» »Unlabelled » Mbinu za Kupata Mtaji wa Biashara

ILI UPATE HABARI ZETU KWA URAHISI BOFYA HAPA KUINSTAL APPLICATION YA MZALENDO HURU KWENYE SIMU YAKO

Watu wengi wanatamani kumiliki biashara siku moja na huenda wana mipango mizuri juu ya bishara zao. Mipango hii inaweza ikawa vichwani tu au mingine katika maadishi lakini inapofika wakati wa utekelezaji wa mipango hii ukosefu wa mtaji wa biashara hiyo ni kipingamizi kwa wengi.

Lakini kuna jinsi kadhaa ambazo zinaweza kusaidia upatikanaji wa mitaji kwajili ya biashara.

 Aina Za Mitaji
Kuna aina mbili ya mitaji kwaajili ya biashara au uwekezaji wa aina yoyote.


  • Mtaji wa Mkopo
  • Mtaji wa Mmiliki

 Mtaji wa Mkopo unakuwezesha kukopa toka kwa taasisi za fedha au mtu binafsi wakiwemo ndugu ,jamaa na marafiki na kuhitajika kulipa katika kipindi maalumu ikiwa pamoja na riba au bila riba.

Aina hii ya mtaji inakuwezesha kufanya biashara lakini ni lazima uwe makini katika utunzaji wa fedha zako na uzalishaji wake kwani mwishowe utahitajika kurudisha fedha zote pamoja na riba pengine kila mwezi.

 Mtaji wa Mmiliki ni mtaji toka kwa mtu au kampuni ambayo inahitaji kuwa na umiliki wa sehemu ya bishara. Hawa wanataka kupata faida kutokana na uwekezaji katika kampuni au biashara yako.

Kama uko tayari kutoa sehemu ya umiliki wa biashara yako basi mtaji wa aina hii utakusaidia kuanzisha au kuboresha bishara yako.

Changamoto Za Kupata Mitaji:
Kupata mtaji wa biashara ni changamoto kubwa kwa wajasiriamali kote duniani. Japo fedha za mikopo zinapatikana katika mabenki lakini bishara nyingi hazina miundo mizuri na mifumo ya fedha kuwezesha kupata mikopo. Benki zimekuwa na masharti magumu sana kiasi kwamba bishara nyingi haziangalii huko kama sehemu ya kupata mikopo.

Mikopo toka kwa ndugu na jamaa pia ina changamoto zake,si rahisi ndugu au rafiki akakuamini au akaamini kuwa biashara yako itafanikiwa,tunajua asilimia 90 za biashara zinazoanza zinakufa kila mwaka. Hili linawapa wasiwasi sana wakopeshaji.

Mambo Ya Kuangalia Kabla Ya Kupata Mtaji



Mtaji Toka Kwenye Mikopo:
Ili kupata mikopo kunahitajika dhamana kuwahakikishia wakopeshaji wako kuwa kama hutafanikiwa basi ni kwa jinsi gani fedha zao zitarudi.

Na utakutana na msharti mengi magumu,dhamana inaweza kuwa kama ifuatavyo:

  • Nyumba
  • Kiwanja
  • Shamba
  • Gari
  • Mali za nyumbani au ofisini(biashara yenyewe)
  • Ni lazima ujiulize mapema kama uko tayari kuweka mojawapo ya vitu hivi kuwa dhamana.


Kwa namna hii ni rahisi kupata mkopo na ni lazima urudishe deni vinginevyo utapoteza.

Huu ndio ujasiriamali wenyewe, uthubutu wa kufanya mambo ya hatari katika harakati za kufanikiwa katika biashara.



Mtaji Toka Kwa Wawekezaji:
Kama utaamua kuingiza wawekezaji wengine katika biashara yako basi pia nilazima ufikirie mapema kuwa kutakuwa na taarifa ambazo watahitaji kujua juu ya mwenendo wa biashara yako.


  • Je unapata faida kwa sasa?
  • Muelekeo ukoje,unapanda na bidhaa au huduma zinahitajika?
  • Ni kwa namna ipi fedha zinzohitajika zitawekezwa ili kuboresha biashara na kuleta faida kwa haraka n.k
  • Waekezaji nao wanaangalia hatari ya kupoteza fedha zao na pia muda wa kurudisha fedha wanazowekeza na faida itakayozalishwa.


Kama biashara yako haiwezi kuonyesha haya kabla,ni ngumu kupata wawekezaji katika bishara yako.

Mpango Bishara na utunzaji mzuri wa mahesabu ya biashara yako yatasaidia sana kutoa taarifa hizi na hivyo kukusaidia kupata wawekezaji

Taarifa Za Fedha Na Mpango Wa Bishara Ni Nyenzo Muhimu Kupata Mtaji Wa Biashara
Kama ni niashara mpya ,kutahitajika kuwa na mpango wa biahsara,andiko ambalo linaelezea jinsi ambavyo biashara yako itafanyika ,kiasi cha fedha kinachohitajika, bidhaa na huduma utakazo toa ,masoko,na wafanyakazi.


Andiko hili litasaidia kushwawishi wawekezaji na watoa mikopo.
Kama biashara yako iko tayari na unataka kuongezea mtaji, basi utahitaji kuwa na taarifa za hali ya fedha ya bishara yako, pia unaweza ukaandaa mpango wa biashara unaoelezea mwelekeo wa biashara katika miaka kadhaa mbele.

Wafanyabishara wengi wa kati na wa chini hawafanyi haya, ndio maana kunakuwa na ugumu kupata mitaji ya kuanzia au kukuza biashara.

Huenda ukahitaji msaada toka kwa wataalamu wa biashara na upate usaidizi wa kitaalamu,andaa fedha kidogo kwajili ya huduma hizi. Kuna makampuni mengi tu sasa hivi ambayo yanatoa huduma kwa wafanyabiashara kwa gharama ndogo.

Mbinu 5 Za Kupata Mtaji Wa Biashara:
Aina hizi zote za kupata mitaji zinaingia katika makundi mawili yaliyotajwa hapo awali aidha ni mkopo au uwekezaji

1. Mkopo Toka Benki Au Tasisi Za Mikopo
Benki zote hutoa mikopo kwaajili ya biashara ila taarifa za muhimu zinahitajika kuhusu mwenendo wa biashara kama tayari imeshaanza au Mpango wa biashara unaoelezea jinsi ambavyo biashara itaendeshwa na jinsi ambavyo deni litalipwa.

Benki huhitaji vitu vya thamani kwajili ya dhamana ya fedha watakazokupa kama mtaji.

Iwapo fedha hazitarudishwa kama ambavyo iliwekwa katika masharti ya mkopo basi mali hiyo itauzwa ili kufidia deni.

Hili limekuwa ni changamoto kwa wengi kupata mikopo toka benki. Hasa kwa biashara anbazo zinaanza na hazina uhakika wa kufanya vizuri na uwezo wake wa kurudisha deni.

Aina hii ya mikopo inaweza ikawasaidia wale ambao bishara zao zimeshasimama na wanafanya kwa faida. Pia kwa zile biashara ambazo mzunguko wa fedha ni mkubwa na hawatahitaji muda mrefu wa kulipa deni.

Benki mpya mara nyingi huwa na msharti rahisi kuliko benki kongwe.
Aina nyingine ya mikopo ambayo inafanana na ile ya benki ni toka katika taasisi za mikopo. Taasisi hizi zinatoa masharti nafuu kido kuliko yale ya benki. Nchini Tanzania kuna tasisi maarufu kama FINCA,Blue ,Branc na nyingine nyingi ambazo zinatoa mikopo ya biashara.

Mara nyingine utahitaji kuwa katika vikundi ili kupata mikopo kwa urahisi au kuwa na biashara iliyosajiliwa kisheria.

2. Mkopo Toka Kwa Ndugu, Jamaa Au Marafiki
Ndugu na Marafiki ni sehemu nyingine ambayo unaweza kufikiria unapohitaji mtaji wa biashara.

Ni watu wanaokupenda na kukuamini na wako tayari kukusaidia katika harakati zako za kufanikiwa kibiashara. Wako tayari kukusaidia kama wana uwezo wakufanya hivyo. Lakini bado wanahitaji uhakika kuwa fedha zao zitarudi. Watapenda kujua mpango wako na ni lazima uwe tayari kuwajulisha,sio tu kabla hata baada ya kupata mkopo ili wajue mwenendo wa fedha zao.

Kumbuka dhamana hapa haitakuwa mali bali uaminifu wako kwao. Ukishindwa kufanya ulichoahidi utavunja uhusiano wenu mzuri uliojengeka kwa muda mrefu.

Ni vyema kufikiria kwa makini kama utahitaji kuchagua njia hii,vinginevyo si njia nzuri sana.


3. Toka Katika Vikundi Vya Kuweka Na Kukopa
Vyama vya Kuweka na Kukopa vinatoa mikopo kwa wanacama wake. Katika vyama hivi wanachama wanatakiwa kuweka fedha katika akaunti zao. Mwanachama anaruhusiwa kukopa kulingana na kiasi alichoweka. Baadhi ya vyama vinaruhusu mwanachama kuchukua mkopo kufikia mara nne ya kiasi alichoweka. Mkopo huu huwa na riba ndogo ulilinganishwa na benki.

Pia masharti yake si magumu na ya hatari kama ya benki.

Kuna vikundi vingine vya kijamii ambavyo wanachama wamekuwa wakifanya hivyo na vinatoa fursa kwa wanachama kupata mitaji kwa kukopa.

Vikundi vya Kuchangiana:
Pia kuna mtindo wa kuchangiana kila mwezi ambapo wanachama katika kikundi watachanga kiasi fulani cha fedha na kumpa mmoja wao ili afanya kitu fulani muhimu ambacho asingeweza kwa kuwekeza binafsi.


4. Mtaji Toka Kwa Wawekezaji Binafsi Wa Nje
Kuna watu binafsi na makapuni ambayo tayari yanafedha na yanahitaji kuwekeza katika biashara yenye kupata faida ili fedha zao ziongezeke. Watu hawa wanaweka fedha benki ambako hazizai kwa riba nzuri kulinganisha na biashara.

Watu hawa wanahitaji taarifa za kutosha kuwashawishi kuwa fedha zao ziko katika mikono sahihi. Pia hata baada ya kuwekeza watahitaji taarifa za mara kwa mara juu ya maendeleo ya biashara. Kama biashara ni mbaya huenda wakatoa fedha zao ili wasipate hasara.

Hii ni sehemu nyingine ambayo huwa haiangaliwi sana na wajasiriamali wadogo kwani ile dhana ya kufanya biashara kwa kushirikiana bado haijakubalika na kufuatwa. Lakini njia hii inatoa nafasi kwa wale ambao wanabiashara yenye mfumo mzuri na inakosa mtaji tu kufanikiwa.

Lakini hata kwa biashara zinazoanza, kama kuna mpango mzuri na wazo lenyewe la bishara linaonyesha kufanikiwa basi wawekezaji hawa watakuwa tayari kuwekeza katika biashara yako.

Hii ni njia nzuri kwa wale wenye uwezo wa kubuni biashara nzuri zenye kutoa huduma kwa watu na yenye nafasi kubwa ya mafanikio lakini wanakosa fedha za kuanzia. Hawa wanaweza wakaanza hata bila kuwa na shilingi moja,mpango wa biashara pekee ndio wanachohitaji.

Kisha ongea na matajiri katika mji wako(angalia usitoe taarifa zote za mpango wako mpaka upate uhakika kuwa utapata fedha-kuzuia kuibiwa mawazo).


5. Uwekezaji Binafsi (Kuweka Akiba)
Inasemekana kuwa zaidi ya asilimia 50 ya bishara ndogo zonazoanzishwa huanza kutokana na akiba binafsi ya wamiliki.

Mmiliki kupitia nyenzo zilizopo za kupata kipato kama ni kazi au biashara nyingine iliyosimama tayari anaweka akiba maalumu kwajili ya kuanzisha biashara mpya. Kiasi cha kuanza kikifikiwa basi fedha hizo zinaingizwa katika biashara mpya.

Fedha hizi zinaweza zikaingizwa kama mkopo binafsi ambapo baadae zitarudishwa katika akaunti binafsi ya mmiliki au zikaingia kama uwekezaji katika biashara ambapo mmiliki atapata faida tu itakayozalishwa.

Vyovyote vile njia hii ni nzuri kwani hakuna madeni toka nje na unaweza ukawa na amani sana katika uendeshaji wake.

Kama wewe ni mwajiriwa na unafikiria kuwa na bishara yako basi njia hii ya kuweka akiba kwajili ya bishara yako ni njia sahihi.

Unaweza ukafungua akaunti nyingine nje na ile ya kawaida na kuhamisha asilimia fulani kila mwezi kwenda katika akaunti hiyo ya biashara (10-25% ni kiwango kizuri)

Ukitaka Mafanikio Ni Lazima Uchukue Hatua Za Haraka
Imesemwa kuwa usisubiri hadi kila kitu kikamilike ndio uanze,katika biashara hiyo inaweza kuwa ngumu au ikakufanya usianze kabisa.

Kama tayari una mpango wa bishara unaovutia usisite kuanza kwa kukosa mtaji,chagua njia mojawapo ya kupata mtaji na uanze.

Ukitaka kupanda jengo la ghorofa ndefu,anza ngazi ya kwanza na utajikuta uko juu .
Ukisubiri kufanya yote kwa mara moja huenda usifanye kabisa. Unapoanza kufanya kitu unapata urahisi kwa jinsi ambavyo unaenda mbele na njia inakuwa wazi kwako katika kila hatua unayochukua.


Nawatakieni biashara na mafanikio mema!
ILI UPATE HABARI ZETU KWA URAHISI BOFYA HAPA KUINSTAL APPLICATION YA MZALENDO HURU KWENYE SIMU YAKO

About Unknown

About Mzalendo Huru Staff:

Send us your articles, questions, feedback, suggestions, press releases and all others to Whats app on +255657905751
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post