilikuwa rahisi kuwarubuni. Kwa hiyo ndani ya CCM itakuwa rahisi kuwarubuni wajumbe, sauti ya wanachama haitasikika sana.”
Uteuzi wa Polepole
“Inasemekana kigezo kilichotumika ni kuwa alishiriki ipasavyo Bunge la Katiba. Binafsi sioni kigezo hicho ni sahihi,” alisema mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI), Dk Jimson Sanga.
“Nilitarajia kusikia kwamba uanachama wake wa muda mrefu, uongozi wake hasa ndani ya UVCCM na uwezo wake wa kukijua chama hicho ndio vimempa sifa ya kushikilia nafasi aliyopewa. Wanapaswa kuteua kwa umakini ili wanachama wasihisi kuna upendeleo.”
Source: Mwananchi
