» »Unlabelled » Hasara mil. 308/- kuungua soko la Mandela

ILI UPATE HABARI ZETU KWA URAHISI BOFYA HAPA KUINSTAL APPLICATION YA MZALENDO HURU KWENYE SIMU YAKO

HASARA ya mali iliyosababishwa baada ya kuteketea soko kuu la wakulima la Nelson Mandela lililopo katika Kata ya Mazwi, Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa ni zaidi ya Sh milioni 308.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Sumbawanga, Saad Mtambule alilieleza gazeti hili jana wakati Mbunge wa Sumbawanga Mjini , Aesh Hilaly (CCM) , Mbunge wa Viti Maalumu, Aida Khenan (Chadema ) na Meya wa Manispaa ya Sumbawanga, Justine Malisawa walipowatembelea na kuwapa pole walioathirika na kuteketea kwa soko hilo.

Mtambule alisema vibanda vya biashara vipatavyo 900 vilivyokuwa ndani ya soko hilo viliteketea kwa moto na kwamba wafanyabishara 3,000 waliokuwa wakifanya biashara ndani ya soko hilo wameathirika na tukio hilo.

Alisema kuwa hasara hiyo ni kutokana na tathmini iliyofanywa na timu ya wataalamu iliyoundwa na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga , Dk Halfani Haule.

Moto huo uliodumu kwa zaidi ya saa nane uliwaka Oktoba 29, mwaka huu na kuteketeza maduka na vibanda vya biashara vilivyomo ndani ya soko hilo ambalo ni la pili kwa ukubwa na umaarufu katika mji wa Sumbawanga baada ya soko kuu lililopo Kata ya Mazwi.

Soko hilo linapakana na Uwanja wa Michezo wa Nelson Mandela ambao haukupata uharibifu wowote.

Mwenyekiti wa soko hilo, Christopher Ntondonkoswe alilieleza gazeti hili kuwa baada ya kuteketea soko hilo kwa moto wafanyabiashara walitengewa maeneo mawili ukiwemo uwanja Sabasaba unaomilikiwa na CCM na eneo la Sabato lililokuwa dampo kwa muda.

Wafanyabiashara hao walipotembelewa jana na wanasiasa hao katika maeneo yao hayo waliwaeleza kuwa wako tayari kulijenga upya soko lao lililoteketea kwa moto wao wenyewe iwapo kama serikali itaandaa michoro ya soko la kisasa.

Wabunge hao waliwataka waathirika hao wajiunge katika vikundi ili waweze kuona namna ya kuwasaidia huku Aesh akimtaka Meya awafukuze mara moja watu ambao si waathirika ambao wamejenga vibanda katika maeneo hayo na kuwapangisha waathirika.

Kwa mujibu wa Meya Malisawa, soko la Mandela linamilikiwa na Manispaa ya Sumbawanga na lilianzishwa rasmi mwaka 2011.

“Soko la Mandela lilikuwa chanzo kikubwa cha mapato ya ndani, kuteketea kwake kumeisababishia Manispaa hasara kubwa, kwani kwa siku tulikuwa tunakusanya kati ya Sh 700,000 na Sh milioni moja,” alieleza Meya huyo.

ILI UPATE HABARI ZETU KWA URAHISI BOFYA HAPA KUINSTAL APPLICATION YA MZALENDO HURU KWENYE SIMU YAKO

About Unknown

About Mzalendo Huru Staff:

Send us your articles, questions, feedback, suggestions, press releases and all others to Whats app on +255657905751
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post